Habari

Tunapaswa kuunga mkono maneno ya Mheshimiwa Hamza

Hamza Hassan Juma ni Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura (CCM) akichangia mada katika moja ya semina za wajumbe wa baraza la wawakilishi zilizofanyika katika ukumbi wa baraza hilo huko Mbweni Mjini Zanzibar

Katika wakati ambao ni muhimu sana kuunganisha nguvu zetu ikiwa kama wazanzibari basi ndio wakati huu kuliko wakati mwengine wowote na kwa hivyo nachukua fursa hii adhimu msimamo wa mtandao huu wa zanzibaryetu kwamba kulipongeza baraza la wawakilishi na wajumbe wake wote waliochangia hoja ya Mheshimiwa Ismail Jussa Ladhu Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF).

Lakini pia kukubaliana na kuiunga mkono kauli ya Mheshimiwa Hamza Hassan Juma Mwakilishi wa Jimbo la kwamtipura (CCM) aliyeitoa katika kikao cha baraza la wawakilishi akisema kama ni agizo maalumu kwa wazanzibari lisemalo hivi, na ninanukuu ” Mheshimiwa Hoja hii aliyeitoa Mheshimiwa Jussa isije ikachukuliwa kisiasa, isije ikachukuliwa kuwa imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) lakini hoja hii ichukuliwe kuwa imetolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Mheshimiwa Ismail Jussa, Mwakilishi halali wa wananchi, tunaomba hoja hii isichukuliwe kisiasa maana hoja hii ikichukuliwa kisiasa itatugawa na tutaweza kupoteza rasilimali na uwezo wa baraza la wawakilishi kuisimamia serikali” Mwisho wa kunukuu.

 

Hayo ndio maneno yake Mwakilishi wa Mwamtipura (CCM) Mheshimiwa Hamza Hassan Juma. Mimi kama mmiliki wa mtandao huu wa zanzibaryetu na ni mzanzibari halisi ninayejivutia uzanzibari wangu na heshima ya nchi yangu adhimu Zanzibar, basi nasema kwamba kwa hakika ni maneno ya maana sana na ni maneno ya hekima kubwa na ni maneno ya kutia moyo sana kwetu sote wazanzibari kwani kauli hiyo sio tu nzuri bali inajenga zaidi na inaonesha ukomavu kwa wazanzibari kwamba wamefika pahala hawataki tena kuchezewa wala kukoseshwa haki zao kwani ni maneno na kauli ya kuonesha umoja na mshikamano wetu katika kuitetea nchi yetu.

Hivyo nachukua fursa hii kuwaomba wazanzibari wote kuiunga mkono kauli hii kwa nia safi na kwa dhati kabisa lakini pia kuisambaza kwa kila mmoja wetu ili tufahamu kwamba wakati ndio huu na tukipoteza fursa hii ya umoja na mshikamano wetu na tukikubali kuwapa maadui nafasi wakatupoteza kama walivyofanya huko nyuma basi naamini hatutaweza tena tuunganisha nguvu zetu na umoja wetu tena hivyo basi fursa kama hiyo tutakuja kuitaka tuikose, shime basi tuwaunge mkono wawakilishi wetu katika kuitetea nchi yetu, sasa ni wakati wa kuungana zaidi na kuongeza nguvu bila ya kujali huyu anatoka chama gani, na hilo sio geni kwetu wazanzibari ikiwa tuliweza katika suala la kuambiwa Zanzibar sio nchi tuliungana na kusema Zanzibar ni nchi itakuwaje tushindwe katika hili?.

 

Na ikiwa tuliweza kuungana katika suala la kupigania mafuta yetu na wazanzibari wote walisimama kidete kupitia wawakilishi wao na kusema ni haki ya Zanzibar hata kama sio kwa vitendo lakini kwa kauli lilisimamiwa kwa dhati na na kwa moyo mmoja na kila mmoja kwa nafasi yake alichukua juhudi kuhakikisha suala hilo naye ameliwakilisha basi iweje tushindwe katika hili? Imani yangu kwamba huu ndio wakati muhimu sana kwetu kusimamia na kuitetea nchi yetu bila ya kujali chochote kwani kutetea nchi yako ni moja katika wajibu wako.

zanzibaryetu

Tagseez
Share: