Habari

Utawala wa mtu mmoja una hatari ya kuliporomoa taifa

Julius Sello Malema (born 3 March 1981) is a Member of Parliament and the leader of the Economic Freedom Fighters (EFF). Picture from Wikipedia

by Ahmed Rajab – Rai Mwema
Januari 25, 2018

JULIUS Malema, kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Afrika Kusini, ni mwanasiasa mwenye tabia ya kukiudhi chama cha African National Congress (ANC) na serikali yake kila anapofungua mdomo wake.

EFF ni kirembwe cha ANC, chama kilichozaliwa 1912. Kwa upande wake, EFF kiliasisiwa 2013 na Malema pamoja na washirika wake walipofukuzwa kutoka umoja wa vijana wa ANC.

Malema amekuwa mwiba unaoichoma ANC tangu akiwa ndani ya chama hicho na ndiyo maana akafukuzwa pamoja na wafuasi wake.

Wanakiona chama cha ANC kuwa ni chama kisichopigania maslahi ya mwananchi wa kawaida na kwamba kinauacha uchumi wa Afrika Kusini uendelee kudhibitiwa na mabepari wa Kizungu.

Ukimsikiliza Malema anapokuwa anahutubia unaweza ukadhani kwamba labda ni mbaguzi mwenye chuki dhidi ya Wazungu pamoja na Wahindi wa Afrika Kusini ambao anasema wanawabagua na kuwaonea Waafrika.

Chuki zake dhidi ya Wahindi zimezidi baada ya kuibuka ushahidi wa kwamba Rais Jacob Zuma ana uhusiano wa chanda na pete na familia ya Gupta, familia ya mabepari wa Kihindi wazawa wa India wenye kumiliki biashara kubwa kubwa Afrika Kusini.

Akina Gupta wamekuwa na ushawishi mkubwa katika serikali ya Afrika Kusini kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu waseme kuwa familia hiyo ni kama “serikali kivuli” nchini humo.

Ufisadi wa hali ya juu umeibuka katika uhusiano huo baina ya familia ya Gupta na Zuma binafsi pamoja na kampuni yake Zuma iitwayo ‘Oakbay Investments.’

Raia Mwema lilipokuwa kifungoni Malema alipata nafasi mwezi Oktoba kuhutubia jumuiya ya mijadala ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza, iitwayo Oxford Union.

Jumuiya hiyo, mara kwa mara huwaalika wahutubu wa kimataifa kwenda kuhutubu na halafu hupigwa maswali na wanafunzi au kujadiliana.

Miongoni mwa wahutubu mashuhuri kutoka nje ya Uingereza, alikuwa Malcolm X, mwanaharakati wa Kimarekani aliyekuwa na asili ya Kiafrika na mtetezi wa haki za kiraia huko Marekani.

Malema hakuwa mgeni katika ukumbi wa Oxford Union kwa sababu alishawahi kuhutubia hapo miaka ya nyuma. Kuna wanaomshutumu kuwa mbaguzi na kuna wasemao kwamba ni mpumbavu. Lakini anaposimama na kuhutubu lazima umsikilize.

Mara nyingi anapohutubu hutema machungu ambayo watawala huwa hawataki kuyasikia. Safari hii aligusia jambo ambalo nadhani watawala wengi wa Afrika wanafaa walitie maanani.

Alieleza kwa nini Mataifa Barani Afrika hushindwa, yasijiweze, yasiweze kujiendesha. Haya ni mataifa yaliyoanguka yasiyoweza kusimama na kujikimu kwa njia zozote zile. Ni mataifa yaliyofeli.

Malema alieleza kwamba mataifa hayo huwa hivyo kwa sababu ya mtu aitwaye “rais”. Alichokusudia kusema ni kwamba ni marais, kwa vitendo vyao, wenye kuugeuza utawala wa kidemokrasia na kuufanya uwe utawala wa mtu binafsi. Badala ya kuziheshimu taasisi za dola, wao huzichimba na hujiheshimu wenyewe tu.

“Ikiwa rais hapendi kofia nyekundu au T-shati basi sheria hutungwa kuzipiga marufuku kofia nyekundu” au T-shati. Kwa hakika, wakati mwingine hata sheria hazitungwi kuvipiga marufuku hivyo visivyopendwa na rais.

Wananchi hushtukia tu wameingia matatani wanapovaa nguo zisizopendwa na rais au na wapambe wake. Hutokea hata kuimba nyimbo Fulani kukawa jambo la hatari.

Utumbo huo hautokei katika nchi zenye utawala bora, zenye kuheshimu sheria, taasisi za kisheria na haki za wananchi kama zinavyoelezwa ndani ya katiba za nchi.

Uozo huo hutokea katika nchi zenye utawala wa mtu mmoja binafsi pale serikali inapoonekana kuwa inaendeshwa na huyo mtu mmoja.

Tunapozungumzia utawala wa kibinafsi huwa hatumkusudii mtawala bali aina ya utawala wake. Kila mtawala huyo anavyozidi kutawala binafsi ndivyo anavyozidi kutawala kama mfalme. Huwa hana wa kumzuia. Taasisi za kisheria huwa ama zimedhoofishwa au zimeuliwa kabisa.

Matamshi ya Malema yalinifanya niukumbuke utawala wa Mfalme Charles wa Kwanza wa Uingereza aliyeanza kutawala 1625. Licha ya kwamba utawala huo ulikuwa wa kale wa karne ya 17 na kwamba haukuwa wa Kiafrika, hata hivyo, kuna mengi tunayoweza kujifunza kutokana nao.

Charles alikuwa mtoto wa Mfalme James wa Kwanza na alikuwa na mawazo sawa kama ya baba yake kwamba mfalme lazima awe na majukumu ya kifalme na akiwa nayo hayo majukumu ya kifalme lazima pia awe na haki za kifalme.

Miongoni mwa haki hizo ni haki ya kutawala ambayo wakiamini walipewa na Mungu. Hivyo, pia ndivyo mtawala wa leo wa kibinafsi, Barani Afrika, anavyoamini. Kwamba yeye ni chaguo la Mungu.

Kwa vile Charles, akiamini ya kwamba alikuwa na haki za kifalme za kutawala hakuona kwamba palikuwa na haja ya kuwa na bunge, kwamba bunge halipaswi kuyapinga maamuzi yake. Akiamini kwa dhati kwamba maamuzi yake yalikuwa sahihi. Hawezi kukosea.

Kwa sababu hiyo alikuwa akilifungua na kulifunga bunge atakavyo na atakapo. Hakuwa na haja nalo. Wanachofanya watawala wa leo wa Afrika wasiojali katiba na sheria za nchi ni kuligeuza bunge liwe bunge bwege lisiloweza kuisimamia ipasavyo serikali.

Ile miaka ambapo Charles wa Kwanza alitawala Uingereza bila ya kulishauri bunge inajulikana kama “miaka kumi na moja ya utawala wa mabavu”.

Katika kipindi hicho bunge lilikuwa halikutani na, kwa hivyo, sheria mpya hazikuweza kutungwa na kupasishwa. Aina ya utawala uliokuwapo katika kipindi hicho ulihatarisha shughuli za kisiasa, sera za mambo ya nje, bajeti ya nchi na hata mambo ya dini.

Tagsslider
Share: