Habarihistoria

Ukweli kuhusu utumwa Zanzibar

Na Ahmed Ngwali.

Ukweli kuhusu Utumwa- Zanzibar,( Unguja na Pemba).

Nimeamua kuandika post hii baada ya kusoma post ambayo imeandikwa na PASCO mmoja wa wanajamvi maarufu katika mtandao wa JF.

Post yake ilikuwa na kichwa cha habari kama ifuatavyo:-
UDHALIMU WA WAARABU ZANZIBAR NA PEMBA KWA NDUGU ZETU WALI-TESWA-HASIWA-WALIBAKWA.

Hoja ya Pasco ilitegemea sana report ya commissioner Donald Mackenzie iliotolewa London mwaka 1895.

A report on slavery and slave trade in Zanzibar, Pemba.

Ambayo ilitayarishawa na The British and Sovereign Ant-Slave Society.

Ukweli wa Mambo.

Ikiwa kweli kisingizio cha mavamizi ya Zanzibar ni utumwa basi utumwa ulikuwepo nchi zote duniani, si Zanzibar tu.

Waliofanya biashara za utumwa ni watu wa kabila zote na dini zote, hata Wapagani wa kiafirika.

Lakini waliotia fora kwa ukatili na ukhabithi mkubwa katika biashara ya utumwa ni mataifa ya kizungu na khasa Waingezera na Wamarekani.

Leo wana uso wa kujigamba na kujidai kama eti wao ndio walio ondosha utumwa?

Ushahidi.

1. Sayyid Said bin Sultan alipiga marufuku biashara ya watumwa baina ya mamlaka zake na mataifa yote ya kikristo mwaka 1822.

2. Pia alizuwia kusafirisha watumwa kutoka Afrika kwenda Oman katika mwaka 1845.

3. Sayyid Barghash alipiga marufuku biashara ya watumwa katika mwaka 1872 na akalifunga soko la watumwa lililokuwepo Mkunazini, Zanzibar.

4. Dola za kizungu zilipiga marufuku biashara ya watumwa kwa hiyo inayoitwa Brussels Act katika mwaka 1890 (yaani Zanzibar iliutangulia ulimwengu mzima kwa miaka kumi na nane (18) katika kupiga marufuku biashara ya watumwa)

5. Sayyid Hamoud ambaye pia nae alikuwa Sultan wa Zanzibar alipiga marufuku kabisa utumwa wenyewe katika mwaka 1897 (yaani mwaka huo hapakuwa na mtu yeyote mtumwa katika mamlaka ya Zanzibar).

6. Waingereza walipiga marufuku utumwa Kenya mwaka 1912 (yaani miaka miaka 15 baada ya Zanzibar).

Katika Tanganyika Wajerumani waliendelea na utumwa kwa muda wote waliotawala na baada ya hapo Waingereza waliendeleza utumwa katika Tanganyika mpaka mwaka 1920 (yaani kwa muda wa miaka 23 baada ya Zanzibar).

Huu ndugu zangu ndio ukweli.

Utumwa khasa ulifanywa na wazungu sio waarabu.

Mwisho:

Katika nchi yetu ya Zanzibar sasa tumebaki Na Ukoloni mweusi kutoka Tanganyika licha ya kuwa tunajinata Na kujigamba kwamba tumejikomboa ili tujitawale, lakini hao wanaoripokwa haya inaonekana wazi kwamba wamelevya Na maslahi yao binafsi Na wengine pangu pakavu tia mchuzi hawana kazi hawana bazi wao ni bendera ipepee tu japo wale dongo.

Tagsslider
Share: