Habari

TUME YA KATIBA MPYA KUMALIZA KAZI OKTOBA 2013

RAIS JAKAYA Kikwete, ambaye jana alitangaza kuunda Tume ya kuratibu mchakato wa Katiba mpya Tanzania, amesema wajumbe wa Tume hiyo wataapishwa wakati wowote ili kuwawezesha kuanza safari ya miezi 18 ya kukusanya maoni ya wananchi na kukamilisha kuandikwa kwa Katiba hiyo, inayotarajiwa kutumika ifikapo mwaka 2014.

Rais alisema Tume hiyo baada ya kukamilisha kazi yake ya kukusanya maoni ya wananchi Tanzania na kutengeneza rasimu ya Katiba, zitakuwa zimebaki hatua mbili muhimu ambazo ni kuundwa kwa Bunge maalumu la Katiba na wananchi kupata fursa ya kupiga kura ya maoni.

“Baada ya hatua hiyo kukamilika, rasimu itawasilishwa katika Bunge hilo ambalo litaundwa kwa ajili ya kujadili na kuchambua mambo yanayofaa kuwemo katika rasimu hiyo. Bunge hili litakuwa kwa ajili hiyo tu na likishakamilisha kazi yake muda wake utakuwa umeisha,” alisema Kikwete.

Alisema baada ya mambo ya msingi kupitishwa na Bunge hilo, mchakato huo utarejeshwa kwa wananchi ambao watapiga kura ya maoni kama wataona yaliyopitishwa yanafaa au laa.

Rais ametangaza kuunda Tume hiyo kufuatia marekebisho katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mkutano wa Sita wa Bunge la 10, marekebisho ambayo yalizua manung’uniko kutoka kwa wabunge wa CCM.

Katika hotuba yake ya Desemba 31, 2010 Rais Kikwete aliahidi kuanzisha mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya ambayo alisema italivusha Taifa katika miaka mingine 50 kwa kuimarisha mshikamano wa Watanzania. 

WATU WALIOTEULIWA WANENA

Baadhi ya watu walioteuliwa kuwemo katika Tume hiyo, wamezungumza kwa nyakati tofauti, wamesema ni mapema mno kuzungumzia uteuzi wao na kusema wanahitaji muda ili watafakari ukubwa wa jukumu hilo.

Dk Mvungi alisema kazi hiyo ni kubwa kwa kuwa wanaotumikiwa ni wananchi, huku akiomba kupewa muda ili aweze kutafakari cha kuzungumza.

“Muda mfupi uliopita ndiyo nilipata taarifa ya uteuzi huo ila nahitaji kujishauri kwanza pia kusikiliza ushauri wa familia yangu, naomba muda niweze kuwa na cha kuzungumza zaidi,” alisema Dk Mvungi.

Kwa upande wake Butiku alisema mpaka alipokuwa akipigiwa simu kuulizwa alivyopokea uteuzi wake alikuwa hajapata taarifa za uteuzi huo.

Alisema atazungumza mara baada ya kuthibitisha rasmi kuwa ameteuliwa, alisema na kuongeza “Hivi sasa mimi sijapata taarifa yoyote, ngoja kwanza nisubiri taarifa rasmi ili niweze kuzungumza vizuri,” alisema Butiku..

Share: