Habari

UVCCM: Kuna mawaziri, wawakilishi waasi tuwashuhulikie

na Hassan Ali Ame, Zanzibar

VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameanza kutafunana baada ya kushutumiana kuwa miongoni mwao kuna mawaziri na wawakilishi wanafiki wasioheshimu sera zao, misimamo na kukiuka Katiba ya Zanzibar.

Hayo yalisemwa juzi mjini hapa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) Zanzibar, Sadifa Juma Khamis, kwenye kongamano la umoja huo.

Sadifa alisema wapo mawaziri na wawakilishi wanaoota kwamba ikiwa CCM itaondoshwa madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 watapata nafasi kupitia Chama cha Wananchi (CUF), jambo alilosema kuwa ni usaliti na uasi usiovumiliwa.

Alisema kutokana na ukiukaji wa maadili na misimamo ya chama hicho wanashindwa kukitetea pale kinaposhambuliwa na wapinzani nje na ndani ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

“Tunakaangwa kwa mafuta yetu wenyewe, watu tuliowakabidhi dhamana na amana hawatendi haki na kutimiza wajibu wao… hawa ni zaidi ya wasaliti na wavurugaji wakiachwa hivi hivi hadi mwaka 2015 watatumaliza,” alisema Sadifa.

Mwenyekiti huyo alisema kitendo cha kuendelea kuwavumilia viongozi hao kinazidi kuwakera wananchi na kutaka hatua za kinidhamu kuchukuliwa kabla ya jahazi lao halijaenda mrama.

“Kila mmoja anaweza kuwa mwakilishi na waziri, anayetuzunguka na kujipendekeza kwa wapinzani atupishe, anayeota kuwa CCM itashindwa mwaka 2015 asahau… hatutakubali kuwavumilia wasaliti,” alisisitiza.

Awali akifungua kongomano hilo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, aliwataka mawaziri na wawakilishi wa chama hicho kutambua majukumu waliyokabidhiwa na wananchi, kulinda Katiba ya Zanzibar na kutokubali sheria zivunjwe.

Vuai alisema vitendo vya kihalifu na hujuma vinavyotokea Zanzibar vimepewa kisogo na wawakilishi na mawaziri kushindwa kukemea vitendo hivyo wakati ni kinyume cha misingi ya haki za binadamu na sheria.

Akizungumzia baadhi ya misikiti kufanya kazi za kisiasa Zanzibar, Vuai alisema si vema vyumba za ibada kutumika kwa kazi hizo na kuwatahadharisha wanasiasa hao.

Chanzo Tanzania Daima

Share: