Habari

Tume ya katiba kuapishwa leo

RAIS Jakaya Kikwete leo atawaapisha Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Ikulu Dar es Salaam ikiwa ni wiki moja tangu awateue.

Taarifa iliyotolewa jana na mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi, Premi Kibanga ilieleza kuwa wajumbe hao wataapishwa leo na kwamba baada ya kuapishwa, tume itaanza kazi zake rasmi Mei Mosi kama ilivyopangwa na kutangazwa awali.

Awali taarifa iliyotolewa Aprili 9 mwaka huu na Katibu Mkuu Kiongozi , Balozi Ombeni Sefue ilieleza kuwa badala ya Rais Kikwete kuwaapisha Ijumaa (leo), sasa atawaapisha Jumatatu Aprili 30 mwaka huu.

Taarifa hiyo ya Balozi Sefue ilieleza kuwa katika kufikia uamuzi wake, Rais Kikwete amezingatia mambo yafuatayo, kutokana na umuhimu wa shughuli hiyo yanahitajika maandalizi ya kutosha ili uzinduzi wa tume upate hadhi inayostahili na kusiwe na muda mrefu kati ya uzinduzi na kuanza kazi.

“Kisheria, Tume itaanza kazi yake Mei Mosi, 2012,”ilieleza taarifa ya Balozi Sefue.

Balozi Sefue alieleza sababu nyingine ni majukumu ambayo tume inakabidhiwa ni makubwa, yanayogusa mustakabali wa Taifa na hivyo kuhitaji umakini mkubwa na muda wote wa Wajumbe na wa Sekretarieti.

“Rais anafahamu fika kuwa aliowateua kwa sasa wanazo shughuli zao na wanahitaji muda wa kujiandaa ili wakiapishwa wawe tayari kuanza kazi mara moja na kuifanya kazi hiyo kwa muda wao wote ili lengo la kuwa na Katiba Mpya ifikapo Aprili 26, 2014, lifikiwe na Katiba hiyo itumike kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,”ilieleza taarifa hiyo na kuongeza;

“Hivyo, Rais anatumaini kuwa walioteuliwa watatumia wiki tatu zijazo kujiandaa kwa kazi kubwa inayowasubiri.”

Alisema sababu nyingine ni Rais amefahamishwa pia kuwa wapo miongoni mwa aliowateua ambao wamesafiri na asingependa kukatisha safari zao hivyo muda alioutoa sasa utawawezesha kurejea na kuhitimisha shughuli zao nyingine tayari kwa kuapishwa Aprili 30 mwaka huu na kuanza kazi yao ya Tume siku inayofuata ya Mei Mosi, 2012 kama ilivyopangwa.

Tume hiyo inaongozwa na Mwenyekiti, Jaji Joseph Sinde Warioba akisaidiwa na Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu, Jaji Augustino Ramadhan ina wajumbe 30, ikiwa ni wajumbe 15 kutoka kila moja ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wajumbe wa Tume hiyo kutoka Tanzania Bara ni Profesa Mwesiga Baregu, Riziki Shahari Mngwali, Dk Sengodo Mvungi, Richard Shadrack Lyimo, John Nkolo, Alhaji Saidi El Maamry na Jesca Sydney Mkuchu. Wajumbe wengine wa Tume hiyo kutoka Bara ni Profesa Palamagamba Kabudi, Humphrey Polepole, Yahya Msulwa, Esther Mkwizu, Maria Malingumu Kashonda, Mheshimiwa Al-Shaymaa Kwegyir, Mwantumu Jasmine Malale na Joseph Butiku.

Wajumbe wa Tume hiyo kutoka Tanzania Visiwani ni Dk Salim Ahmed Salim, Fatma Saidi Ali, Omar Sheha Mussa, Raya Suleiman Hamad, Awadh Ali Saidi, Ussi Khamis Haji na Salma Maoulidi. Wengine kutoka Visiwani ni Nassor Khamis Mohammed, Simai Mohammed Said, Muhammed Yussuf Mshamba, Kibibi Mwinyi Hassan, Suleiman Omar Ali, Salama Kombo Ahmed, Abubakar Mohammed Ali na Ally Abdullah Ally Saleh. Shughuli za Tume hiyo zitaratibiwa na Sekretarieti ambayo Katibu wake atakuwa Assaa Ahmad Rashid na Naibu Katibu atakuwa Casmir Sumba Kyuki.

mwananchi

Share: