Habari

Ujenzi ‘Terminal III’ kumaliza kwa wakati – Dk. Sira

October 2, 2018

TATU MAKAME NA NASRA MANZI

WAZIRI wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Dk. Sira Ubwa Mamboya, amesema wizara inaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar na SMT, kuhakikisha mkataba wa fedha za ziada unasainiwa ili ujenzi wa jengo la abiria la uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume (Terminal III) ukamilike kwa wakati.

Alisema hayo wakati akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji ya Baraza la Wawakilishi.

Aidha alisema wizara inachukua kila aina ya mikakati na tahadhari kuhakikisha jengo hilo linakidhi viwango vya kimataifa.

Mapema wakichangia hotuba hiyo, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliishauri serikali kuweka simu za mkononi kwenye minara ya kuongozea meli, ili inapotokezea ajali iwe rahisi kuwasiliana.

Mwakilishi wa jimbo la Kijitoupele, Ali Suleiman Ali (Shihata) alisema kuwepo mawasiliano yaliyounganishwa na simu yatasaidia kupunguza maafa pale ajali zinapotokea kwa sababu waokoaji watawahi kufika eneo la tukio.

Aidha aliitaka mamlaka inayohusika na masuala ya mafuta, kufuatilia bei zinapopanda na kushuka ili wananchi wajue kinachoendelea.

Akiwasilisha hotuba ya kamati hiyo, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Suleiman Sarahani Saidi, alisema kamati hairidhishwi na ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja huo kutokana na kutoendelea kama ilivyopangwa awali ambapo ulipangwa kumalizika ndani ya miezi 18.

Zanzibarleo

Share: