Habari

Tuwaombe radhi “Waarabu/Machotara” wote.

Bila kuona haya,soni au aibu leo nimerudi ukumbini makusudi kuweka bayana kwani haijawahi kuwa siri lakini ile mila,utamaduni na asili yetu tulio zoweshana kwa muda mrefu ni vema tukaujadili kwa kina badala ya kuufutika chini ya zulia kwa matumizi ya baadae,huu si mwingine bali ni ule uhayawani unao tumika wakati wa kampeni zetu za uchaguzi mpaka wakati wa kujitangazia ushindi wa kishindo CCM ndio hupona au kupata afueni tu kwani mara baada ya miaka mitano kupita kama moshi maradhi haya huturudia kwa kasi ya moto wa volcano na wazimu huturudia vichwa tele na kuanza kutukana makabila ya watu,rangi za watu,asili za watu na vyama vya watupamoja na dini yetu wenyewe ili tukidhi shida yetu ya kutawala bila kupingwa milele Mungu akipenda asipende hiyo ndio amri yetu sio ombi.

Hili hatuna budi kulichambua “once and for all” kwa manufaa ya watu wetu,utu wetu na ustaarabu wetu ulio bakia kwa sababu kila kukicha unapungua kama tunavyo pukutika sisi wenyewe,nina hakika wengine wasingelipenda sisi kuya”revisit” haya yaani kuyadurusu au kuyapitia wangelifurahi sana kwa kuwa ule wakati wa kujibebesha sahau ya makusudi “amnesia” umeshafika basi ni lazima sisi waungwana tuyasahau haya na tuendelee na utu wetu ulio jaa mapenzi,uhusiano mwema,udugu na urafiki wa jadi uliodumu kiasi ya karne mbili na zaidi nitakuwa mnafiki ikiwa nitakubali kusubiri uchaguzi ujao kama nitakuwa hai ili nijiunge na wenzangu chamani katika kuanza kurusha matusi upya kwa visingizio vile vile vya kurudisha waarabu na kuwafukuza machotara upya ili sultani wetu mweusi au maji ya kunde{salmin} aka kikalie au kukirithi chetu maalum kwa ngozi iliyo kusudiwa huu ni ubaguzi ulio jaa chuki na maradhi yasio tibika kwa sababu nimechoka na kupata nafuu.

Nimehuzunishwa sana na baadhi ya wenzangu ambao siku zote nina waheshimu na kuheshimiana nikijua kuwa ni wacha Mungu na watu wenye shahada za elimu tofauti za kidunia lakini wengi kati yao walishika milingoti ya kutukana waungwana wa kiarabu, kichotara na kufika kutamka kuwa hawataki tena kina mama na dada zetu wetu kufagilishwa barabara zetu safi na waarabu kwa kutumia maziwa yao kama ndio ufagio, hizi ni kauli zilizotolewa na wasomi wetu wa vyuo vikuu waliobobea katika fani tofauti za elimu na kusoma katika vyuo vikuu karibu duniani kote,mimi hujiuliza hawa waungwana ingelikuwa hawakusoma kama mimi angeli salimika mtu hapa ikiwa wamesoma hali ndio kama hii?maneno kama haya ningelisema mimi, Borafya au hata huyu mheshimiwa Mohamed Aboud waziri wa nchi{kama ipo} katika afisi ya makamo wa pili wa rais nahakika ingelikuwa kauli thabiti kwa kuwa sote elimu zetu zina fanana lakini wakiandika,wakinon’gona na kuyamka wenyewe mabalozi, madaktari na maprofesa hapo ndipo penye kitendawili.

Mimi sipendi kuinukuu misaada kuwa ndio kigezo cha sisi kuacha kuwatukana watu,mataifa au waarabu kwa kuwa hutugaiya au kutukopesha fedha pamoja na zawadi basi iwe hawatukani au kwa kuwa hautupati au hatufaidiki kwa lolote na kaumu niliyoitaja basi ruhsa kuwabagua,kuwatukana na kuwafukuza nchini hii sio dini sio utu wala sio ustaarabu tunojipachika bila aibu siku zote kuwa sisi wazanzibari ni watu wenye hulka njema na karima kama mmesahau nitakumbusha leo sio zaidi ya wiki mbili tangu uchaguzi na uchafuzi kwisha yale mliyo yashuhudia yote ambayo karibu yote mabaya na ya kutia kichefu chefu wale ndio sisi wazanzibari ninao wajua mimi siku zote sio wale wanao tangazwa maredioni na kusifiwa kama hawazijui nafsi zao,nia zao na unyama wao dhidi ya raia wenzao.

Zanzibar ni toto yatima kwa miaka mingi na ataendelea kuwa mtoto wa aina hiyo kwa miaka mingi ijayo kwa sababu wazee wake wameuliwa miaka mingi na wajomba zake sio watu wema,Marehemu Mzee Karume alimpeleka kulelewa mtoto huyu Tanganyika mwaka 1964 kwa kisingizio cha muungano lakini dhumuni halisi na halali lililo mfanya kumpeleka mtoto huyu kushinda Daresalaam au Tanganyika ilikuwani kutafuka usalama wake binafsi pamoja na serekali yake kwa sababu hakuwa na ubavu wa kujilinda na kuilinda serekali yake changa baada ya mapinduzi na wengine wanasema hata hayo mapinduzi yalitokea huko kwa hiyo inaingia akilini kukimbilia huko huko kutafuta manusura.

Sasa haya mnayo yashuhudia sasa binafsi nilikuwa na wasi wasi nayo kuwa yatatokea na chini chini nimeyaongea haya na sahib yangu msomi mmoja miaka ya nyuma,hivi visiwa vina kabidhiwa tena kwa mara ya pili na ya mwisho kwa nduguzetu wale wale wa Tanganyika kwa kuvi hifadhi la kujiuliza safari hii vina kimbizwa kwa kuogopwa nani? jawabu nahakika waungwana mnalo sina haja ya kupoteza wino lakini inaingia akilini kweli kuwa ni bora kutawaliwa na Mnyamwezi anae kuja na minyororo na “Makufuli” yake tayari kwa kuvi burura hivi visiwa na kuvipeleka ziwa voctoria karibu na kwao wakati huku kuna bahari ya Hindi kubwa ipo na inatupa upepo wa pwani kwa buraha kwa karne na karne lakini tume pungukiwa na uwezo wa kufikiri kwa CHUKI na UBAGUZI bila kuvionea huruma hivi visiwa au huyu mtoto yatima.

Ni lazima tukae kitako chini na kutafakari mengi hasa hili la kuombana radhi kwanza kwa yote tuliyo tendeana na tunayo endelea kutendeana kwa nia safi kabisa,hata ikibidi turudi nyuma kwenye mapinduzi basi tukae kitako na kusoma DUWA/HITMA pamoja za wale wote walio dhulumiwa roho na mali zao siku hiyo bila kujali alikuwa muarabu,muhindi,muafrika,chotara,baniani,mwanamke,mwanamme,mtoto au mzungu kwa sababu hapa tulipofika ni Mola peke yake ana tunusuru na kudhulumiana tena roho na vitu hivyo kwa kuzitumia sababu zile zile zilizo tufanya tukauwana ovyo 1964 kwa kigezo cha Mapinduzi.

Na sasa tunataka kuuwana ovyo tena upya kwa kigezo cha kulinda Mapinduzi, kweli sisi tuna vichwa vikubwa kwa vidogo tuna vibeba mabegani wapi tunakwenda navyo mimi sikujui na kila mmoja wetu hataki kukitumia kichwa chake tuko radhi kuranda navyo ovyo tu,naelewa fika kuna wenzangu ukitaja au kuhoji mapinduzi na mauwaji yake basi wewe sio mwenzatu au muumini wa Mapinduzi hapana mimi mwenzenu lakini bora niwe muumini wa dini ya kiislamu kuliko Mapinduzi kwa sababu sitaki turudie makosa ya kuwauwa watu OVYO wasio husika na mapinduzi bure,ndio maana iko siku nilisema tutarithi yale yalio mema peke yake na yale maovu ni lazima tuyajue na tusiyarudie.

Kwa kuwa wana rangi tofauti na mimi au wanaongea lugha tofauti na yangu iwe basi inatosha kusulubiwa na hatimae wauliwe kwa kuwa hawa wapemba/waarabu hawa kuhusika wala kushiriki mapinduzi hawayajui,hatukujali wala hatutojali kama wana hatia au la,au hawa waarabuna machotara basi inatosha kuwa hukumu na kuwafukuza zanzibar kwa kuwa hapa petu sisi weusi watupu.

Afrika ya kusini baada ya utawala wa walio wengi walikaa kitako na kuitana mmoja mmoja na kuulizana na kusema yote waliweka wazi waliyo tendeana wakati wa utawala wa wachache nia na madhumuni ya vikao hivyo ilikuwa sio kunywa chai peke yake bali ni “KUSAMEHEANA” ‘Truth and Reconciliation Commission’ baada ya kuuweka ukweli wazi.

Sisi hatutaki kuukubali ukweli siku zote sasa hatu toweza kusamehena ikiwa tunadumisha kuficha uchi na hapo hapo tunatarajia kumsitiri huyu mtoto yatima zanzibar kwa nguvu za dola na majeshi ya bara siku zote na wakati huo huo tukailinda heshima yetu,utu wetu,DINI YETU, ustaarab,mila,silka na utamaduni wetu badala yake tuna jikuta katika utamaduni wa wenzetu ambao ndio tulio nao sasa,huu uhuni wa magari ya doria kutembea na kupiga watu ovyo wakati wa uchaguzi ni mila na desturi tulizo zowea kuziona katika televisheni peke yake matukio hayo yakitokea huko nyuma Afrika ya magharibi na nchi za wenzetu leo hii ndio MILA yetu na imesha zoeleka ni lazima tukubali waungwana.

Uchaguzi na Uchafuzi wa marudio umekwisha sisi sote wapenda amani,haki na usawa hatukushinda na wale walio hubiri fujo,vita,ubaguzi,chuki na uafrika peke yake wameshinda kwa nguvu za dola na uchache wa askari,ccm wala cuf wote hawa kushinda hapa kina chotendeka ni kununua wakati tu, kwa sababu wingi wa watu umeamua kukaa kimya na kupunga upepo kwa sasa sijui kama wana tafakari hatua gani wachukue au ndio wamesha vuta mashuka tayari kwa kusinzia na wengine kukoroma kwa miaka mitano mingine. Wosia wangu ni mfupi sana kwetu,mimi ni mpenzi wa wana harakati na mafilosofa wawili maarufu walioishi duniani hayati Mahatma Ghandi wa India na Martin Luther King wa Marekani viongozi hawa waliongoza watu wao kwa amani lakini hawakuvuta mashuka.

Ninacho taka kusema ni kuwa viongozi wa cuf na wapenda haki wote msitafune maneno kila siku kwa kuogopa kufunguliwa mashitaka na hatimae kufungwa, hivi visiwa vinaondoka kwa ukimya wenu hili baraza la wawakilishi lina subiri kutoa KIBALI tu cha kuimaliza zanzibar ni lazima mtamke wazi kuwa sasa ni wakati wa kuingia barabarani na kudai visiwa hivi kwa nguvu ya umma ambao mnao, na uko tayari,hatuwezi kupona haya maradhi ikiwa hatutafi kufanya upasuaji MKUBWA wa kuondoa hii TEZI inayo leta kansa katika kichwa chetu,dawa za kupaka na za kunywa hazikufaa wala hazitofaa kwa miaka mingine ishirini mnasubiri ushahidi gani zaidi ya mlio kwisha pewa bure,na kama kuna tatizo la uongozi basi huu ni wakati muafaka kuwapisha viongozi wapya vijana waje kumaliza kazi iliyofanywa kwa ustadi na umakini wa hali ya juu wa Maalim Seif Sharrif katika kuleta upinzani wa kweli Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, hata Lowassa ujio wake ni moja ya mafanikio ya Maalim ndio maana hata Tanganyika kwa mara ya kwanza kumepatikana upinzani wa uhakika, sio ule wa usanii wa siku zote uliozoeleka na ukitumika na kutengenezwa kufurahisha wa magharibi na wenye kutembea na vichwa pasi na kujua kazi yake.

Naomba radhi kwa matatizo ya uchapaji yakijitokeza kwani sijapata muda wa kuipitia mada upya kwa masahihisho.

Asanteni.
Mzee wenu.

Mzeekondo.

Share: