Habari

Uchaguzi wa marudio; CUF Zanzibar haishiriki wala haijakata tamaa – Maalim Seif

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, amesema wakati uchaguzi wa marudio Zanzibar ukitaraji wa kufanyika Machi 20, mwaka huu, anaamini Wazanzibari walifanya uamuzi wa kumchagua Rais, Wawakilishi na Madiwani katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015.

Matokeo ya uchaguzi huo yalifutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Oktoba 28, 2015 ambapo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa tume hiyo, Jecha Salim Jecha, alisema zipo kasoro mbalimbali zilizosababisha kufutwa kwa matokeo hayo.

Baadhi ya vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi huo Oktoba 25,2015, tayari vimetoa tamko la kutoshiriki uchaguzi wa marudio wakipinga uamuzi wa ZEC kufuta matokeo hayo.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Hindu Mandal ambako alipumzishwa juzi asubuhi kwa ajili ya matibabu na kuruhusiwa jana jioni.

Alisisitiza kuwa, ZEC haina mamlaka ya kufuta matokeo hayo hivyo CUF Zanzibar wanaamini kuwa, haki yao haitapotea kutokana na ushindi walioupata kwani Wazanzibari walishafanya uamuzi na msimamo wao ni kutoshiriki uchaguzi wa marudio.

Aliongeza kuwa, CUF hakiungi mkono uchaguzi wa marudio na tayari kimewataka wanachama wao kutoshiriki na hawatapeleka mawakala wao kwenye vituo vya kupigia kura.

Akizungumzia afya yake kwa sasa, alisema anaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo na baada ya wiki nane, atakuwa katika hali nzuri ya kuendelea na majukumu yake ili kuhakikisha matakwa ya Wazanzibari yanaheshimiwa.

“Jana (juzi), wakati natoka Zanzibar, kabla sijaanza safari ya kuja Dar es Salaam, nilijisikia kizunguzungu hivyo nilisaidiwa kupanda kwenye ndege na baada ya kufika, hali hiyo iliendelea hivyo nikakimbizwa hospitali ya Hindu Mandal.

“Baada ya kupatiwa matibabu hali yangu iliimarika na hivi sasa naendelea vizuri…lengo la safari yangu kuja Dar es Salaam nilikuwa nikutane na baadhi ya Mawaziri wa nchi za nje ambao niongee nao lakini sikuweza bali walikutana na viongozi wenzangu wa CUF, mazungumzo yalikwenda vizuri,” alisema.

Baada ya Maalim Seif kulazwa hospitalini hapo, viongozi mbalimbali wa CUF walikwenda kumjulia hali akiwemo Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano, Ismail Jussa, Naibu Katibu Mkuu, Nassoro Ahmed Mazrui, Juma Duni Haji, aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba na Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru.

MAJIRA

Tagsslider
Share: