Habari

TUME YA KATIBA IACHE KUJIFUNGIA NDANI

KATIKA vitu ambavyo vimekuwa ni changamoto kubwa kwa nchi za Afrika ni uwazi. Mifumo ya kuendesha Taasisi za umma na hata uendeshaji mzima wa shughuli za Serikali vimejikita kwenye usiri. Nia ya kufanya hivi ni kukwepa uwajibikaji.

Nchini Tanzania kwa sasa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaendelea na mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi. Kwa ujumla kazi inakwenda vizuri kwa sababu kuna mwitikio wa hali ya juu sana wa utoaji wa maoni.

Ilianza na raia mmoja mmoja katika mikutano iliyoitishwa na Tume kisha ikaingia hatua ya Makundi, Taasisi na watu mbalimbali wenye hadhi ya Kitaasisi.

Wakati Tume ikipita katika Mikoa mbalimbali, vyombo vya habari vilipewa fursa ya kusikiliza wananchi walikuwa wanasema nini. Habari zilinukuliwa katika mikutano hiyo na kutangazwa ama kuandikwa bila kuchujwa kadri chombo cha habari kilivyoona inafaa.

Kwa bahati mbaya, tunasikitika uwazi uliokuwako ngazi ya kupokea maoni ya mwananchi mmoja mmoja, umeondolewa katika ngazi ya utoaji maoni kwa Makundi na Taasisi.

Maamuzi haya yamefanywa na Tume, inawezekana Tume ina sababu zake, lakini hisia za wengi ni kwamba usiri haufai kabisa katika kupokea maoni ya aina yoyote juu ya kuandikwa kwa Katiba mpya.

Zimeandikwa habari na tahariri juu ya suala hili, lakini tunaona inafaa kurejea tena suala hili kwa nia moja tu, kuikumbusha Tume kuwa iwajibike kufanya kazi zake kwa uwazi wa hali ya juu. Daima uwazi hukaribisha uwajibikaji.

Kimsingi iwe ni mwananchi mmoja mmoja anatoa maoni, Makundi au Taasisi ni maoni tu, kwa maana hiyo haiingii akilini kwamba ni kwa nini awali uwazi utamalaki na vyombo vya habari ambavyo hufanya kazi kwa ajili ya umma viruhusiwe kuripoti, lakini sasa ionekane haifai? Hili ni fumbo kubwa na zito.

Tumesema hapo juu, tatizo kubwa la Taasisi nyingi za umma katika nchi za Afrika ni kukwepa uwazi kwa sababu hulka ya uwazi ni kujenga uwajibikaji.

Ni jambo la bahati mbaya kwamba sasa wananchi wanakosa fursa ya kujua nani kasema nini katika kutoa maoni ya Katiba kwa sababu tu kuna kitu kama woga kimevamia Tume.

Tunaanza kujenga hisia kwamba Tume imeanza kujenga urasimu ambao kwanza hauna sababu wa kuamini kwamba wana hati miliki na maoni ya wananchi yanayotolewa juu ya kuandikwa kwa katiba yao.

Ni vema Tume ikaelewa kuwa haya ni maoni ya Wananchi, iwe Vikundi au Taasisi hakuna sababu yoyote ya maana ya kuyafungia ndani ili yasijulikane kwa umma kwa uwazi.

Tunapenda kuitaka Tume kufikiria upya, itambue kwamba kazi wanayofanya kwa sasa ni ya umma, si ya kwao wenyewe, si kazi ya Makamishna na watendaji wengine wa Tume.

Ni kazi ya umma wametumwa kukusanya maoni ya Watanzania kwa upana na uwazi unaostahili, ili pamoja na mambo mengine kujiepusha na lawama mbele ya safari kwa rasimu ya Katiba itakayopatikana.

Tunawashauri na kuwanasihi wahusika wa Tume, iache vyombo vya habari kuendelea kuripoti mikutano ya kutoa maoni katika hatua ya sasa kwa maslahi ya wananchi wote.

Katika mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba wadau wa vyombo vya habari wamezungumza kwa kina na kuwasilisha maoni yao juu ya matarajio yao kwenye Katiba mpya ijayo, bila kumung’unya maneno.

Wamesema Katiba ya sasa na Sheria za nchi zimefisidi uhuru wa habari na haki ya kupata habari, Tume pamoja na kutambua ukweli huo na kuelewa kwamba habari ni haki ya wananchi.

Tume yenyewe ghafla, nayo imeibuka na maamuzi ya kuzidi kukwaza haki hiyo ya wananchi ya kupata habari ambazo hata hivyo, hazina sababu ya kuzuiwa.

Kila tukiwatazama Makamishna wa Tume tunawaona kuwa ni watu waadilifu, waelewa na wenye weledi wa kiwango cha juu sana kuhusu haki za raia. Ni watu waliyobobea katika masuala ya Diplomasia, Demokrasia na wataalamu wa sheria.

Pia kila tunapojiuliza sababu za maana na za msingi za kufanya ukusanyaji wa maoni katika ngazi ya sasa kuwa siri ni kwa faida ya nani? Tunapata wakati mgumu kupata jibu.

Kwa kutafakari mambo haya, tunafikiri kwamba Tume itambue kadri itakavyofungua milango na madirisha katika kuendesha mambo yake, ndivyo itajijengea uhalali wa kukubalika.

Lakini zaidi, kuaminiwa na wananchi wanaosubiri Katiba yao ambayo imetokana na maoni yao wenyewe na si ya kutengenezewa na watawala kama ambavyo imekuwa huko nyuma – Tume ibadilike sasa..

Share: