Habari

UKO WAPI UTU WAKO?

Dr. Ali Mohammed Shein,
Rais wa Zanzibar
Ofisi ya Rais
P.O.Box 2422
Zanzibar – Tanzania.

Mheshimiwa Rais

Uko Wapi Utu Wako?

Nijambo lililo wazi na lililopo kwenye rekodi kuwa wewe ni mtaalamu mahiri uliyekhitimu katika vyuo vikuu mbali mbali duniani. Kama Wazanzibari ambao hatma ya nchi yetu kwa hivi sasa iko chini ya mikono yako, hatukuandikii kuhusu utaalamu wako; ila dhamira yetu ya kukuandikia ni kuutafuta ubinaadamu au utu wako. Uko wapi utu wako Dr. Shein?
Tunalitilia mkazo suala letu hilo kwa sababu moja kubwa. Nayo ni kwamba hapo mwanzoni ulipopewa madaraka kuna watu waliokubandika utukufu mkubwa. Watu hao walitufahamisha kuwa wewe ni mtu usiyetaka makundi. Aydhan, walitueleza kwamba ukishamaliza salaa zako hutoki nje na kwenda mabarazani. Kwa hivyo, tuna kila sababu ya kutumia vigezo vikali kukutathmini.
Mheshimiwa Rais, historia yako haina mizizi ya ukereketwa. Umeanzia kupanda ngazi za kisiasa kwa kuteuliwa na marais waliopita. Dunia nzima inajuwa kwamba wewe si mtu uliyepikwa kichama. Uongozi umekuteremkia kwa bahati. Ni matokeo ya mazingira ya wakati fulani. Hatudhani kuwa hata kama umewahi kusimamia kiti katika jimbo lolote la uchaguzi. Kama umewahi kufanya hivyo basi hujawahi kufuzu kwani tungelilikumbuka tukio kama hilo.

Tunakumbuka kwamba katika ule uchaguzi uliokupa ushindi wa Urais hujajishughulisha hata kujiandikisha kupiga kura. Siri ya kufanya hivyo unaijua mwenyewe. Mwenye Enzi Mungu akitaka riziki imuangukie mja wake basi ndio hivyo tena hakuna wa kuizuia. Kufumba na kufumbua umekuwa Rais wa Serikali ya Maridhiano inayotambuliwa na wengi kama Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), ambayo kuwepo kwake kumebarikiwa kwa kura ya maoni ya Wazanzibari walio wengi. Kwa muda wa miaka miwili sasa tumekuwa tukijitahidi kuamini kwamba yale mema tuliyoambiwa juu yako yalikuwa si uzushi. Lakini matokeo ya hivi karibuni yametufanya tutokwe na imani hiyo. Tumetokwa na imani hiyo kwa masikitiko makubwa. Jambo ambalo lenye kutusikitisha zaidi ni kuona kwamba wewe Rais wetu mpendwa, tuliyekuamini na kukuthamini umechagua kuwa upande wa wale wasioitakia mema Zanzibar. Ushahidi wa hayo ni vitendo vyako mwenyewe. Miongoni mwa vitendo hivyo vyenye kukatisha tamaa ni:

• Katika hotuba yako ya Eid umetoa pole kwa upande mmoja tu wa waathirika na kuusahau kwa makusudi upande wa pili. Hivyo sivyo inavyotakiwa, ukiwa wewe ni Rais wa nchi.
• Umeamua kukaa kimya huku wananchi wanapigwa, wanakamatwa na wanadhalilishwa kwa kufanyiwa kila aina ya idhilali.
• Wahuni kutoka chama chako (tunaona uzito kutumia neno hili ‘wahuni’ lakini hapana budi) wanahutubia katika majukwaa si matusi tu bali wanatoa matamshi ya kuangamizana raia; matamshi ambayo katika nchi zenye kufuata sheria na kuheshimu misingi ya
haki na demokrasia zingepelekea wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
• Viongozi wa Uamsho wamewekwa vizuizini katika hali isiyokubalika hata kwa sheria zetu sisi wenyewe.
• Tunathubutu kusema kwamba ulionyesha ishara ya kuelemea upande wa wale wenye kuleta fitina pale ulipomtoa katika Baraza la Mawaziri yule kijana aliyefanya kazi kubwa mpaka yakapatikana haya Maridhiano.

Mheshimiwa Rais, unajuwa fika kwamba wengi walishindwa huko nyuma kutufikisha penye utulivu na amani. Kwa kudra ya Mola Wetu na kwa baraka za Rais Mstaafu Amani Abeid Karume pamoja na Maalim Seif Shariff Hamad, Wazanzibari waliweza kuunda Kamati ya Maridhiano chini ya uongozi wa mzee wetu Hassan Nassor Moyo. Naam, Wazanzibari hao wameweza kutupa sote fahari kubwa na kutamka kwa kinywa kipana “Ndio Tumefanya”, “Ndio Tumeweza”. Hapa inabidi tukukumbushe kwamba wewe hukuwamo katika hili. Licha ya hivyo kwa muda mrefu umekuwa ukipokea pongezi kutoka sehemu mbali mbali na kutoka kwa Mabalozi wanaokutembelea.

Mheshimiwa Rais, ikiwa wewe ni mtu muadilifu na mwenye insafu inabidi ujiulize hivi kweli unastahiki pongezi hizo? Ama sisi kwa upande wetu na Wazanzibari walio wengi tunakuuliza nini kinachokuzuia kuienzi na kuitunza Kamati ile? Hivyo wewe kama Mzanzibari mwenye uchungu na nchi yako unaona ni sawa ufanyavyo kuwaachia wahuni wawakashif wajumbe wa Kamati ya Maridhiano, kuchochea chuki na kuleta suitafahamu katika nchi yetu ya Zanzibar?

Mungu akuhidini..

Wazanzibari Wenzako,

Kwa niaba ya Kamati

Hashil Seif Hashil

Zanzibar Committee for Democracy
Gustav Bangs Gade 11st, th
2450 Copenhagen SV
Denmark

17 November, 2012

Tagsslider
Share: