Habari

Uchafu wote wa siasa za Zanzibar, umehamishiwa Tanganyika

Elbattawi
Jumapili, Februari 11, 2018

TANGU mfumo wa kisiasa wa vyama vingi Tanzania (Tanganyika na Zanzibar), kuanza tena mwaka 1992 Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho kinachobuni hujuma zote za ukorofi, ukatili na uharamia dhidi ya upinzani na wananchi wanaokipinga.

Kwa siasa za kisayansi CCM kimepoteza dira na mwelekeo, siasa safi zimewashinda, kwani kilipaswa kuwa mwalimu wa kuendesha siasa za kistaarabu na za wazi, ili wapinzani wasome. CCM ni chama kikongwe kinachofanya aina ya siasa za msituni.

Kilipaswa kuwa chuo cha kufundishia vyama vipya vilivyoundwa baada ya mwaka 1992 na kuwa mwalimu wa vyama hivyo. Kinyume chake upinzani umechukuwa nafasi hiyo. CCM, kimebaki kuwa chama cha hujuma na dhuluma.

CCM kimegeuka kuwa chama cha watu wajinga, waliyopoteza mwelekeo wala wasiojuwa wanalolifanya katika mizani ya siasa na umma wa watanzania.

Ajabu na aibu inayoonekana kwa CCM kimegeuka kuwa chama cha msituni kinachofanya hujuma za kiharamia dhidi ya wananchi. CCM inaongoza kwa siasa za kishenzi, ubabe na ujinga. Tayari kimepoteza mwelekeo na hekima.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kiliundwa tarehe 5/2/1977 (41) ni Muungano wa Chama cha TANU ya Tanganyika na ASP ya Zanzibar. Tangu mfumo wa siasa wa vyama vingi iliporejeshwa tena mwaka 1992, CCM imekuwa ikikabiliwa na upinzani mkali na wazi.

Kwa upande wa Zanzibar, CCM imekuwa ikipoteza nguvu za utawala (madaraka), kila baada ya miaka mitano ya uchaguzi mkuu, kinachofanya kuendelea kutawala ni ubabe na nguvu za kijeshi kutoka kwa mkoloni mweusi, Tanganyika.

Mfano wa karibuni unaoweza ukatupa kigezo kwa wananchi wa Zanzibar, kuchoshwa na CCM kuwa kwenye madaraka ni Uchaguzi Mkuu wa siku ya Jumapili, Oktoba 25, 2015. Ilikuwa aibu na fedheha kubwa kwa CCM.

Hapa sina budi kusema kwamba dhuluma ya kupora madaraka kwa mbinu, ujanja na kwa kishingizio cha uchaguzi wa marejeo wa Machi 20, 2016 itawatesa sana viongozi wa CCM hasa Dk Shein, kwa kuwa yeye ni Muislamu, anayefahamu kosa la mwenye kudhulumu haki za watu, iwe fedha, mali pamoja na madaraka ya utawala ya kuchaguliwa na raia kwa makubaliano.

Naamini kwamba, CCM Zanzibar na Tanganyika kwa uchaguzi huru wa wazi na haki, (uchguzi wa kidemokrasia) usiyotumia nguvu za Jeshi na Vikosi, kuhujumu wananchi wapigakura, CCM hakiwezi kushinda milele kwa aina ya siasa zake na matamko ya viongozi wake.

Nikinukuu habari iliyoandikwa na Gazeti la Mwananchi la Jumapili, Februari 11, 2018 kuhusu CHADEMA, yalalamika dhidi ya msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni kuendesha uchaguzi huo kwa upendeleo na mawakala wake kutopewa hati zao za viapo. Inathibitisha makala yangu haya.

Kwa mujibu wa Gazeti la Mwananchi: “CHADEMA imemshutumu msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni ikidai anaashiria kuharibu uchaguzi wa Februari 17, 2018.

Chama hicho kimedai kutowapa viapo mawakala jana (Jumamosi) Februari 10, 2018 kunaashiria njama za kutaka wasishiriki shughuli za upigaji na kuhesabu kura.

Viongozi wa CHADEMA wamesema hayo leo (Jumapili) Februari 11, 2018 walipozungumza na waandishi wa habari kuhusu uchaguzi mdogo katika jimbo hilo na la Siha pamoja na kata tisa.

Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa CHADEMA, Benson Kigaila amesema sheria inataka mawakala wa upigaji wa kura kula kiapo cha kutunza siri, siku saba kabla ya kupiga kura na wanapaswa kupewa kiapo hicho.

“Anayeapisha ndiye anayesaini, hawezi kuapa mbele ya mtu mmoja na kusaini mtu mwingine, kwa kila mwapishaji katika kila kata anakuwa na sababu zake, msimamizi wa uchaguzi anatumika,” alidai Kigaila.

Kigaila amesema, “Kinachoendelea Kinondoni ni tofauti na Siha, kule Siha wameapa jana na kila wakala ameondoka na kiapo chake, sasa sijui sheria inayotumika Siha ni tofauti na inayotumika Kinondoni,” alihoji.

Meneja kampeni wa Chadema Kinondoni, Saed Kubenea amesema kila linalopangwa kutaka kuuharibu uchaguzi huo hawatalikubali.

Baada ya habari hii ya Gazeti la Mwananchi, sasa narudi kwenye kichwa cha habari cha MAKALA yangu kwamba, ‘Uchafu wote wa siasa za Zanzibar, umehamishiwa tena Tanganyika’, ambako ndiyo asili yake, ndiko unakotokea.

Yanayotokea Tanganyika sasa hivi kwa Zanzibar si mambo mageni, tangu ulipoanza mfumo wa vyama vingi chini ya CCM mwaka 1992 kwa Zanzibar, yamezoeleka wala hakuna la ajabu tena. Siasa za aina hii zinazofanyika sasa Tanganyika, ndiyo sababu inayoelezwa ya kutokomea kwa CCM Zanzibar.

Kuna msemo kwamba: “Kila mchimba kisima huingia mwenyewe” Nina hakika kwamba ubaya na hujuma dhidi ya Wazanzibari, ni mipango inayosukwa na kupangwa na CCM Tanganyika, halafu kupelekwa Zanzibar, kutekelezwa. Watanganyika wataingia wenyewe kisimani.

Kupotea kwa watu, kupiga na kujeruhi wananchi, kuwabambikizia kesi wapinzani hususan CUF na kuwaweka magerezani bila makosa ni jumla ya mambo na mikakati inayotoka Tanganyika. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu, kwamba sasa yanawerejea wenyewe.

Hili linajidhihirisha sasa hivi kufuatia matukio kiharamia yanayoendelea kutokea Tanganyika ni kaburi waliyoichimba CCM Tanganyika dhidi ya Wazanzibari, sasa wameanza kuingia na wao wenyewe. Kwa asilimia mia moja Tanganyika, haiko salama labda CCM kibadilishe mfumo wa siasa zake.

Aidha, nisema kuwa, Wazanzibari wamekuwa wavumilivu kwa mateso yote yaliyowakumba kabla na baada ya mfumo wa vyama vingi hadi leo. CCM Zanzibar, haina ubaya mpya ambao haijawatendea Wazanzibari.

(1) CCM, imemuweka jela kwa miezi 31 Maalim Seif Sharif Hamad (Utawala wa Ali Haasan Mwinyi na Idris Abdul Wakil), Maalim Seif yupo na Wazanzibari wanampenda kupita kiasi haijawahi kutokea kwa kiongozi yoyote wa Zanzibar.

CCM Zanzibar, iliwaweka jela miaka mitatu, viongozi 18 wa CUF (utawala wa Salmin Amour Komando).

CCM Zanzibar, imekuwa ikifanya uovu wa mara kwa mara hadi leo dhidi ya Wazanzibari. Utawala wa Dk Shein na Balaozi Seif Ali Iddi, imewachukuwa Masheikh wa Jumuiya ya Uamsho, imewapeleka jela za Tanganyika, sasa zaidi ya miaka minne.

Wanachama wa CUF, wanavamiwa majumbani wanauawa huku, serikali ya Dk Shein, ikihushwa kuwa na mkono wake.

Vikosi maalumu vinapofanya hujuma dhidi ya CUF, hakuna hatua zinazochukuliwa. Kama vile wanaofanyiwa hujuma hizo si raia na wanaofanya uhalifu huo wana hati miliki.

Kauli ya Balozi Seif Ali Iddi, kuhusu viongozi wa Uamsho kunyea ndooni, ni moja ya kauli mbaya inayowasononesha sana wananchi wa Zanzibar.

(2) CCM Zanzibar, tangu kurejea kwa mfumo wa siasa wa vyama vingi, imewafukuza kazi wafanyakazi wa serikali na kuwafukuza wanafunzi masomo na kuendesha shughuli za serikali na nchi kwa misingi ya ubaguzi kwa kuangalia asili ya mtu na itikadi za kisiasa.

Kwa mfano, Idara ya Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi na hata Jeshi la Wananchi (JWTZ), idadi kubwa ya waajiriwa ni wenye asili za Tanganyika na wanaoonekana kutokuwa na nasaba za makabila ya kiarabu.

(3) CCM Zanzibar, tarehe 26 na 27 Januari 2001, imewauwa kwa kuwapiga risasa wananchi wa Zanzibar, wasiyokuwa na silaha, wasiyokuwa na hatia. Kosa lao ni hoja ya kidemokrasia suala ambalo katika utawala bora unaozingatia haki za binadamu halipaswi kutumia nguvu hadi kuuwa wananchi.

Kuhusu kuwanunua viongozi wa upinzania kwa Zanzibar, siyo jambo jipya wala geni. Salim Msabah, Mbunge wa CUF Jimbo la Mkunazini, Unguja mwaka 1995, CCM walimnunua. Na mgogoro wa sasa wa CUF kupitia Lipumba na Msajili wa Vyama vya Siasa ni njama na hujuma za CCM Tanganyika. Hakuna asiyejuwa, hata viziwi hawahitaji kupigiwa tutu kuhusu hilo.

Hujuma dhidi ya upinzani hususan kwa vyama vya UKAWA hasa wakati wa chaguzi za kisiasa ni mikakati ya wazi ya CCM na serikali zake. Zaidi ya miaka 50 ndani madaraka CCM imeshindwa kujitathmini, kujuwa ni wapi inapojikwaa.

CCM Tanganyika na Zanzibar, wana changamoto nyingi za kuzitatua ili kurejesha imani za wananchi kuona kuwa kweli ni chama cha siasa kwa kuwa kimepoteza mwelekeo. Badala yake kimegeuka kuwa chama cha kuhujumu, kutesa na kuuwa.

Duniani kote, isipokuwa Tanzania na baadhi ya Mataifa ya Afrika, siasa ni suala linaloendeshwa kitaalamu na kistaarabu wala siyo mbinu na mabavu, kama inavyofanya CCM.

Tunapowaangalia na kuwasikiliza viongozi wa CCM katika mikutano yao ya kampeni za uchaguzi hata huu uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kindondoni, ni rahisi kubaini kuwa CCM kimeishiwa ajenda za kuwaeleza wapiga kura.

Wanachofanya, wanazungumza kama vile hawajawahi kushika dola na kumbe nusu karne, wao ndiyo watawala.

CCM kwa miaka 20 kimepoteza utawala Pemba, isipokuwa kinaendelea kuweka viongozi wake kwa mabavu, lakini kisheria hakina mamlaka. Hilo linafahamika mpaka Umoja wa Mataifa (UN).

Kadhalika, CCM kimepoteza utawala Ukerewe, Mwanza kwa miaka 15, kinahitaji kujitathmini, wala hakipaswi kutumia nguvu na mabavu kwa kuviamrisha vikosi vya Polisi, JWTZ na vikose maalum visivyojuilikana. Kikiendelea kufanya siasa za aina hiyo kitakuwa kinaongeza petroli kweny moto.

Jakaya Kikwete (Rais mstaafu), aliwahi kuwasihi CCM, kuacha siasa za kutumia vikosi vya Polisi ili kujipima nguvu na upinzani yaani kuweka mizani sawa ya ushawishi kwa wananchi. Hadi leo hilo limewashinda bado wamo ndani ya kwapa za Polisi.

CCM kiache mtindo wake wa siasa wa kutumia jasho la wananchi kuwanunua wapinzani, siasa aina hiyo zina mwisho. Kila ubaya ni siku 40 tu, hata wizi na uchawi vinabainika katika siku 40.

Kwa ufupi, ningeishauri CCM na serikali zake wapeleke bungeni mswaada wa kubadilisha sheria na katiba zao, mfumo wa chama kimoja cha siasa urejeshwe, ili wananchi wapumue. Pia, itarahisisha kumuongezea rais wao miaka saba, wapunguze kumwaga ovyo povu.

CCM, hadi lini itakuwa inakamata viongozi wa upinzani na wananchi kwa sababu za kijinga na kipuuzi. Kumkosoa au kumsifu (kumsifia) kiongozi wa nchi ni muono wa wananchi wanapoangalia utendaji wake.

Magufuli, kama anapenda kusifiwa kwa sifa nzuri, kwa sifa njema katika utawala wake aache kuvunja sheria na katiba za nchi katika kuwakandamiza wapinzani na wananchi wasiokubalina na siasa zake.

Magufuli, aruhusu shughuli za ustawi wa kisiasa kuendelea aondoshe vikwazo na sababu, hasa mikutano ya hadhara, maandamano na chaguzi zilizo huru, wazi na za haki, bila kuingiliwa na yoyote.

Aache vitisho na majigambo. Kufanya hivyo atapata kipimo cha wananchi wanampenda kiasi gani, yeye na serikali yake.

Zanzibar kuna nyimbo iliyoimbwa miaka ya nyuma 1970/80 na kikundi cha Mila na Utamaduni maarufu ‘culture’ Muimbaji Khamis Shehe: ‘tenda watu wataona majivuno weka kando’ katika wimbo wa ‘MAUMBILE SOTE SAWA’.

CCM, inapaswa kujitathmini na kubadilika kufanya siasa za kisayansi badala ya kuendelea kufanya siasa za ovyo ovyo za chuki, majungu, dhuluma na ubabe, dunia imebadilika. Hii ni karne nyingine. Jamii ya Watanzania inahitaji ustaarabu, inahitaji kuishi kwa amani na furaha..

Tagsslider
Share: