Habari

Utafiti wa mafuta kwa mtetemo wakamilika kwa mafanikio

DECEMBER 4, 2017 BY ZANZIBARIYETU
Utafiti wa mafuta kwa mtetemo wakamilika kwa mafanikio

NA MADINA ISSA

MKURUGENZI Mwendeshaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar, Omar Zubeir, amesema zoezi la utafiti wa mafuta na gesi kwa njia mtetemo (seismic) katika eneo la bahari, limefanikiwa licha ya kujitokeza changamoto.

Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya kukamilika zoezi hilo,katika ukumbi wa zamani wa baraza la wawakilishi Kikwajuni.

Alisema zoezi hilo limefanikiwa na muelekeo umeonekana unakwenda vizuri ambapo matumaini ya kupatikana mafuta yanaonekana kwa kasi kubwa.

Alisema zoezi limechukua takribani mwenzi mmoja ambapo lilianza Oktoba 28 hadi Novemba 28 mwaka huu.

Alisema katika zoezi hilo idadi ya mistari iliyofanyiwa utafiti ndani ya kitalu cha Pemba Zanzibar ilikuwa ni 62, huku idadi ya kilomita zilizofanyiwa utafiti ni 2,482.

Aidha alisema mistari iliyofanyiwa utafiti nje ya kitalu ilikuwa ni minne huku idadi ya kilomita zilizotafitiwa zilikuwa 333.6.

Alisema changamoto zilizojitokeza ni kuwepo wavuvi katika baadhi ya maeneo hali iliyosababisha shughuli za utafiti kusimama kwa muda.

Alisema kuna baadhi ya nyavu za wavuvi ziharibiwa na mamlaka imeahidi kulipa fidia.

“Hatua tulizozichukua ni kuhakikisha mkandarasi analipa fidia kwa uharibifu ulioripotiwa licha ya kuwa hakukua na idadi kubwa ya wavuvi waliojitokeza kulalamika,” alisema.

Alisema zoezi la utafiti sasa linatarajiwa kufanyika katika eneo la nchi kavu kazi ambalo itaanza karibuni na kuchukua zaidi ya miezi saba.

Zanzibar Yetu

Share: