Habari

Uandikishwaji Vitambulisho vya Mzanzibar Una nia njema?

Hivi karibuni Dr Ali Mohammed Shein Rais wa Zanzibar akiongozwa na Waziri Haji Omar Kheir walikwenda kwenye uzinduzi na kufunguliwa ofisi ambayo hata jina lake bado sijalijuwa sikwambii madhumuni yake.

Jana nilisoma chapisho moja la Bi Ummy Aley, huyu mke wa Jaji Mkuu mstaafu ambaye sasa ndio mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Zanzibar. Aligusia kitu kimoja kuwa Zanzibar na Wazanzibar wamewatangulia Tanganyika na Watanganyika kwa kila kitu. Nirudi kwenye mada sasa.

Zanzibar ilikuwa ya kwanza kuanzisha BVR (biometric voters registered) ikitanguliwa na Kitambulisho cha Mzanzibar (ingawa jina lake haswaa sio hilo ila naona tabu kulisema). Tukitumaini kuwa ingekuwa hatua moja mbele nasi Wazanzibar kupata haki zetu.

Kama kawaida yetu Kitambulisho cha Mzanzibar kikatumika kinyume na madhumuni ya uletwaji wake. Pengine ni mbinu za mkoloni kuona hapo itakuwa imechezwa rafu. Mkoloni akijuwa fika kuwa ndani ya Katiba ya Zanzibar kuna mtu anayeitwa MZANZIBAR, akaanzisha hila na yeye akaleta chake. Kitambulisho cha Mtanzania kimekuja wakati Kitambulisho cha Mzanzibar kishatumika (iwe vizuri au Vibaya).

Tumuache mkoloni, turudi kwetu wenyewe. Idara hii ya vitambulisho alikabidhiwa mmoja Bwana mkubwa Mohamed Juma Ame, na akafungua ofisi pale Mazizini, akiwa mtu nyeti aliweza kuiunganisha system ile ya vitambulisho na system ya Kiisrail. Hivyo kufyonza datas za wananchi wa Zanzibar bila ya ridhaa zao.

Bwana Mohamed alirudi akajinyakulia mamlaka ya Idara nyengine ya e government, ambapo kaitia hasara nchi ya dollar million 20 kwenye mradi huo kupitia mkonga (fibre optic). Hadi leo hakuulizwa kitu zaidi ya kuhifadhiwa.

Akarudi Bwana Mohamed akaiunganisha idara hii na tume ya uchaguzi. Kama vile Kitambulisho cha Mzanzibar mi haki ya wapiga kura. Ikiwa huna mnasaba na kupiga kura hayo mashakili yake ukikhiari mwenyewe kusalimu amri na kumuachia Mohamed Ame Kitambulisho chake.

Baada ya miaka 10 leo unaletwa usanii mwengine ambao hata binafsi sijaelewa mantiki yake na chanzo chake hasa ni nini.

Ninacho Kitambulisho cha Mzanzibar pia wako Wazanzibar wengi wenye navyo kwa maana bado havija expire, leo nikipi kilichotupata hata tukaanza uandikishwaji upya wa vitambulisho hivi. Jee kuna usalama hapo.

Nasema usalama haupo. Nnazo sababu kadhaa. Moja, nna wasiwasi hii idara ya vitambulisho tushamsabilia Mkoloni kwa bei chee ya kutaka uluwa. Jina la hii idara sasa linaitwa Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar. Hapo peke yake tushapoteza muelekeo.

Pili, kuna kila dalili Kitambulisho cha Mzanzibar kumezwa na Kitambulisho cha Mtanzania.

Tatu, hili jengo la idara limekosa eneo la kujengwa Hadi dunga. Tunafahamu Zanzibar hadi huduma uifuate, na sio huduma kukufuata wewe. Mjini Magharibu kuna zaidi ya nusu ya wakaazi wa Unguja, wote hao watoke hadi Dunga kufuata vitambulisho.

Viongozi wetu kila akaaye kwenye kiti kile lazima aache athari yake kuiuwa Zanzibar. Na hii serikali iliyopo kimya kimya inaacha athari kama hizo. Miaka michache ijayo lengo litatimia. Nimeona mfumo wa uendeshaji serikali sasa hivi ni mmoja, hakuna madai ya haki za Zanzibar, wala hakuna kero kutatuliwa zaidi ya kuongezeka.

Share: