Habari

Uchambuzi wa Rasimu ya Katiba – Utangulizi

UTANGULIZI

 

KWA KUWA, Sisi, Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayoheshimu na kuzingatia misingi ya utu, uhuru, haki, usawa, udugu, amani, umoja na mshikamano katika nyanja zote za maisha yetu;

 

NA KWA KUWA, tunaamini kuwa misingi hiyo inaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye mfumo wa demokrasia na utawala bora ambayo Serikali yake inasimamiwa na Bunge lenye Wabunge waliochaguliwa na wanaowawakilisha wananchi na Mahakama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga wala upendeleo wowote, na kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinalindwa na kudumishwa na kwamba wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu;

 

NA KWA KUWA, umuhimu wa kutunza mali ya Mamlaka za Nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu, ubadhilifu, na kuhimiza matumizi bora na endelevu ya rasilimali na maliasili zetu pamoja na kulinda na kuhifadhi mazingira yetu kwa mustakabali wa maisha ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo;

 KWA KUWA, azma ya kujenga Umoja wa Bara la Afrika katika misingi ya Umajimui wa Afrika ambao inadhihirishwa na Muungano wa iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar;

 NA KWA KUZINGATIA, urithi tulioachiwa na Waasisi wa Taifa letu wa kujenga nchi yenye Umoja wa Watu wake ambao hawabaguani kwa misingi ya ukabila, udini, rangi, jinsi au ubaguzi wa aina nyingine yoyote;

 NA KWA KUZINGATIA, uzoefu wa zaidi ya Miaka Hamsini ya Uhuru na Miaka Hamsini ya Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na umuhimu wa ushiriki mpana na bayana wa wananchi katika utungaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Note

Kwa ufupi maneno yote niliyo andika kwa rangi nyekundu yanahitaji kufanyiwa marekebisho.

Msisitizo uwe kila panaposomeka neno NCHI libadilishwe na liwe TAIFA.

Mahkama haikutajwa kwamba ni suala la Muungano, hivyo orodha ya mambo ya muungano lazima itamke kuwa Mahkama nalo limo.

Unaposema “uzoefu wa zaidi ya Miaka Hamsini ya Uhuru” hapa lazima ielezwe ni uhuru wa nani. Kwani hapa kinachozungumzwa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

SEHEMU YA KWANZA

1.-(1) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Shirikisho lenye mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati za Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi huru.

(2) Jamhuri ya Muungano ni Shirikisho la kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, usawa wa binadamu, kujitegemea, utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu.

(3)Hati ya Makubaliano ya Muungano iliyorejewa katika Ibara ndogo ya (1) ndio msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba hii, kwa kadri itakavyorekebishwa, itakuwa ni mwendelezo wa Makubaliano hayo.

 

2. Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara ikijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar ikijumuisha sehemu yake ya bahari

3.-(1) Alama za Taifa ni:

(a) Bendera ya Taifa;

(b) Wimbo wa Taifa; na

(c) Nembo ya Taifa,

kama zitakavyoainishwa katika sheria itakayotungwa na Bunge.

(2) Siku Kuu za Kitaifa zitakuwa ni:

(a)Siku ya Uhuru wa Tanganyika, itakayoadhimishwa tarehe 9 Disemba;

(b)Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar, itakayoadhimishwa tarehe 12 Januari;

(c)Siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, itakayoadhimishwa tarehe 26 Aprili; na

(d)Siku Kuu nyingine zitakazoainishwa na sheria za nchi.

(3) Kila Siku Kuu ya Kitaifa itakuwa ni siku ya mapumziko.

NOTE

Neno “lenye mamlaka kamili” halitakiwi liwepo kwani kuna mamlaka nyengine Jamhuri ya Muungano haihusiki nazo. Ikumbukwe kwamba kuna mgawano wa madaraka. Sasa ukitowa kwa mamlaka kamili, vipi zile nchi washiriki umezichukulia mamlaka zao.

Unaposema “zilikuwa nchi huru”. Bado Tanganyika na Zanzibar ni nchi huru, hakuna nchi iliyoeteza uhuru wake. Hivyo isemwe

Nani mwenye mamlaka ya kuirekebisha Hati ya Makubaliano ya Muungano,Hili linahitaji mjadala.

Eneo la Jamhuri ya Muungano hili linahitaji kuelezwa kwa mipaka ya nchi washirika. Kama ilivyotajwa Jamhuri ya Tanganyika ielezwe mipaka yake halkadhalika Jamhuri ya Watu wa Zanzibar nayo ielezwe mipaka yake. Hapo ndio tupate mipaka ya Jamhuri.

Jamhuri isihusike na kutangaza sikukuu, hili liachwe kwa nchi washirika wao ndio watakaoamuwa siku zinazofaa kuwa sikukuuu. Jamhuri ya Muungano ni kuzitambua sikuuu zote pale nchi washiriki wakishazitangaza.


Share: