Habari

Ufagio wa umma unaposafisha Ikulu

Walipokua Jeshini Blaise Compaoré na Thomas Sankara

Raia mwema Ahmed Rajab

12 Nov 2014

Unapokua askari zima moto kazi yako inakuwa ni kuuzima moto. Hutarajiwi kuwa na mazoea ya kufanya utundu wa kuuwasha wewe moto na halafu kujidai kwenda kuuzima. Mtu kama huyo Wafaransa humuita ‘un pompier pyromane.’

Hivyondivyo Mfaransa mmoja aliye mchambuzi wa siasa za Burkina Faso alivyomuelezea Blaise Compaoré, Rais aliyepinduliwa wa nchi hiyo.

Compaoré alikuwa miongoni mwa marais kadhaa wa Kiafrika walioanzia jeshini na baadaye wakajikuta wamekalia viti vya enzi katika Ikulu za nchi zao. Wa mwisho kufanya hivyo ni Luteni-Kanali Isaac Zida aliyeshika hatamu za uongozi wa Burkina Faso baada ya Compaoré kuanguka.

Kabla yake alikuwa Field Marshal Abdel Fattah al Sisi wa Misri aliyejiuzulu jeshini Machi 26 mwaka huu na akatangazwa rasmi Juni 3 kuwa alishinda uchaguzi wa urais.

Miongoni mwa wanajeshi marais kuna walioondoka vitini mwao kwa usalama, kuna walioangushwa wakaanza kuzipiga mbio kwa izara kama alivyofanya Compaoré na kuna wanaovikalia kwa nguvu viti hivyo wakikataa kubanduka.

Ukanda wetu wa Afrika ya Mashariki una marais saba waliowahi kupitia jeshini: Pierre Nkurunziza wa Burundi, Isaias Afewerki wa Eritrea,Omar al Bashir wa Sudan, Salva Kiir Mayardit wa Sudan ya Kusini, Yoweri Museveni wa Uganda, Paul Kagame wa Rwanda na Jakaya Kikwete wa Tanzania.

Kusini mwa Afrika kuna José Eduardo do Santos wa Angola na Ian Khama wa Botswana. Felipe Nyussi, Rais mpya wa Msumbiji alipitia jeshini kwa muda mfupi alipokuwa kijana mdogo akiwa katika jeshi la Ukombozi la Frelimo na kupata mafunzo ya kijeshi Nachingwea, Tanzania

Ukanda wa Afrika ya Magharibi una wanne: Idris Déby wa Chad, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Equatorial Guinea,Yahya Abdul Aziz Jammeh wa Gambia na Mohamed Ould Abdel Aziz wa Mauritania.

Na sikuisahau Burkina Faso ambayo katika muda wa saa 48 baada ya kuangushwa Compaoré, watu wasiopungua watatu walijitokeza kila mmojawao akidai kwamba yeye ndiye Rais mpya. Marais watatu katika kipindi cha siku mbili wa nchi ambayo kwa muda wa miaka 27 ilikuwa ikitawaliwa na mtu mmoja.

Mmoja wa hao waliojidai kuwa ni marais alikuwa mwanamke na wawili wanajeshi.Kati ya hao wanajeshi aliyeweza kuushika usukani wa utawala ni Luteni-Kanali Isaac Zida ambaye ndiye atayesimamia kipindi cha mpito.

Compaoré alikuwa miongoni mwa marais wajanja barani Afrika. Ujanja wake ulidhihirika zaidi katika ule utundu wake wa kuwasha mioto na halafu kwenda kujaribu kuizima. Aliiwasha mioto hiyo nchi kadhaa kwa misaada ya kijeshi na ya fedha alizokuwa akipewa na Kiongozi wa zamani wa Libya, Kanali Mu’ammar Qadhafi.

Misaada hiyo ilimwezesha kuyaunga mkono makundi ya waasi wa Côte d’Ivoire, Guinea, Liberia na Sierra Leone. Ilikuwa taabu lakini kuiona mikono yake. Alifanya ujanja wa kuwaunga mkono kwa mbali waasi.

Anashutumiwa pia kuwasaidia chini kwa chini waasi wa Mali na Niger. Ndiyo maana Rais wa Mali, Ibrahim Boubacar Keita (IBK) na serikali yake wamekuwa meno wazi wakionyesha furaha yao kwa kuanguka kwake.

Baada ya kuzuka kwa maasi aliyoyachochea au kuyaunga mkono katika nchi za wengine Compaoré alikuwa wa mwanzo kujitolea kwenda kuleta suluhu. Madola ya Magharibi, hususan Ufaransa na Marekani, yakazidi kumpenda.

Madola hayo yalimuona kuwa yeye ndiye askari wao katika eneo lililokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe pamoja na ugaidi wa kimataifa, hasa katika eneo la Sahara. Ndo tukamshuhudia akisuluhisha mizozo ya Guinea, Mali na kabla ya hapo ya Côte d’Ivoire, alikozaliwa mkewe Chantal na ambako ndiko alikokimbilia.

Zaidi ya hayo Compaoré aliyaruhusu majeshi ya Marekani yaitumie yatakavyo ardhi ya nchi yake na aliiruhusu Ufaransa iwe na kambi zake za kijeshi.

Kwa vile alikuwa akiwafaa katika mikakati yao ya usalama, viongozi wa Ufaransa na Marekani wakifumba macho alipokuwa akiwasha mioto yake na kuwakandamiza wananchi wenzake. Walijifanya hawayaoni aliyokuwa akiyafanya.

Kwa hakika, madola ya Magharibi yalianza kumuangalia Compaoré kwa jicho la rehema tangu Oktoba 15, 1987 aliponyakua madaraka katika mapinduzi ya kijeshi yaliyosababisha kifo cha mwenzake Rais Thomas Sankara. Sasa Mariam Sankara, mjane wake Sankara, anataka Compaoré ashtakiwe kwa mauaji ya mumewe.

Wanaharakati wanaopigania haki za binadamu nchini Liberia nao wanataka Compaoré ashtakiwe kwa mauaji na makosa ya jinai ya kivita.Na kuna kadhia ya mwanahabari Nobert Zongo aliyeuawa Burkina Faso 1998.

Visa kama hivi vya ukiukwaji wa haki za binadamu, kuuawa mwanahabari na kuteswa au kudhalilishwa kwa wanahabari wengine yamewahi pia kutokea Tanzania.

Mwanahabari David Mwangosi aliuliwa na polisi Septemba 2012. Kadhalika watu hawajasahau mauaji yaliyotokea Zanzibar baada ya chaguzi za 2000 na 2005.

Na kama ilivyo Tanzania baada ya kuondoka kwa Julius Nyerere, ufisadi umekithiri pia Burkina Faso tangu Sankara auawe. Waafrika wa nchi mbalimbali walijikuta kama ni wao waliofiwa. Sababu ni namna Sankara alivyokuwa akiongoza nchi yake.

Sidhani kama tangu alipouliwa kikatili (maiti yake ilikatwakatwa na kuzikwa mahala pasipojulikana) pametokea kiongozi mwingine wa Kiafrika mwenye sifa kama zake. Huyu alikuwa kiongozi aliyeamini kwa dhati kwamba matatizo ya nchi yake hayawezi kutanzuliwa kwa ruzuku na misaada kutoka nje.

Sankara aliupunguza mshahara wake wa Urais na akawa analipwa dola za Marekani 450 tu kwa mwezi.Mali aliyokuwa nayo ilikuwa ni motokaa moja, baiskeli nne, friji moja, friza moja lililokuwa limevunjika na magitaa matatu. Akipenda sana kupiga gitaa, naye ndiye aliyeutunga wimbo wa taifa wa Burkina Faso.

Alikataa picha yake isitundikwe katika maofisi kama zinavyotundikwa picha za viongozi wengine wa Kiafrika. Alikuwa akijitetea kwa kusema “wapo Thomas Sankara milioni saba”. Aliwaamrisha watumishi wa serikali wawe wanavaa nguo za kitaifa, zilizoshonwa na washoni wa Kiburkinabé kwa kutumia pamba ya Burkina Faso.

Sankara aliligeuza duka la vyakula na vifaa lililokuwa likiwahudumia wanajeshi peke yao kwa bei rahisi na akalifanya duka kuu la mwanzo mjini humo kuwahudumia wananchi wote.

Aliziuza motokaa zote za serikali za aina ya Mercedes. Mawaziri wakawa wanapanda motokaa za aina ya Renault 5 ambazo kwa wakati huo ndizo zilizokuwa rahisi sana nchini humo.

Hatua yake nyingine iliyowafurahisha wananchi ilikuwa ni kupiga marufuku utumizi wa madereva wa serikali na aliharamisha mawaziri na wakuu wengine kusafiri kwa ndege kwa kutumia tiketi za daraja ya kwanza.

Sankara alitoa wito kuyataka mataifa ya Kiafrika yaungane kukataa kulipa madeni ya kigeni. Muhimu zaidi kwa wakulima wa Burkina Faso Sankara aliitwaa ardhi ya mamwinyi na kuwagaia wakulima wa chini.

Matokeo yake ni kwamba katika kipindi cha miaka mitatu tu uvunaji wa ngano ulipanda kutoka kilo 1,700 kwa hekta moja na kufikia kilo 3,000 kwa hekta hiyo hiyo moja.

Baada ya kumpindua Sankara, Compaoré alizibiruwa sera zote za Sankara. Burkina Faso ikakimbilia tena kuikumbatia Idara ya Mchango wa Fedha za Mataifa (IMF) na ikajiweka chini ya mbawa za Ufaransa na Marekani kiuchumi, kisiasa na kiulinzi.

Waburkinabé wengi wanaamini ya kuwa shida zao za kimaisha zimesababishwa na hatua za Compaoré za kuukumbatia ulibirali mamboleo na kuzifuta sera za Sankara.

Matokeo ya hayo ni kwamba licha ya kuwa ni nchi ya nne ya Kiafrika yenye kuchimba dhahabu kwa wingi bado wananchi wake ni hohehahe. Yaliyonufaika yalikuwa makampuni ya nchi za Magharibi.

Wakati huohuo ufisadi ukashamiri na watu walio karibu na Compaoré wakijiona kuwa wao ndio wenye kuimiliki Burkina Faso. Katika safu ya mbele alikuwa François Compaoré, mdogo wake Blaise Compaoré na aliyekuwa mshauri wake wa mambo ya uchumi.

Nakumbuka kama mwaka mmoja hivi uliopita mshauri mmoja wa kisiasa wa Rais Compaoré alinambia kwamba kama asilimia 80 ya matatizo yote yanayomkabili Compaoré yamesababishwa na huyu mdogo wake.

Tangu siku za Sankara Burkina Faso imekuwa na utamaduni wa kimapinduzi wa kupigiwa mfano. Mapinduzi ya Sankara yaliwaamsha Waburkinabé. Kipindi cha utawala wake (1983 hadi 1987) kilikuwa kipindi cha mwamsho mkubwa wa kisiasa na uanaharakati.

Ni rahisi kung’amua kwanini Compaoré aangushwe sasa na si kabla ya sasa. Utawala wake ulibadilika katika muda wa miaka 27. Mwanzoni ulikuwa wa kikatili na watu wakiishi kwa hofu.

Polepole watu wakaanza kutokwa na hofu. Compaoré naye akakua, akawa mtu mzima na akaacha kutawala kimabavu.

Mwaka huu akitaka kuibadili Katiba ya nchi ili apate muhula mwingine wa kutawala. Aliwahi kuibadili mara mbili alipokuwa na nguvu zaidi na watu wakimuogopa.

Uasi wa kijeshi uliotokea 20011 kuhusu mafao ya wanajeshi na kuruka kwa bei za bidhaa kuliishusha hadhi yake na kuwapa nguvu wananchi safari hii wajiandae kupambana naye.

Wananchi wakipinga asiibadili Katiba na walianzisha lile waliloliita vuguvugu la “Le Balai Citoyen” (Ufagio wa Raia). Na ni huo ufagio wa umma uliomfagia Compaoré. Kung’oka kwake kwa haraka kwenye madaraka kuliwashangaza wengi — madola ya Magharibi, jeshi lake, wanasiasa wake na hata wapinzani wake.

Huo ndio mwisho wa viongozi wasiowasikiliza wananchi. Sijui iwapo viongozi wa Chama cha Mapinduzi wanajifunza chochote kutokana na mkasa huo.

Raia Mwema Ahmed Rajabu

Share: