Habari

Uzalendo na umoja wa Wazanzibar ndio silaha ya kumshinda aduwi yetu

Mzeekondo
12 Januari, 2018 at 20:20

Demokrasia ni neno linalo pendwa sana na wana siasa hasa Madikteta, kwa sababu neno hilo ni “chaka” lao la kifichia maovu yote wanayo fanya katika tawala zao. Afrika neno hili utalisikia sana kutoka katika vinywa vya watawala wetu. Mara zote huwa hata wao hawamini wanayoyasema, au kutamka hadharani, ndani ya mioyo yao, wanajua kuwa wanachokihubiri ni wajibu tu. Lakini mfumo wa kututawala halisi ni ule wa kutulazimisha kuiabudu demokrasia ya mdomo na sio vitendo hata kama kila kukicha mazombi na vikosi vya ulinzi vya umma vinatumika kuitangaza dhima ya utawala bora kwa mitutu, bakora na mapanga.

Uzalendo pia ni neno linalopendwa kutumika kumshutumu au kumsifu raia yeyote, hasa wale wa upinzani. Watawala mara zote hupenda kuwahusisha wao kuwa hawana Uzalendo na nchi yao, eti kwa kuwa kosa lao wanaihoji serekali na kuionya pale inapokosea. Unachotakiwa kufanya ili uwe mzalendo ni kukaa kimya au kusifu serekali ovyo hata kama unajua au kuona maovu yanafanya hadharani au mafichoni, lakini ni wajibu wako kama mzalendo kuiweka nchi yako mbele, na uisitiri na kashfa au aibu za makusudi zinazofanya kwa niaba yako au nchi yako na serekali iliyopo.

Kukaa kimya na kuyafumbia maovu hayo huo sio uzalendo. Mzalendo ni lazima uwe tayari kufa, lakini serekali inayovunja sheria na kutoheshimu haki za wananchi wake au binaadamu huo ndio uhaini.
Pia sio lazima uipende nchi yako, iwe inafanya mema au mabaya matupu. Hiyo ni hiari yako na pia ni haki yako kama raia. Mfumo wa nchi za kikomunisti huko tunakotoka, uliaminisha na kulazimisha watu wake kuwa ni lazima uipende nchi ili uwe raia muaminifu na mwema. Katika nchi zenye kufuata demokrasia ya vitendo huna ulazima wowote wa kuipenda nchi yako, hata kama huna sababu yoyote ya msingi. Sasa kwa nini uwe mzalendo ikiwa utawala uliopo hauwatendei haki sehemu ya wananchi wake na unatawala kwa misingi ya kivyama, ubaguzi, vitisho na kila aina ya uonevu, ikiwemo mauwaji ya wanahabari, wanasiasa nk. Nani anadhani kutokuwa mzalendo ni kosa la jinai au dhambi katika mazingara kama haya.

Miaka 54 imepita tangu tujitawale na kujivunia mapinduzi. Kujivunia mapinduzi ndio, lakini kujitawala sio. Sisi ni watumwa na tunatawaliwa na Tanganyika, ndio maana amiri jeshi mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Tanganyika alikuwa mgeni rasmi katika shughuli yetu hii ya sherehe za mapinduzi. Amekuja kushuhudia koloni lake linavyopiga hatua katika kulinda maslahi ya taifa lake la Tanzania. Kama ilivyokuwa huko nyuma kabla uhuru, nchi nyingi za kiafrika mara kwa mara mkoloni awe Muingereza, Mfaransa, Mreno au Mjerumani, katika dhifa tofauti, ilikuwa ni wajibu au lazima kumuarifu na kumualika mkuu wa himaya ili aje ahudhurie sherehe na kutoa baraka zake. Makoloni yalikuwa yakiwakilishwa na kuongozwa na Magavana wa sehemu hizo, ambao wote ni wananchi wa asili wa nchi husika.

Miaka 54 tangu mapinduzi bado tunaendeleza mfumo ule ule, tulicho jaaliwa kubadili ni rangi ya “MKOLONI”. Tumewaondoa wale walio kuwa na rangi tofauti na yetu TU, na kumkumbatia “John Okello” au mtu mweusi, kwa kuwa tumefanana rangi basi salama itapatikana. Hapana sisi bado tunahitaji darasa zima la kujifunza. Miaka 54 haijatutosha na wala haijatusomesha kitu, ni aibu ya kiwango cha juu kusherehekea mauti kila mwaka. Sumu ya kuchukiana baina yetu ndio imekuwa kichocheo kikubwa cha msiba huu. Bado tuna watu wetu kwa makundi wanao ona ni kheri kutawaliwa na mnyamwezi kuliko Mzanzibari. Hata kama mzanzibari huyo ni baba yake mzazi, ami yake, mkewe, mumewe, mwanawe, damu yake, haloo lake au jirani yake tu basi hayo yote hayamtoshi/hayamridhishi, kwa sababu ana chuki ya dhati, HUU MSIBA MKUBWA HAPA KWETU.

Tunaweza kujinasua na dhiki hizi ikiwa tutakuwa wamoja. Visiwa vyetu vina umasikini wa ajabu, mimi nina umri wa kutosha kukumbuka kuwa sio zamani sana Zanzibar ilikuwa aibu kumuomba mtu senti, leo hatukopeshani tena, kwa sababu utakipata wapi cha kulipa. Sasa ni kugaiana na kuombana tu majiani, ili tupate riziki ya kutia tumboni au dawa ya kujinusuru na maradhi yaliyojaa kama taka hapa kwetu. Hii nayo ni faida kubwa ya kutawaliwa, sio Mapinduzi…………. Kwa sababu MAPINDUZI sio msiba wetu tena, bali MUUNGANO ndio adui yetu na ndie anae tumaliza kila kukicha.

Zanzibar ni moja tu. (one Zanzibar)

Share: