Habari

UCHOCHEZI NA KUPIMWA MKOJO HAVIENDANI.

Mheshimiwa Tundu Lissu amekamatwa tena na jeshi la polisi akiwa uwanja wa ndege wa Daressalaam akitokea Dodoma, ambako awali walitaka kumkamata huko huko lakini ilishindikana, baada ya Lissu ambae ni Rais wa chama cha mawakili wa Tanganyika kuhamia mahakamani na kukataa kutoka nje kwa muda mpaka pale alipohakikishiwa na afisa wa polisi kuwa hawatomkamata kwa siku hiyo.

Tanganyika kwa sasa kila anaetafutwa kwa upande wa wapinzani wa serekali hii ya Magufuli,ni lazima apimwe choo kidogo au kikubwa na mkemia mkuu wa serekali, ambae anatumiwa vibaya kwa maslahi ya kulinda ajira yake na kuisaidia CCM kuendelea kutawala, hata kama sasa tuna endesha siasa za vyooni.

Nilisema zamani kuwa hizi sio siasa tena, huu ni uhuni wa kisiasa unaoendelea sasa nchini kwao/kwetu,ccm tumeshindwa upinzani hatuuwezi ni vema tukakubali kuliko kuendesha nchi kama choo cha serekali.

Tanzania inapita katika kipindi kigumu sana kwa sasa,pande zote mbili za muungano wa Taifa hili hakuna tena sheria, POLISI ndio sheria za nchi sio katiba wala mahakama,mabunge yote ya nchi hii, yaani bunge la jamhuri, na baraza la wawakilishi, haya ni mali ya ccm,vyombo vyote vya ulinzi na usalama wa taifa hivi ni mali ya ccm,sasa kitengo kilichosalia ambacho dunia nzima huwa lazima kijitegemee, nacho tunakitaka, kitengo hiki ni MAHAKAMA, hapa ndio mahali pekee  ambapo haki  inatafutwa na kupatikana,sasa ccm na utawala huu, wameamua tuichukue na hiyo, ili tuitumie kuumaliza upinzani, na wale wote watakaobatizwa jina la ugaidi, hasa waislamu wenye misimamo tofauti na serekali.

Haya hayataki uwe mpinzani ndio uyaone au uyajue,yanataka uwe muungwana na hupendi dhulma tu inatosha, wala usiwe na elimu ya juu au ya kati,ya chini au usiwe nayo kabisa inatosha, muhimu ujue kuna MOLA na iko siku ya mwisho, utaulizwa jee sheikh, uljaribu japo kuyakemea haya, au ndio ulikuwa uanogopa kuitwa mpinzani? kama si kufungwa?

Sheikh Khalifa ambae hivi karibuni alijitoa muhanga kuwasemea mahabusu wa uamsho,tayari yuko polisi mahabusu kwa ajili ya kupata chai,wengi tulijua hayo yako njiani, japokuwa kuna mkanda mzima wa vidio uliorikodiwa maneno murua kabisa aliyosema kuinasihi serekali kuacha kuwanyanyasa Waislamu  wa nchi hii,hakuna uchochezi  hata herufi moja katika mkanda huu,lakini serekali ya Magufuli inataka isiulizwe wala isihojiwe na kiumbe yoyote yule.

Haitowezekana katika karne hii,hili tunajidanganya sana kudhani kutumia nguvu ndio tutaweza kuwanyamazisha watu, na tutaendelea kuwasweka mahabusu siku zote, halafu watu hao hao muda ukifika tuende tukawaombe kwa hisani zao na Mola wao watupe kura zao sisi CCM, binafsi nitamshangaa muislamu hata awe mmoja pekee, ambae ana akili timamu kama atakipigia kura chama changu basi huyu lazima mgonjwa.

 

Hujakatazwa kuwa mwanachama wa ccm lakini sio lazima ukipigie kura,mimi huwa sipendi siasa za udini, wala ukabili au za kikanda, lakini kwa mtindo huu unaofanywa na serekali hii kwa sasa, kuhusu kuwadhibiti masheikh na waislamu kwa ujumla, unategemea nini?kila muislamu wa nchi hii akiamua kuinyima kura ccm, chama hiki sio hakitoweza kuingia madarakani tu, bali lazima KITAKUFA na hili halitokuwa kosa kwa sasa au siku za usoni.

Chama kinachoendeshwa kwa misingi ya kibaguzi,iwe wa rangi,dini,kabila au sehemu wanakotoka wasukuma au waarabu huwa hakina maisha marefu,nani kasahau ubaguzi ulioendeshwa Zanzibar kuhusu machotara wakati wa uchaguzi halali na haramu?sisi wengi hatuna ‘amnesia’ na tunaweka kumbukumbu,haya sio mageni kwetu, tatizo hayazoweleki.

Wazanzibari ni lazima tuamke huu sio wakati wa kusinzia seuze kulala,Mheshimwa Tundu Lissu amejitolea siku tele kututetea sisi Wazanzibari, ni lazima tulipe fadhila hasa wakati huu mgumu kwake,tusikae kimya kama hiki cha masheikh wa uamsho,ni lazima tukubali kuwa ubaguzi wa dini pia haufai, isiwe kwa kuwa hivi sasa tunabaguliwa/tunashughulikiwa sisi, basi tena na sisi wakti ukiwadia, iwe ndio muda wa kuwatundika WAKRISTO misalabani, kama bwana Yesu au nabii Issa.

 

Tanzania haitowezekana kurudi nyuma kidemokrasia,haki za binaadamu na uhuru wa watu kutoa maoni yao kwa mujibu wa katiba, kwa sababu ya kiongozi mmoja au wawili wanaopita,hawa sio miungu ni watu kama sisi, vyeo tu vinawalevya,wamesahau kuwa cheo ni dhamana,waliyo kababidhiwa na wananchi kwa ajili ya kuwa saidia katika kuwatataulia matatizo yao na sio kinyume chake, yaani kuwatia matatizoni.

Asanteni.    Comrade.

 

MUNGU IBARIKI ZANIBAR/TANGANYIKA.

 

 

Share: