Habari

TUKAE MGUU SAWA 2015

salam wana mzalendo.

Kwa hapa kwetu Zanzibar huu mwaka 2015 ni muhimu sana kwetu na ni lazima tukae mguu sawa.

Kuingia kwa mwaka huu kunahitimisha ile miaka yetu 50 ya Mapinduzi na tunaanza awamu nyengine. Tunaanza kuhesabu moja kuelekea tena miaka hamsini mengine. Tumshukuru mungu kwa hilo.

Naam tuna mengi ya kujikumbusha mwaka huu.

Wadau msisahau ile dhana ya mamlaka kamili bado iko na inaendelea, safari ilianzia tarehe ya kura ya maoni ya kuunga mkono GNU 2009 na inaendelea sasa. Kila mmoja atumie nafasi yake kuhakikisha lengo hilo linafikiwa hapo mbele kidogo.Kuna haja ya wadau wote kujipanga na kutotetereka.

Msisahau ndoto ya kuwa na maamuzi yetu kwa ajili yetu na vizazi vijavyo na msisahau kuwa hatua hiyo itapatikana kwa kushiriki na kuamua ilivyo kupitia michakato ya katiba mpya na uchaguzi mkuu 2015. tumejipangaje kuzuia kila aina ya hila na hadaa? tukae mguu sawa.

Msisahau kuwa kuna wazanzibari wenzetu walitangulia mbele ya haki kwa kushiriki katika harakati za kutaka mageuzi kwa njia mbali mbali, hawa tusiwasaliti leo na kesho, madhali kumekuja njia sahihi za kutaka mabadiliko basi tuwaunge mkono watu wetu ili wapate ahuweni huko waliko. Tuhamasishane kuhakikisha tunaleta mageuzi ya kweli na tujipange kimkakati hasa. mwaka 2015 uwe ni mwaka wetu kweli na uwe ndio kigezo cha mahesabu yetu ya muda mrefu ya MAMLAKA KAMILI. Mazingira sio mabaya kihivyo tunatakiwa tuongeze jitihada kidogo tutafanikiwa inshaallah.

Tukumbuke madhila yanayowapata ndugu zetu waliomo jela na magerezani, viongozi wetu na masheikh wetu namna wanavyonyanyasika kwa kusema ukweli na kuunga mkono ukweli wa kutaka mamlaka na usawa katika muungano wetu. Hawa tusiwasaliti enyi wana wa zanzibar yetu njema.Mijini na mashamba kote Unguja na Pemba tushikamane na tusibabaishwe na wabaya wetu wanaotumia husda ya kuwagawa watu kunenepesha matumbo yao. TUWAKATAE kiungwana lakini wajuwe kama tumechukia mambo yao.

Tushiriki harakati za maendeleo yetu kuisaidia serikali yetu changa kimaendeleo na tushiriki kutafuta riziki za halali na kipato,tukumbuke wajibu huo na tusikose kuweka hakiba kwa ajili ya harakati zetu. Mwaka huu uwe wa hamasa ya hali ya juu kupeleka salamu zetu kwa watawala wasiotaka mabadiliko. Tushikamane TUTASHINDA.

Msisahau kuwa tuna deni kwa kizazi kijacho kuwaletea mazingira rafiki ya kuchuma ,kuamua, kuishi na kijidai katika nchi yao hili ni deni kubwa mno kwetu sisi vijana na wazee wa leo. Tuitumie fursa iliyopo mbele kupitia mchakato wa katiba na uchaguzi kuamua. Wakati ni huu kwa sasa ,tujipange TUKAE MGUU SAWA. Tutashinda.

Watu wajipange , tuhamasishane kujiandikisha ili kupata fursa ya kufanya maamuzi muhimu yajayo. wale wasio na hati stahiki vikiwemo vyeti vya kuzaliwa watafute sasa, wale wenye uwezo wa kifedha wawasaidie ambao hawana ili wapate fursa hio, wale wenye uwezo wa kunasua vitimbi vya masheha kuzuwiya watu kupata haki zao wasaidie hilo na tufanye kila aina ya maandalizi FURSA INAKUJA TUITUMIE Maandalizi ni sasa.

Tukae mguu sawa.

Share: