Habari

Utata kifo cha Karume: Chuki binafsi au mapinduzi? II

Nasaha za Mihangwa

Joseph Mihangwa

KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya toleo lililopita, tuliona jinsi Rais wa Serikali ya awamu ya kwanza Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Abeid Amani Karume, alivyouawa kikatili na wanajeshi wakati akicheza bao, Aprili 7, 1972 mjini Unguja.

Kwa kifupi, tuliona kwamba, kwa vigezo vyovyote vile vya utawala na uongozi, Karume alitawala kwa mkono wa chuma; alitawala kidikteta katika nyanja zote za maisha ya Wazanzibari kisiasa, kiuchumi na kijamii. Alikuwa kero pia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kwa Muungano.

Kwa kusema haya sina maana kwamba Karume hakutenda mema kwa Zanzibar na kwa Wazanzibari; bali najaribu kutafiti tu kuona ni mazingira na sababu zipi zilizochochea na kuharakisha kuuawa kwake; kati ya sababu hizi kuu za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimuungano. Kwa vyovyote vile, moja au zaidi ya mambo haya manne yalichangia.

Tunajua kwa mfano, kwa baadhi ya Wazanzibari, Karume alikuwa mtawala mkatili asiye na huruma wala hakujua kusamehe; lakini pia alikuwa na sifa za pekee nzuri kama kiongozi na binadamu; alikuwa mhimili na mtetezi wa Waafrika wa Kizanzibari na hakuyumbishwa na siasa za migogoro Visiwani.

Alikuwa mwenye fikra zenye kujitegemea, alifanya maamuzi yake bila woga wala kuhofia matokeo; alikuwa kiongozi mwenye kuthubutu na mwenye kujituma.

Mwisho tutaona jinsi mpango mzima wa mauaji ulivyoandaliwa kwa wasomaji kuona kama ilikuwa chuki binafsi au mapinduzi. Si madhumuni ya makala haya kumwona Karume kama dikteta mwema (benevolent dictator) au dikteta katili (ruthless tyrant), maana hilo ni jambo la maoni ya kila mtu binafsi.

Alitawala kwa mkono wa chuma

Tumeona jinsi Karume alivyoitawala Zanzibar kwa mkono wa chuma, na namna alivyowaengua wote aliodhani hawakuwa upande wake, ama kwa kuwahamishia kwenye Serikali ya Muungano, ama kwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Sambamba na hatua hiyo, jamii ya Kiarabu wasio Wazanzibari, iliamriwa kuondoka, na wale Waarabu raia waliobaki waliishi chini ya jicho kali la Serikali; waliweza kukamatwa, kama Wazanzibari wengine na kutiwa kizuizini bila kufunguliwa mashitaka. Walifanyiwa jinsi serikali ilivyofikiri inafaa; mashamba na mali zao zilitaifishwa bila kufidiwa.

Wapo waliohukumiwa na “Mahakama ya wananchi” (tutaiona baadaye), kifungo na kuchapwa viboko kuonyesha kwamba Serikali ya Karume haikuwa ya mchezo; akaionya jamii ya Ki-Athnasheri wa Kiajemi kwamba kama wangeendelea kuleta “mgogoro”, wangefukuzwa wote Zanzibar licha ya kuwa raia.

Alitawala bila Sheria wala Katiba

Karume alitangaza utawala wa chama kimoja cha ASP na kuamrisha kila Mzanzibari mtu mzima, kuwa mwanachama. Kila familia ilitakiwa kutundika picha ya Karume nyumbani; kutofanya hivyo lilikuwa kosa la jinai lenye adhabu kali.

Kikosi cha Usalama wa Taifa chini ya Kanali Seif Bakari, kilichopewa jina la “Viwavi Jeshi”, na kufunzwa Ujerumani Mashariki kikaiva kwa mbinu za utesi na mauaji, kilipewa mamlaka ya kukamata, kutesa, kutia kizuizini na hata kuuwa bila mashitaka. Yeyote aliyelalamika, hata juu ya upungufu wa chakula tu, aliitwa “adui wa Mapinduzi” na hivyo mhaini. Enzi hizo, nduguyo akigongewa mlango usiku na kutakiwa kwa mahojiano na Serikali, usingemwona tena milele.

Wakati wa Karume hapakuwa na utawala wa Sheria wala Katiba; amri za rais (decrees) ndizo zilizotawala nchi. Mapema mwaka 1966, mfumo wa mahakama wa kawaida ulipigwa marufuku; na Oktoba 1966, rais alijipa madaraka ya kuteua mahakama maalumu za watu wasiozidi 14 wenye mamlaka ya kusikiliza kesi za makosa ya kisiasa kama vile uhaini, uhujumu uchumi na wizi wa mali ya umma.

Mahakama hizi hazikufungwa na kanuni zozote katika kusikiliza kesi; huduma za kisheria kwa watuhumiwa zilifutwa na mawakili kupigwa marufuku Zanzibar. Upande wa mashitaka ndio uliokuwa pia upande wa utetezi; kwa maana kwamba, mwendesha mashtaka wa serikali alipomaliza kuwasilisha mashtaka dhidi ya mtuhumiwa aligeuka kuwa mtetezi wa mtuhumiwa.

Mahakama hizi zilipewa uwezo wa kutoa hukumu za kifo. Mwaka huo huo (1966), Baraza la Mapinduzi lilipiga marufuku pia haki ya kukata rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashariki [EACA] na rufaa zote zikawa kwa Rais Karume pekee.

Mwaka 1970, Karume alipitisha amri (decree) ya kuanzishwa mahakama (za kienyeji) za watu watatu. “Mahakimu” wapya wa mahakama hizo waliteuliwa na Karume mwenyewe kutoka miongoni mwa makada wa ASP.

Moja ya sifa ya kuteuliwa ni kutokuwa msomi wa sheria, na ikiwezekana uwe hujui kusoma na kuandika. Adhabu ya kifo ilipanuliwa kuingiza makosa kama vile utoroshaji wa karafuu, uhaini na utoaji mimba. Matumizi ya vidonge vya uzazi wa majira lilikuwa kosa kubwa pia.

Karume alichochea hasira na chuki kubwa ya Wafanyabiashara wa Kiasia mwaka 1971, pale alipowapa notisi ya mwaka mmoja kufungasha virago kwa madai ya kuonekana kudhibiti uchumi wa Zanzibar. Hasira yao iliungana na ile ya Waarabu ugenini waliofukuzwa mwaka 1964 na kupokonywa mali na mashamba yao bila kulipwa fidia; achilia mbali wale ambao mabinti zao waliozwa kwa nguvu kwa Wazanzibari Waafrika.

Wakati huo huo, Karume aliendelea kuwaachisha kazi na kuwatimua Visiwani, watumishi wa serikali waliojulikana au ndugu zao kuwa wafuasi wa zamani wa vyama vilivyopigwa marufuku vya ZNP na ZPPP na nafasi zao kujazwa na “watiifu” kwake. Hata hivyo, kwa huruma ya Nyerere, walipewa utumishi serikalini Tanzania Bara.

Mapema mwezi Januari 1972, Waziri mdogo, Ahmed Badawi Qualletin, na afisa mwingine wa Serikali, Alli Sultani Issa, walifukuzwa kazi. Kisha, Februari 1972, ujumbe mzito wa watu sita ulitumwa kwa Nyerere kumwambia awarejeshe Zanzibar, Abdulrahman Babu na wenzake kadhaa wakahojiwe kwa tuhuma za kutaka kuiangusha Serikali.

Babu ambaye alikuwa bado mwenye ushawishi mkubwa wa kisiasa Zanzibar, na aliyeamua kutorejea Zanzibar ya Karume kwa kuhofia usalama wake, kivuli chake na mzimu wa wahanga wa ukatili vilimtisha na kumnyima usingizi Karume, mithili ya Macbeth kwa mzimu wa Mfalme Duncan na Banquo, aliowaua kwa upanga ili atawale.

Nyerere, kwa kuhofia yaliyompata Hanga, Twala, Othman Sharrif na wengine kutokea alipowarejesha Zanzibar mwaka 1967, safari hii alikataa kumrejesha Babu Zanzibar, ingawa alikubali shinikizo la Karume la kumwachisha uwaziri katika Serikali ya Muungano.

Karume aliwatimua pia wataalamu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na kufunga Kituo chao cha Utafiti na Udhibiti wa malaria Visiwani kwa madai kwamba, Wazanzibari walikuwa “malaria proof”, yaani hawaguswi wala kuugua malaria.

Kwa hatua hiyo, ugonjwa wa malaria uliongezeka kwa asilimia 45. Na ingawa Zanzibar ilikuwa na akiba kubwa ya fedha za kigeni, zaidi ya pauni za Uingereza milioni 14 kwenye Benki ya Urusi mjini London, (taarifa nyingine zinadai dola milioni 80), Karume hakuwa tayari kutumia fedha hizo kudhibiti malaria wala kuagiza chakula; badala yake akaona muhimu zaidi kuanzisha kituo cha televisheni ya rangi na ya pekee barani Afrika wakati huo.

Mwaka huo huo (1971), katikati ya mrindimo wa njaa Visiwani, Karume alipiga marufuku uagizaji wa chakula (mchele, sukari, unga wa ngano) kutoka nje, kama hatua ya kujitegemea kwa chakula.

Hatua hii ilizua tafrani na malalamiko na kusababisha biashara ya magendo ya chakula kushamiri; hapo, “Viwavi Jeshi” na mahakama za “kangaroo” zikapata wahanga kukamatwa, kushitakiwa na kunyongwa. Watu wengi wakaikimbia Zanzibar. Aprili 1972, ukosefu wa chakula ulikithiri. Ni wakati huo Rais Karume alipouawa ghafla.

Kwa yote hayo, pamoja na tabia yake ya kutoamini wasomi na kuchukia wataalamu, Karume hatimaye alianza kuchukiwa pia na Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi wenye siasa za mrengo wa ki-Karl Marx.

Karume adha kwa Nyerere na Muungano

Nyerere alikuwa ameyatoa sadaka mengi ya Tanganyika kwa Zanzibar, ilimradi tu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ufikiwe. Kwa mfano, wakati Tanganyika ilipoteza hadhi ya kuwa nchi na baadaye jina lake, pale Muungano ulipobadili jina kutoka “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar”, kutwa “Jamhuri ya Muungano wa Tan-zan-ia”, Zanzibar ilibakia kuwa Zanzibar, na Karume akabakia Rais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania.

Si hivyo tu, Wazanzibari watano walipewa uwaziri kamili katika Baraza la Mawaziri 14 la Muungano. Na ingawa idadi ya Wazanzibari ilikuwa asilimia tatu tu ya Watanganyika, lakini Zanzibar iliruhusiwa kuwa na Wabunge 52 katika Bunge la Muungano, wakiwamo Wajumbe wote 32 wa Baraza la Mapinduzi.

Licha ya upendeleo huu, Nyerere hakufanikiwa kudhibiti mhimili wa kisiasa Zanzibar chini ya Karume. Mfano, Zanzibar chini ya Karume, ilikataa kuhamishia kwenye Muungano mambo mengi yaliyopaswa kuwa chini ya Serikali ya Muungano; kwa mfano, iliendelea kudhibiti jeshi lake la ulinzi na Idara ya Uhamiaji, Karume akiwa amiri jeshi wake Mkuu. Ndiyo kusema, aliuawa na wanajeshi wa jeshi lake la Zanzibar, si Wanajeshi wa JWTZ.

Karume alikataa Serikali ya Muungano kugusa akiba ya fedha za kigeni ya Zanzibar, japokuwa fedha lilikuwa jambo la Muungano. Aidha, Karume na Baraza lake la Mapinduzi walikiuka mara nyingi mapendekezo ya kisera kutoka Bara kiasi kwamba Nyerere hakuwa na kauli tena juu ya sera za kiserikali.

Karume akakataa pia mazungumzo zaidi ya kikatiba kwa hofu ya Zanzibar kupoteza hadhi na mamlaka yake. Karibu kila alichopendekeza Nyerere, alipata jibu la mkato kutoka kwa Karume: “Kama hivyo ndivyo, tuvunje Muungano”.

Mitazamo hasi ya viongozi hawa wawili juu ya Muungano, ndiyo iliyosababisha mchakato wa kupata Katiba ya Muungano ndani ya mwaka mmoja kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano usifanyike, na Muungano kuongozwa kwa Katiba ya Muda kwa miaka 13 hadi 1977 na baada ya Karume kufariki.

Nyerere alipowasilisha na kupitishwa kwenye Bunge la Muungano, Mpango wa kwanza wa Maendeleo wa miaka mitano, na kutangaza nia yake kuona unatumika pia Visiwani, Karume aliupinga; akaja na mpango wake tofauti wa miaka mitatu kwa Zanzibar ulioandaliwa na mchumi kutoka Ujerumani Mashariki.

Kwa yote hayo na mengine, Nyerere alianza kuonyesha dhahiri chuki yake kwa utawala wa kimabavu wa Karume. Naye (Karume) alipotambua hilo, alizuia mwingiliano huru wa watu kati ya Visiwani na Tanzania Bara kwa hofu na kwa sababu zinazofahamika.

Si mara moja, hofu na wasiwasi wa kimaasi vilipojionyesha Zanzibar, mamlaka za usalama zilimshauri Mwalimu kufuta ziara zake Visiwani. Hofu hizi zilijidhihirisha zaidi pale Othman Sharrif, baada ya uteuzi wake wa Ubalozi Marekani kufutwa kwa shinikizo la Karume na kurejea Zanzibar, alipokamatwa na kutiwa kizuizini bila kosa.

Ilibidi Nyerere aingilie kati na kumwita Karume Ikulu, kuonyesha jinsi alivyochukizwa na kitendo hicho; lakini Karume alimkatalia, kuonyesha kwamba Nyerere hakuwa na mamlaka kwake. Sharriff aliachiwa baadaye kwa hiari ya Karume, na Nyerere akamteua kuwa Afisa Mifugo Tanzania Bara.

Hata hivyo, Oktoba 1969, wakati Nyerere akiwa ziarani nchi za nje, Sharrif alikamatwa Tanzania Bara na kurejeshwa Zanzibar alikouawa.

Zipi adha nyingine kwa Nyerere? Ni nani huyu Luteni Hamoud Hamoud? Kwa nini aliongoza mauaji ya Karume?

Share: