Habari

VAT ya umeme Zanzibar yamliza waziri wa zamani

Waziri wa fedha wa serikali ya awamu ya nne, Saada Mkuya amemwaga machozi bungeni baada ya serikali kusema ufumbuzi wa tatizo la Zanzibar kutozwa VAT ya umeme mara mbili halitapata ufumbuzi kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2018.

By Sharon Sauwa – Mwananchi
Saturday, June 30, 2018

Waziri fedha wa serikali ya awamu ya nne, Saada Mkuya amemwaga machozi ndani ya ukumbi wa bunge baada ya serikali kusema ufumbuzi wa tatizo la Zanzibar kutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya umeme mara mbili halitapata ufumbuzi kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2018.

Saada ambaye ni mbunge wa Welezo (CCM), alimwaga machozi wakati wabunge walipokaa kama kamati ya bunge zima kupitia vifungu vya Muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2018.

Saada ni mbunge wa tatu kumwaga machozi katika bunge la bajeti mwaka wa fedha 2018/19 lililoanza Aprili 3 na kumalizika jana Ijumaa, Aprili 29.

Wengine ni Jacqueline Ngonyani (Viti Maalumu – CCM) ambaye alimwaga machozi akitaka fedha za mawakala wa pembejeo zinazotolewa na serikali zilipwe. Na Katani Ahmed (Tandahimba – CUF) alilia akitaka fedha za mauzo ya nje ya korosho zisipelekwe kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

Juzi usiku, baadhi ya wabunge akiwamo Saada walilalamika kuwa VAT imefanya kuwapo kwa ongezo kubwa la bei ya umeme kwa Wazanzibari.

Akijibu hoja za wabunge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Adelardus Kilangi alisema ili kuondoa VAT kwenye umeme unaopelekwa Zanzibar, ilitakiwa mabadiliko hayo kuwasilishwa kwenye marekebisho ya sheria mbalimbali na si Sheria ya Fedha.

“Mimi kama mwanasheria mkuu wa serikali nashauri mabadiliko haya yaje katika mabadiliko ya sheria mbalimbali,” alisema Kilangi.

Hata hivyo, baada ya bunge kukaa kama kamati, Kamati ya Bunge ya Bajeti inayoongozwa na Hawa Ghasia iliibuka na hoja hiyo ikiwa ni sehemu ya mapendekezo yake ilitaka kufutwa VAT katika umeme unaopelekwa Zanzibar.

Akichangia hoja hiyo, mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, alisema Sheria ya VAT inatoa msamaha wa kodi kwa bidhaa inayoenda upande wa pili (Zanzibar) lakini kwa sharia ilivyokaa sasa hivi haitoi mwanya huo.

“Sheria ya VAT si ya Muungano hapo ndipo tatizo linapoanza na jambo hili ni la muda mrefu sana. Kwa hiyo unapopata opportunity (fursa) ya kulinyoosha kama sasa unalinyoosha. Ndio maana mimi naliona katika sura hiyo kuhakikisha kuwa haizalishi kero nyingine ya Muungano,” alisema Chenge.

Baada ya Chenge kusema hayo, Saada alisema anaunga mkono pendekezo hilo la kamati kwa kuwa ni la siku nyingi na kwamba kila mwezi Shirika la Umeme la Tanzania (Tanesco) limekuwa likiliuzia Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) kwa kujumlisha VAT.

“Namuomba sana Waziri wa Fedha walitazame katika muktadha huo. Hili jambo linatozwa kinyume na taratibu mheshimiwa Spika hili si jambo la mabadiliko ya sheria mbalimbali ni la Sheria ya Fedha,” alisema Saada.

Hata hivyo, Kilangi alisema itakuwa si sahihi kwa kupitia sheria hiyo kwa sababu linataka majadiliano na wadau wengine ili kupatikana kwa muafaka.

“Waziri wa Nishati alisema hatua zilishaanza na sisi tutalichukua kwa speed (haraka), inayotakiwa lakini tukiliibua hapa huko mbele litaleta matatizo mengine huo ndio ushauri wangu,” alisema.

Mbunge wa Ubungo (CUF), Saed Kubenea alisema kuitoza VAT Zanzibar si sahihi na kwamba hiyo ni kero ya Muungano na ndio sababu wabunge wa Zanzibar wameongea kwa hisia kubwa.

“Sasa umeme huo unaopelekwa Zanzibar, ZECO inalazimika kuuza kwa kampuni, hoteli za kitalii kwa bei ya juu tofauti na Tanzania Bara. Kwanza mfumo ule wa umeme wa Zanzibar ni wa Muungano kwa hiyo ni jambo linaloshirikisha nchi mbili,” alisema Kubenea.

Alisema hoteli za Zanzibar hazitumii umeme wa Tanesco kwa kiasi kikubwa bali wanalazimika kutumia jenereta.

Aliongeza, “Umeme ni tofauti na bidhaa nyingine ambazo hazitozwi VAT upande wa Tanzania Bara, bali zinaenda kutozwa kule na ndio maana tunasema umeme unaopelekwa Zanzibar usitozwe VAT.”

Hali hiyo ilimfanya Spika wa Bunge, Job Ndugai kusema, “Sijui ni kwa sababu tulitawaliwa na Waingereza? Tunapenda sana vimajadiliano majadiliano. Unanunua umeme kutoka Uganda hulipi VAT Uganda, ndugu yako wa Zanzibar tuzungumzezungumze.”

Si imeandikwa wapende wengine kama unavyojipenda mwenyewe? Kwa kweli linanipa tabu, yako mambo Zanzibar wanalalamika, we have been very unfair (kwa kweli hatutendi haki) yaani wenzetu wanalipa VAT asilimia 36 ndio maana hoteli ni ghali sana.”

“Sisi tuna ofisi zetu kule Zanzibar hatujawahi kupeleka kamati zetu kule maana ukiwapeleka hivi…kiposho cha hapa kinayeyuka. Maisha ghali sana Zanzibar. Huenda na haya mambo yanachangia,” alisema Spika ndugai.

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe alisema bei ya umeme kwa kilowati moja imepanda kutoka zaidi ya Sh8,000 hadi kufikia Sh16,000 na bado wanaongezewa VAT.

Hata hivyo, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema suala hilo halina mgogoro lakini shida iko kwenye tafsiri ya kisheria na kushauri serikali ilifanyie kazi jambo hilo katika utaratibu wa kawaida.

Baada ya mjadala huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Jitu Son alipendekeza wabunge wapige kura kuamua jambo hilo lakini Dk Kilangi alipinga akisema tatizo hilo linatokana na mabadiliko ya sheria ya VAT ambayo yalifikishwa bungeni na wabunge wa pande zote mbili za nchi walikuwapo.

Alisema sheria inasema umeme ukitoka nje ya Tanzania unatozwa VAT na kwamba kuna changamoto ya Zanzibar iko wapi. “Lakini VAT sio suala la muungano,” alisema AG.

Baada ya kauli hiyo, Spika Ndugai alisimama na kusema, “Duniani hapa tutakufa siku moja, hata kama tuko serikalini tuko wapi? Jambo ambalo si la haki sisi tunaosali Jumapili.”

“Kweli Kongwa mnalipa hivi mbunge mwenzangu akalipe hivi? Tanzania hii! Au Zanzibar ni matajiri sana. Ninaomba Mwenyekiti (Ghasia) tuwaachie wao (serikali) wakajadiliane. Liko wazi kabisa lakini tuwaache wakajadiliane,” alisema Ndugai.

Kauli hiyo ilisababisha kelele bungeni, wabunge wakitaka kutoa taarifa wengine wakisema si haki, hali iliyomfanya Ndugai kumpa nafasi mbunge wa viti maalumu, Bahati Ally Abeid ambaye alisema kuwa mjadala huo ulipofikia si mahali ambapo wabunge wataweza kupiga kura na kutaka serikali iwaachie umeme bila VAT.

“Wanafanya hivi wakijua ZECO wanaoitoza VAT, kule inaenda kuhudumia hadi Idara za Muungano kwa nini mnatunyanyasa tena? Tuachieni serikali imefika wakati sasa mtuachie,” alisema Bahati.

Lakin, Ndugai aliamua kuliruka na kuendelea na vifungu vingine vya sheria na baadaye kurudi tena katika kifungu hicho.

Hali hiyo ilimfanya Mhagama kuiomba serikali kupewa nafasi ya kukutana na upande mwingine wa Muungano na kuahidi kwamba katika mkutano ujao wa bunge watakuwa wamemaliza suala hilo ili kuondoa wingu la kuonekana kama Zanzibar inaonewa.

Baada ya Waziri Mhagama kuyasema hayo, Spika Ndugai alisema, “Waje kujadiliana nanyi nini? Mnataka toeni kama hamtaki liacheni.

Maana mimi kama jirani yako nakwambia unaniumiza unataka tujadiliane tujadiliane nini? Hili ni jambo la kukaa wenyewe na kuliona.

Mnakaa mnajadiliana mnawaambia kwamba sisi tumekataa ili? Vipo vitu vya kujadiliana lakini sio hili nakwambia mwenzio umenibana unasogea, sasa mnajadili nini?” alihoji na kisha kuwahoji wabunge kama pendekezo la kuwapa muda serikali linaafikiwa…Liliafikiwa.

Baada ya kupitishwa kwa sheria hiyo, Saada alionekana kuvua miwani yake na kufuta machozi huku wabunge walioketi karibu naye, Magreth Sitta (Urambo CCM) na Shukuru Kawambwa (Bagamoyo CCM) wakimbembeza.

Akizungumza katika viwanja vya bunge, Saada alisema kilichomuumiza ni serikali kutotatua tatizo hilo licha ya yeye kulizungumzia tangu mwaka 2014 ilipoanzishwa kodi hiyo.

Alisema Rais John Magufuli amelisikia tatizo hilo na kwamba Wazanzibari wana matumaini makubwa naye kwa sababu ni Rais wa wanyonge.

Share: