Habari

Uchambuzi wa habari: ‘Vijana wakumbusheni wabunge, wawakilishi ahadi zao kwenu

January 8, 2018

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA:

TAKRIBAN ni miaka mwili, tokea wajumbe wa baraza la wawakilishi, waachane na makundi ya wananchi pale walipokuwa nao kwenye chochoro na viriri vya kuwaomba kura.

Si unakumbuka wawakilishi hawa na wabunge, walikuwa mithili ya mtu anaeposa kwenye nyumba asiotakiwa vyema, walikubali kukaa, kulala na kuzungumza na kila mmoja ili ammimininie kura.

Hapo wagombea hao, walikuwa na maneno kushinda asali kwa utamu, ingawa ilikuwa ni sehemu ya kampeni, kwa kuwataka wananchi na hasa kundi la vijana, kuwapa kura ili kisha wawatekekezee shida zao.

Wapo wabunge na wawakilishi waliowaahidi vitu vinono vijana hao, na ndio maana pengine leo hii, mbunge huyo ama mwakilishi ameshaivaa suti na tai, kwa kura ya kijana wa jimboni kwake.

Leo nawakumbusha vijana kwamba, lazima muwafuate na kuwakumbusha wabunge hao na wawakilishi, kwamba sasa watimize ahadi zazo, kwenu.

Uchaguzi si umeshakamilika, wameshaanza kupata visenti hata kupitia mfuko wa majimbo, sasa wafuateni viongozi hao, watekeleze pole pole ahadi walizowawekea wakati ule wao walipokuwa na shida.

Maana inawezekana, sasa wamesahau kuwa waliwaahidi nyinyi vijana mambo kadhaa, mfano kuimarisha vikundi vyenu vya ushirika, au kuwaanzishia mitaji, sasa wakati ndio huu kuwafuata kwa kifua mbele.

Walishatangaaza Ilani za vyama vyao na nyinyi mkazikubali, ndio maana alfajiri mlifika kwenye vituo vya kupigia kura, na kuzimimina bila ya hofu, mkijua kuwa mbunge huyo au mwakilishi, atatimiza ndoto zenu.

Husema waswahili kuwa, mwenye shiba hamjui tena mwenye njaa, sasa kama mnasubiri wawaite inawezekana mkaa sana hadi kufikiwa na kampeni nyengine.

Kama waliwaahidi kuwasomesha au kuwasaidia vifaa vya kisasa vya kuendeshea kilimo cha mboga mboga, basi hima na haraka kwa sasa wapo majimboni, lazima muwafuate kuwakumbusha.

Na kizuri zaidi wakati wa kuangalia ni mwanachama wa chama gani kwenye kutekeleza ahadi zao, hilo halipo maana kwa mbunge au mwakilishi alipata nafasi, sasa uchama haupo.

Kama ilivyo kwamba rais aliepo madarakani ni wa wananchi wote wa Zanzibar bila ya kujali chama, basi halikadhalika na mbunge, mwakilishi na hata diwani sasa ni wananchi wote.

Maana inawezekana mbunge au mwakilishi, pengine akatunisha mashavu na kuvimba akiendewa na vijana anaojua kuwa hawako chama kimoja, akijua kuwa anataka kitu gani kwake.

Hilo sitarajii lijitokeza, kwa kiongozi huyo, sasa lililopo mbele yake ni kufungua Ilani ya chama chake au karatasi alioitumia kuombea kura na kuwashawisha vijana kwamba akipata atawafanyia nini.

Maana rais wa wazanzibari wote, amekuwa akitekeleza ahadi zake ikiwa ni pamoja na nyongeza ya mishahara, kuwalipa wazee shilingi 20,000 kila mwisho wa mwezi waliofikia umri wa miaka 70, ujenzi wa miundombinu ya barabara na maji safi na salama bila ya kujali chama.

Sasa nanyi wabunge na wawakilishi wetu, mnangoja nini mbona wapo baadhi yenu mmekuwa kimnya kuwatekelezea ahadi zenu kwa vijana ndani ya majimbo yenu.

Kama hivyo ndivyo, lazima vijana na pengine kwa kutumia mabaraza ya vijana muwapitie hatua kwa hatua wabunge na wawakilishi wenu, ili kuona mnawakumbusha ahadi zao kwenu.

Lakini wabunge na wawakilishi wetu, tuseme mmesahau, hamkumbuki kuwa mliwaahidi vijana pindi mkizipata nafasi hizo, mtawafanyia moja mbili, tatu?

Lakini hata viongozi wa vyama husika, kupitia mikutano yenu mikuu ya vyama basi wakumbusheni, wahimizeni, waulizeni na wakaripieni viongozi hao wa majimbo, ili kuma wanatekeza ahadi zao kwa vijana.

Lakini hata wale waandishi wa habari pamoja na vyombo vyao waliokuwa mstari wa mbele kumnadi na kumtangaaza mgombea na sera zake, sasa mgeukieni kwamba azitekeleze.

Pemba Today

Share: