Habari

Upandacho ndio uvunacho

Baada ya Zanzibar kuifunga Tanganyika mabao mawili kwa moja, kumekuwa na shamrashamra na vijembe kwenye mitandao ya Kijamii. Tafauti na inavyopambwa na baadhi ya vyombo vya habari mbali mbali pamoja na Watawala, yanayoandikwa na kuzungumzwa tangu jana hasa kutoka Zanzibar hayaashirii mapenzi baina ya pande mbili za Muungano.

Kilicho wazi ni kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar haujaundwa kwenye misingi ya haki, mapenzi na usawa wa nchi zilizoungana. Yanayoandikwa kwenye mitandao ya kijamii hivi sasa yanabainisha kutokuwepo kwa mapenzi baina ya Wananchi wa pande mbili za Muungano. Hii inatokana na upande mmoja wa Muungano kujihisi unaonewa na upande mwengine wa Muungano. Jambo hili linaongezeka siku hadi siku kutokana na kutokuwepo kwa juhudi za maksudi kuyashughulikia malalamiko ya Zanzibar kwa zaidi ya miongo mitano tangu kuasisiwa kwa Muungano huu.

Wetu si muungano wa watu bali viongozi, hivyo ipo haja ya kuyasikiliza maoni ya Wananchi wa pande zote mbili za Muungano kwa mintaraf ya kuziridhisha pande zote mbili za Muungano pamoja na kujenga mapenzi baina ya watu wa pande mbili husika. Vile vile, ipo haja sasa ya kufikiria namna ya kuzitatuwa kero zilizopo kwa misingi ya haki na uwazi huku kipaumbele katika utatuzi huo kikiwa ni maoni ya Wananchi wa pande mbili husika.

Tusipoziba ufa tutajenga ukuta

Mohd Juma Abdalla
Zanzibar.

Tagsslider
Share: