Habari

Ujumbe wa UAE wakamilisha ziara yao kwa kutembelea Pemba

Daktari Mkuu wa Hospitali ya Wete Pemba, Dk Omar Issa (kushoto) akitoa maelezo kwa ujumbe wa wataalamu kutoka Umoja wa Nchi za Kiarabu (UAE) ulipotembelea sehemu mbali Hospitali ya Wete, Pemba leo Ijumaa, Agosti 10, 2018

Rajab Mkasaba wa Ikulu Zanzibar
Ijumaa, Agosti 10, 2018

UJUMBE wa wataalamu kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umetoa shukrani kwa mapokezi na ukarimu walioupata kutoka kwa wananchi na viongozi wa Zanzibar katika ziara yao ya siku tatu waliyofanya Unguja na Pemba.

Akitoa shukrani hizo baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Pemba, zikiwemo barabara, hospitali na bandari, Mshauri wa Waziri wa Nchi Ushirikiano wa Kimataifa wa EAU, Najla Al Kaabi alisema Wazanzibari wameonesha moyo wa upendo kwao, hivyo kuna kila sababu na wao kuonesha upendo katika kuhakikisha dhamira ya ziara yao hiyo inazaa matunda.

Najla Al Kaabi aliyasema hayo leo Ijumaa, Agosti 10, 2018 kwenye uwanja wa ndege wa Pemba baada ya kukamilisha ziara yao ya siku tatu visiwani humo iliyowezesha kutembelea barabara ya Chake Chake hadi Mkoani, Hospitali ya Mkoani ya Abdalla Mzee na Bandari ya Mkoani.

Kadhalika ujumbe huo ulitembelea Hospitali ya Wete, Bandari ya Wete na Kikundi cha Wajasiriamali cha Upendo cha Wete mjini na kupewa maelezo ya kutosha kutoka kwa wenyeji wao viongozi wa Idara za Serikali ya Zanzibar ambao walishiriki katika ziara hiyo.

Katika maelezo yake Mshauri huyo wa Waziri wa Nchi Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali ya UAE, alieleza kuwa Wazanzibari wameonesha upendo mkubwa kwake pamoja na ujumbe aliofutana nao kutoka UAE, hivyo kuna kila sababu na wao kuonesha upendo wao katika kuhakikisha azma ya ziara yao hiyo inazaa matunda.

Alisema ujumbe wake umepata fursa nzuri ya kujionea maeneo ambayo yamo katika makubaliano yaliofikiwa kati ya UAE na SMZ wakati wa ziara ya Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein aliyoifanya kwenye nchi za UAE mwezi Januari mwaka huu.

Najla Al Kaabi, alieleza kuridhishwa kwao na juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Zanzibar katika kuimarisha sekta za kiuchumi na kijamii na kusisitiza azma ya umoja wa nchi hizo za UAE katika kuunga mkono juhudi hizo.

Aidha, Mshauri huyo wa waziri wa nchi alieleza kuvutiwa kwake na wajasiriamali wa Kisiwani Pemba kwa jinsi wanavyopambana katika kujiimarisha kiuchumi na katika maisha yao kwa kujiendeleza katika shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kazi ya ushoni.

Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Taaluma wa Idara ya Mambo ya Afya ya Abudhabi Dk Ali AbdulKareem Al Obaidli kwa upande wake alipongeza juhudi za Serikali ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya na kueleza jinsi serikali ilivyoweka mazingira mazuri ya huduma za afya baada ya kutembelea Hospitali ya Wete na Hospitali ya Mkoani (Abdalla Mzee) na kuwaona wananchi wanavyopatiwa huduma.

Dk Ali Al Obaidli aliahidi kwamba atahakikisha Umoja wa Falme za Kirabu (UAE) unafanya juhudi za kuhakikisha inashirikiana na Serikali ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya Unguja na Pemba.

Akitoa shukurani kwa ujumbe huo kwa kukamilisha ziara yao Unguja na Pemba, Mshauri wa Rais wa Zanzibar, Masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa, Fedha na Uchumi, Balozi Mohamed Ramia alipongeza ujumbe huo kwa kazi kubwa waliyofanya ya kutembelea maeneo mbalimbali yalioanishwa katika ziara hiyo.

Pia, Balozi Ramia alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa taarifa za kutosha juu ya utekelezaji wa miradi iliyoanishwa katika ziara hiyo hatua kwa hatua.

Alisema Serikali ya Zanzibar itaendelea kuimarisha uhusiano wa kidugu uliopo baina ya watu wa Zanzibar na ndugu zao wa Falme za Kiarabu huku ikizingatiwa kuwa nchi hizo zina uhusiano wa kihistoria.

Wakati huo huo, Balozi Ramia alitumia fursa hiyo kuvipongeza vyombo vya habari vya ndani na nje ya Zanzibar kwa kuitangaza vyema ziara ya ujumbe huo wa wataalamu kutoka UAE tangu ulipowasili.

Share: