Habari

TRA tunda adhimu la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar 1964-2019

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

APRILI 26, mwaka 1964 waasisi wa Muungano wa Tangayika na Zanzibar, hayati Mwalimu Julias Kambarage Nyerere na marehemu sheikh Abeid Amani Karume, walichanganya mchanga kama ishara ya kuziunganisha nchi zao.

Kila mmoja alilazimika kupoteza hadhi na heshima ya nchi yake, na kisha mataifa hayo mawili kuzaliwa upya, na leo tukisherehekea miaka 55 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maana historia zisizo na shaka zinaeleza wazi, kuwa kabla ya Aprili, 26 Zanzibar, ikijulikana kama Jamhuri ya watu wa Zanzibar, na kule Tanzania bara kulijulikana kama Jamhuri ya Tanganyika.

Mitandao ya kijamii, inabaisha kuwa, ilithibitishwa na bunge la Tanganyika kwa wakati huo na Baraza la la Mapinduzi kuwa, Aprili 26 na Aprili 27, mwaka 1964 viongozi walikutana ukumbi wa Karimjee jijini Dar-es Salaam kwa lengo la kubadilisha hati za Muungano.

Mitandao inaendelea kutupasha kuwa, dola hizo mbili zilibadilishwa jana mnamo Oktoba 28, mwaka 1964 na sasa kutambulika rasmi kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ambapo jina hilo lilizaliwa kupitia sheria ya Muungano namba 61 ya mwaka 1964 ambapo wakati hayo yanafanyika tayari viongozi hao walishawatimua watawala wa kigeni katika mataifa yao.

Inaelezwa kuwa hati za makubaliano hayo ya kisheria, yaani ya Muungano wa Tangayika na Zanzibar yalitiwa saini na rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Nyerere sambamba na rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Sheikh Abeid Amani Karume, Aprili 22, 1964.

Hapo sasa kilichofuata kwa vile waasisi hawa walikuwa wanaelewa wanachokifanya, ndipo Aprili 27, mwaka 1964 viongozi hao wakabadilisha hati za Muungano.

Tena kubwa zaidi na zuri, katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaani ile ya mwaka 1965, iliainisha mambo 11 kwamba yawe ndio ya Muungano baina ya Zanzibar na Tanganyika kwa wakati huo.

Moja na kubwa zaidi ni Katiba yenyewe ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mambo ya nchi za nje, Ulinzi, Polisi, Mamlaka ya juu ya mambo yanayohusika na hali ya hatari, uraia, uhamiaji, mikopo na biashara za nje.

Mambo mengine ambayo pia yamo kwenye katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ukurasa wa mwisho ni utumishi wa Muungano, kodi za mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika. Ushuru wa forodha na ule wa bidhaa zinazotengenezwa Tanzania na unaosimamiwa na Idara ya forodha.

Jengine ni bandari, mambo yanayohusika na usafiri wa anga, posta na simu, ingawa kwa sasa mambo kutoka 11 na kufikia 22 kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania.

Jambo la mwisho la 22 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao mwaka huu wa 2019 unatimiza miaka 55, ni lile lililoingizwa mwaka 1992, kufuatia kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi, ambalo ni uandikishaji wa vyama vya siasa.

Zanzibar imekuwa ikitajwa na baadhi ya wasiofahamu mambo kwamba, ndani ya miaka hii 55 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kwamba inayonywa na kuchukuliwa uchumi wake.

Lakini nakumbuka sana maneno ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Zanzibar dk: Ali Mohamed Shein, kwamba Muungano huu unafaida lukuki kwa Zanzibar.

Moja akisema kuwa, wanafunzi wa elimu ya juu ambayo ni jambo la 14 kati ya yale 22, wamekuwa na fursa ya kukopa fedha za kujisomeshea kwenye mifuko mwili.

Maana Zanzibar ipo bodi ya mikopo ya elimu ya juu, ambayo inatoa mikopo kwa wanafunzi wa Zanzibar pekee, lakini na ule mfuko wa elimu ya juu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kwa ajili ya wanafunzi wote.

Kubwa zaidi na la kujivunia na pengine ndio tunda adhimu na adimu la Muungano wa Tangayika na Zanzibar, tena kwa hasa kwa Zanzibar ni kuwepo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA.

Ambapo hichi ni chombo cha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kipo hadi Zanzibar na miongoni mwa kazi zake ni kusimamia kodi kwa niaba ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Suala la kodi ya Mapato yanayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini Tanzania unaosimamiwa na Idara ya forodha ni jambo la 10 kwamba ni la Muungano.

Ndio maana hapa kwa kodi zile ambazo hazikusanywi na Bodi ya Mapato Zanzibar ZRB, basi chombo hichi cha Muungao wa Tanganyika na Zanzibar cha TRA ndio hubeba kazi hiyo.

Tena aliwahi kusema na ndio ilivyo, rais wa Zanzibar dk Ali Mohamed Shein, kwamba fedha zote zinazokusanywa na TRA Zanzibar zinaingia kwenye mfuko mkuu wa hazina wa SMZ.

Hapa ndio wanaojua mambo, wakisema kumbe azma na nia ya kweli ya viongozi wetu na waasisi wa Muungano huu, waliungana kwa nia safi na ya kweli.

Hata mjumbe wa baraza la Mapinduzi na mjumbe wa baraza la Wawakilishi Zanzibar Said Soud Said, aliwahi kusema kwenye moja ya mikutano yake, kule Kengeja Mkoani kuwa, muungano huu ni adimu duniani kote.

TRA ambayo watendaji wake waliopo Zanzibar, majengo, vitendea kazi na huduma nyingine zote licha ya kutolewa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini mapato wanayoyakusanya hubakia Zanzibar.

Ndio maana juhudi kubwa zilizochukuliwa na Serikali katika kuimarisha uchumi zimewezesha kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato

Na jumla ya shilingi bilioni 548.571 zilikusanywa katika mwaka 2017 ikilinganishwa na shilingi bilioni 487.474 zilizokusanywa katika mwaka 2016.

Hivyo kwa kule ZRB kushirikiana na TRA katika makusanyo ya mapato na ushuru mwengine, katika mwaka 2017, mapato yameongezeka kwa shilingi bilioni 61.097, ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi cha mwaka 2016, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 12.5.

Kwa kazi hii, ndio maana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar dk Ali Mohamed Shein, akatoa pongezi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ‘TRA’ na Bodi ya Mapato Zanzibar ZRB, kwenye hutuba yake kilele cha miaka 54 ya Mapinduzi Zanzibar.

Kwa kuwepo kwa TRA Zanzibar kama tunda la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambao sasa unatimiza miaka 55, tokea ulipoasisiwa kwakwe Aprili 26, 1964, hata pato la taifa limeongezeka kutoka thamani ya shilingi bilioni 2,308 mwaka 2015 na kufikia thamani ya bilioni 2,628 kwa mwaka 2016.

Tena pato hilo lilikadiriwa kufikia shilingi bilioni 2,827, mwaka 2017, kwa bei za soko na katika jitihada zilizochukuliwa mwaka 2011/2012, hivi sasa, utegemezi wa bajeti umepungua kwa mwaka.

Maana 2017/2018, umefikia asilimia 7.3, ikilinganishwa na asilimia 30.2 katika mwaka 2010/2011, ambapo mafanikio hayo hasa kwa nchi inyoendelea ni makubwa.

Uwepo wa Muungano huu, unaweza kuwa chanzo kikubwa pia hapa Zanzibar kwa ukuaji wa uchumi, kwa bei halisi, maana imekua kwa asilimia 7.0 kwa mwaka 2017.

Tena ikilinganishwa na asilimia 6.8 kwa mwaka 2016, idha, pato la mtu binafsi nalo limeongezeka na kufikia shilingi 1,806,000 ikilinganishwa na shilingi 1,632,000 kwa mwaka 2015.

Omar Haji Machano ambae ni mfanyabiashara wa chakula Mkoani Pemba, anasema Muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar, umekubali sasa kusikiliza kilio chao cha kulipa kodi mara mbili.

“Maana ilikuwa ukichukua bidhaa kutoka Mbeya, ukifika bandari ya Dar-es Salaam unalipa, na ukifika Unguja Malindi unalipa naona sasa hili silioni tena,”alieleza.

Hata Mmanga Hassan Shaib anaefanya biashara ya vyombo vya plastiki, anasema hata hiyo TRA imekuwa na utaratibu nzuri wa utoleshaji kodi, na hasa kwa vile wao huangalia faida zaidi.

Nakumbuka sana Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anasema changamoto za Muungano zimekuwa zikichambuliwa kila siku.

“Unajua Muungano huu umeasisiwa na wanaadamu hautaacha kuwa na kasoro, na ndio ambazo watendaji wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale wa Zanzibar hukutana kila wakati,”anafafanua.

Matunda ya vikao hivyo, hutajwa kuwa pamoja na kuondolewa kwa mafuta na gesi na kupunguza gharama za VAT kwa bidhaa zinazozalishwa nchini, sambamba na uondoaji wa kodi mara mbili kwa wafanyabiashara wa Zanzibar.

Hongera hayati Mwalimu Nyerere na hongera marehemu sheikh Abeid Amani Karume kwa kuuwasisi Muungano huu April, 26 mwaka 1964 na leo mwaka 2019 twatimiza miaka 55.

Mwisho

PembaToday

Share: