Habari

Tumekubali kuandikiwa katiba kibabe?

Nukuu kutoka gazeti la Tanzania Daima

Posted by Edson Kamukara

WATANZANIA haijulikani kama ni waoga au wajinga kwa sababu wamekuwa wenye kukubali kila kitu halafu mwishowe wanabaki kunung’unika wakati uwezo wa kuchukua hatua stahiki wanao.

Ukisoma sura ya pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 toleo la 2005 katika ibara ya 8-(1) (a) hadi (d), mamlaka ya wananchi dhidi ya serikali yao yameainishwa lakini inashangaza kuona serikali inafanya itakavyo.

Ibara ya 8.-(1) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo- (a) wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii.

(b) lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi; (c) Serikali itawajibika kwa wananchi na (d) wananchi watashiriki katika shughuli za serikali yao kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.

Hii ndiyo nguvu ambayo wananchi wanayo kikatiba kuisimamia na kuiwajibisha serikali yao. Sasa inakuwaje serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inatumia ubabe kuandika katiba pasipo kuzingatia maslahi ya wananchi?

Kwanini wananchi hawasemi hapana hata kwa kujikusanya na kuandamana hidi Dodoma, wakauzunguka ukumbi wa Bunge na kumweleza Samuel Sitta na wajumbe wake kwamba wanataka ijadiliwe rasimu yenye maoni yao waliyotoa kwa tume ya Warioba?

Wananchi hawa walitoa maoni yao kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kisha tume hiyo ikaanda rasimu ya kwanza yenye mapendekezo yao na wakarudishiwa wayatazame na kuyaboresha kupitia mabaraza.

Katika rasimu hiyo ya kwanza, muundo wa muungano uliyopendekezwa ni ule wa shirikisho lenye serikali tatu, yaani Tanganyika, Zanzibar na ile ya shirikisho.

Na katika maboresho yao kwenye mabaraza ya katiba, wananchi waliendelea kutaka mapendekezo yao yabakie hivyo, ndiyo maana katika rasimu ya pili ya katiba iliyowasilishwa kwa Bunge Maalum la Katiba, muundo wa muungano umebakia kuwa serikali tatu.

Kwa bahati mbaya sana kama ambayo walikuwa hawataki katiba mpya, CCM wameibuka na kukataa maoni ya wananchi kwenye rasimu na sasa wanataka yakubalike mapendekezo ya chama chao ya serikali mbili.

Mvutano huu umefika mahala pa kulimega Bunge Maalum la Katiba katika makundi mawili. Moja linaundwa na vyama vikubwa vya upinzani ambalo linataka maoni ya wananchi kwenye rasimu yaheshimiwe.

Kundi la pili linaundwa na serikali ya CCM ambalo linataka rasimu ifumuliwe na kuondoa mapendekezo ya serikali tatu na kurudisha mbili za sasa ambazo zimekuwa donda ndugu kwa muungano wetu.

Kukwama kwa Bunge Maalum la Katiba, kumeibua migongano mingi kiasi cha wengi kumwomba Rais Jakaya Kikwete alivunje Bunge hilo hadi hapo maridhiano yatakapokuwa yamepatikana ndipo mchakato huo uendelee kwa faida ya kupata katiba bora.

Lakini CCM hawataki kuheshimu katiba ya sasa inayotoa mamlaka kwa wananchi kuisimamia na kuiwajibisha serikali yao, badala yake serikali imejigeuza kuwawajibisha wananchi kwa kuwalazimisha wafuate inavyotaka.

Huu ni uoga wa wananchi au ni ujinga wa kutotambua mamlaka yao? Kwanini tumekubali kuandikiwa katiba mpya kibabe? Hii katiba ni ya wananchi au viongozi wa serikali na CCM?.

Kama sio uoga ama ujinga wa wananchi, kwanini wamekuwa kimya katika hili kwa kuendelea kuwatazama CCM wakifuja mabilioni ya fedha zao huko Dodoma wakati wakifahamu fika kwamba theluthi mbili ya kura ya kuamua katiba katika Bunge hilo haitimii?

Hivi CCM ni nani yenye kiburi cha namna hiyo, wako wangapi hadi waogopwe hivyo. Wananchi wanataka mamlaka gani zaidi ili waweze kuisulubisha CCM isiwaingize kwenye machafuko ya Katiba?

Tumeandika mara nyingi kwamba CCM hawakuwahi kuwa na wazo wala nia ya kuandika katiba mpya, na ukweli utabakia hivyo kwamba hawawezi kuipata nia hiyo leo, isipokuwa wanahadaa wananchi.

Wakati ni sasa wa wananchi kuisimamia na kuiwajibisha serikali yao iliyotokana na matakwa yao. Kwa vile serikali ya CCM imeziba masikio na inatumia nguvu kuandika katiba isiyotokana na misingi waliyojiwekea wananchi basi hawana budi kuiweka kando.

Tume ya Jaji Warioba ilitumia zaidi ya sh. bilioni 74 kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa rasimu kisha ikakabidhi jukumu hilo kwa Bunge la Katiba.

Bunge la Katiba lilimaliza siku zake 67 likiwa limetumia sh. bilioni 27 bila kutimiza wajibu wake, badala yake liligeuka kujitwisha kazi ya kutetea maslahi ya CCM ya kulinda muundo wa serikali mbili.

Sasa Bunge hilo lililoshindwa kazi kwa siku 67 limeongezewa siku 84 ambapo litatumia zaidi ya sh. bilioni 20 halafu mwisho wa siku katiba mpya haitapatikana kutokana na idadi ya wajumbe kutokidhi matakwa ya sheria inayotaka theluthi mbili ya kura kwa Bara na Visiwani.

Hivi huruma ya CCM iko wapi kwa wananchi. Kwanini hizi fedha wanazolipana maposho zisielekezwe kwenye hospitali ambapo wajawazito wanakosa vifaa vya kujifungulia, wanakosa vitanda na kulazwa wawili kitanda kimoja.

Shule za serikali za msingi za serikali takribani zote nchi nzima hazina madawati ya kutosha, vyoo, maktaba, vitabu na mahitaji mengine lakini serikali ya CCM badala ya kujibana fedha zikaelekezwa huko, inatumia kwa wajumbe wa Bunge la Katiba kulipana posho kwa kazi ambayo haitakamilika.

Itoshe kwa wananchi kuwa na ujasiri wa kuwakabili watawala na kuwaeleza kwamba imetosha, ubabe huu basi tunataka utawala wa kidemokrasia ambao unatokana na matakwa yetu na sio yale ya viongozi.

Kushidwa kufanya hivyo na kuendelea kuichekea CCM, wananchi hawa watakuwa wamekubali kujiuza kwa gharama nafuu nchi yao ambayo mwisho wake wataujutia haki hii ya msingi baada ya kuandikiwa katiba ya viongozi. Tafakari!

Share: