Habari

Uchambuzi wa Rasimu ya Katiba – Mamlaka ya wananchi

SEHEMU YA PILI

MAMLAKA YA WANANCHI, UTII NA HIFADHI YA KATIBA

6. Jamhuri ya Muungano ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia inayozingatia haki ya kijamii, na kwa hiyo:

(a) wananchi ndio msingi wa mamlaka za nchi, na Serikali itapata madaraka na  mamlaka yake kutoka kwa wananchi ambao kwa umoja na ujumla wao wanaimiliki na kuipatia Katiba hii uhalali;

7.-(1) Muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake, katika uendeshaji na utekelezaji wa shughuli zake utazingatia azma ya kukuza umoja wa kitaifa na kudumisha heshima ya Taifa.

(2) Kwa madhumuni ya masharti ya Ibara ndogo (1), mamlaka ya nchi na vyombo vyake vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote kwa lengo la kuhakikisha kwamba:

(b)sheria za nchi zinasimamiwa na kutekelezwa;

(h)mamlaka za nchi zinatoa fursa na haki zilizo sawa kwa wananchi wote, wanawake na waume, bila ya kujali rangi, kabila, nasaba, dini au hali ya mtu;

(j)utajiri wa rasilimali na maliasili za Taifa unaelekezwa katika kuleta maendeleo, kuondoa umaskini, ujinga na maradhi; na

(k)nchi inatawaliwa kwa kufuata misingi ya demokrasia na kujitegemea.

8.-(1) Bila ya kuathiri masharti ya Katiba za Washirika wa Muungano kwa mambo yasiyo ya Muungano, Katiba hii itakuwa sheria kuu katika Jamhuri ya Muungano.

(2) Mtu yeyote, chombo, taasisi, jumuiya na wakala wowote wa mamlaka ya nchi na mamlaka binafsi zinao wajibu wa kuzingatia masharti ya Katiba hii na kuyatii.

(3) Sheria yoyote, mila, desturi au uamuzi wowote wa chombo cha dola, ofisa wa Serikali au mtu binafsi ni sharti ufuate na kuendana na masharti yaliyomo kwenye Katiba hii na kwamba, sheria, mila, desturi au uamuzi wowote ambao hautawiana au kwenda sambamba na masharti ya Katiba hii utakuwa batili.

9.-(1) Mtu au kikundi cha watu hakitachukua au kushikilia mamlaka ya nchi isipokuwa kwa mujibu wa Katiba hii.

(2) Kitendo chochote kinachokiuka masharti ya Ibara ndogo ya (1) ni batili na ni kitendo cha uhaini kama itakavyoelezwa katika sheria za nchi.

(3) Kwa madhumuni ya kuhifadhi masharti ya Ibara ndogo ya (1) na (2), Serikali itaweka utaratibu wa kuisambaza Katiba hii kwa wananchi na kuiweka katika mitaala ya elimu ili kuwezesha wananchi kuifahamu, kuilinda na kuitii.

 

NOTE

Sijuwi tofauti na matumizi ya  “mamlaka za nchi” na “mamlaka ya nchi” pamoja na kuonekana ni tafsiri ya umoja na wingi lakini jee hivyo ndio ilivyokusudiwa.

Kwa vile Jamhuri za Muungano wa Tanzania sio ni Taifa, neno nchi bado linaendelea kutumiwa kuwavuruga wananchi.

Hivi kuna “maliasili za Taifa” zilizoingizwa katika katiba hii kuwa ni miongoni mwa mambo ya muungano. Vipi tuanze kujigawia.

Bila ya kuathiri masharti ya Katiba za Washirika wa Muungano kwa mambo yasiyo ya Muungano,

Hapa inahitaji ibadilishwe maneno badala ya “mambo yasiyo ya Muungano” na iwe “mambo yahusuyo Muungano”

Tuchukulie kuna mambo katiba za nchi washirika hazikusema kitu juu ya masuala hayo, hivyo ni kusema Katiba hii inajibebea. Huo ni upotofu.

Mtu yeyote, chombo, taasisi, jumuiya na wakala wowote wa mamlaka ya nchi na mamlaka binafsi zinao wajibu wa kuzingatia masharti ya Katiba hii na kuyatii. Hapa ilikuwa iekewe mipaka kwa yale mambo ya muungano na sio kuchwa wazi kiasi hichi.

Sheria yoyote, mila, desturi au uamuzi wowote wa chombo cha dola, ofisa wa Serikali au mtu binafsi ni sharti ufuate na kuendana na masharti yaliyomo kwenye Katiba hii na kwamba, sheria, mila, desturi au uamuzi wowote ambao hautawiana au kwenda sambamba na masharti ya Katiba hii utakuwa batili.

Hapa kwa ufupi tumepiga marufuku sheria za Kiislam kwamba ziweko chini ya katiba hii. Hili ni tatizo kubwa sana hata ikizingatiwa jamii imejengeka na inatofautiana kimila, desturi, nakadhalika. Kuna haja ya kupitiwa tena.

 

 

 

 

 

 

 


Share: