Habari

Uchafuzi wa Mazingira kuuwa Taifa

Na Mwajuma Juma, Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa taifa linaweza kuangamia kutokana na uchafuzi mkubwa wa kimazingira unaofanywa na baadhi ya wananchi kwa kisingizio cha kujitafutia maisha.

Hayo yameelezwa na Makamu wa pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi huko Bumbwini mkoa wa  Kasakazini Unguja,  baada ya kulikagua  eneo lililokatwa Minazi kwa dhamira ya kutaka kuchimbwa Mchanga  akiwa katika ziara yake ya kukagua miradi ya Maendeleo na ile ya Kijamii ndani ya Mkoa huo.

Amesema kuwa kuna uharibifu mkubwa wa kimazingira unaofanywa na baadhi ya wananchi kwa makusudi huku walidai kufanya hivyo kwa kisingizio cha kujitafutia riziki jambo ambalo linatakiwa kuwa macho na wahusika wa mazingira.

Amesema kuwa kutokana na kuwepo kwa hali hiyo kuna wajibu kwa viongozi na watendaji wa Serikali hususan wanaoshughulikia mazingira kuishajiisha jamii juu ya athari za mazingira kwa taifa.

Hata hivyo amesema shughuli za mazingira hivi sasa ni muhimu Duniani kutokana na athari zilizojitokeza  ambazo zinaashiria kuleta balaa katika baadhi ya Mataifa Duniani.

Amefahamisha kwamba pamoja na kuwa Serikali ilipiga marufuku zoezi la uchimbaji mchanga lakini bado kuna kila dalili zinazoonyesha baadhi ya Watu kujiandaa kuendelea na mpango huo.

Mapema Afisa Misitu  anayeshughulikia Mapato na Mashamba yote ya Serikali Bw. Mwinjuma Muharami alisema kibali cha kuruhusu uchimbwaji wa mchanga hutolewa baada ya uhakiki wa kuliona eneo husika kama halina uwezo wa uzalishaji wa mazao.

Amesema kuwa uhakiki huo umekuwa ukifanywa kwa pamoja na wawakilishi kutoka  Taasisi za Misitu, Mazingira, Masheha, Halmashauri, pamoja na Wilaya husika.

Hata hivyo amesema kuwa mpango maalum umeandaliwa wa kuoteshwa Miti ya kudumu katika Maeneo yote yaliyochimbwa Mchanga kwa lengo la kuhifadhi Mazingira na kurejesha haiba ya Maeneo hayo.

Share: