Habari

Utandawazi usiruhusiwe kuharibu utamaduni wa mzanzibari – Maalim Seif

Hassan Hamad (OMKR).

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameitaka kamisheni ya utamaduni na michezo kuweka mikakati imara ili kulinda utamaduni na maadili ya Zanzibar yasiathiriwa na utandawazi.

Amesema utamaduni ni kielelezo mahsusi cha taifa ambacho kinapaswa kulindwa kwa nguvu zote, na kwamba kamisheni hiyo ina jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa vitu hivyo vinalindwa.

Maalim Seif ameeleza hayo katika kamisheni hiyo iliyoko Mwanakwerekwe wakati alipofanya ziara ya kutembelea taasisi mbali mbali zilizo chini ya Wizara ya habari, utamaduni, utalii na michezo.

Amefahamisha kuwa wakati serikali ikijiandaa kutekeleza mpango wake wa kuwa na utalii kwa wote, ni vyema kujiwekea mikakati ya kulinda utamaduni wa Zanzibar ambao kwa kiasi kikubwa unachangia maendeleo ya sekta hiyo nchini.

Katika ziara hiyo Maalim Seif alitembelea maeneo mbali mbali yakiwemo uwanja wa Amaan ambapo ameuagiza uongozi wa Wizara ya habari kuchukua hatua za haraka kudhibiti uchafuazi wa mazingira katika eneo hilo unaotokana na uchimbaji wa mchanga karibu na uzio wa uwanja Amaan.

Amesema iwapo hatua za haraka hazitochukuliwa, eneo hilo litazidi kuharibiwa na kupoteza hadhi yake, hasa ikizingatiwa kuwa tayari wamejitokeza wafadhili watakaoiendeleza hoteli ya uwanjani Amaan kuwa ya kimataifa.

Katika idara ya makumbusho na mambo ya kale, Maalim Seif ameitaka idara hiyo kufanya utafiti wa kina ili kuieleza kwa usahihi historia ya Zanzibar kwa wenyeji na wageni wanaotembelea makumbusho hiyo.

Amesema wageni wengi wamekuwa na hamu ya kuifahamu historia ya Zanzibar lakini watu wengine huipotosha kutokana na kutofanya utafiti wakati wanapotoa historia hiyo.

Mkurugenzi wa Idara hiyo bibi Amina Ameir Issa amesema idara hiyo imeweka mkazo wa kuyaendeleza maeneo ya kihistoria yakiwemo majengo, ambapo hadi sasa tayari majengo 85 Unguja na Pemba yameshatangazwa kuwa ya hifadhi.

Bi Amina amesema wanakusudia kuifanya makumbusho ya viumbe hai iliyopo Mnazi mmoja kuwa makumbusho ya mazingira ambayo itasaidia kuhifadhi viumbe mbali mbali vikiwemo vya baharini.

Amesema changamoto kubwa wanayokamiliana nayo kwa sasa ni mwamko mdogo wa wananchi kutembelea maeneo ya kihistoria ambayo ni muhimu katika kufahamu ukweli kuhusu historia na kujionea mambo mbali mbali ya kihistoria yaliyotunzwa katika makumbusho hizo.

Maeneo mengine aliyoyatembelea ni pamoja makumbusho ya kasri Mtoni pamoja na pango la kisima cha chini kwa chini lililoko mangapwani ambalo linasadikiwa kuwa lilifanyika kiasi cha miaka milioni moja na nusu iliyopita.

Share: