Habari

vijana CCM waibana ZEC ugawaji majimbo

Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka

CHANZO: Mtanzania

IMECHAPISHWA: Ijumaa, Mei 8, 2015

JUMUIYA ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), imeitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuacha kuendeshwa na wanasiasa na badala yake itangaze mipaka ya majimbo ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria.

Imesema kitendo cha kushindwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria na utaratibu unaotaka mipaka ya majimbo itangazwe kila baada ya miaka 10.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar jana, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka alisema ZEC imepewa jukumu hiyo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 katika kifungu cha 120(1)(3)(5) ambayo inaipa uwezo tume hiyo ya uchaguzi.

Alisema hatua ya ZEC kukaa kimya na kushindwa kutangaza mipaka mipya ya majimbo inatokana na woga na vitisho vya siasa kutoka kwa vyama vya upinzani.

“Tunapata shaka huenda wamekubaliana au kupata vitisho vya wanasiasa wasiotaka majimbo ya uchaguzi kupitiwa upya, ila ZEC inachotakiwa ni kutimiza wajibu wake wa sheria na si kuzubaishwa na miluzi ya wanasiasa mapepe,” alisema Shaka.

Alisema taarifa za ndani zinaeleza kuwa kazi ya kukagua mipaka ya majimbo iliyokuwa ikifanywa na ZEC imekamilika siku nyingi jambo ambalo UVCCM inajiuliza kwa nini viongozi wake wamekaa kimya hadi sasa.

“Hatua ya kuweka mipaka ya majimbo siyo ya kwanza kufanywa na Tume ya Uchaguzi…ilifanyika hivyo mwaka 2005 lakini mwaka huu tunaona kuna mchezo wa kuigiza unataka kufanywa.”

“Sisi UVCCM tuko macho tutafuatilia kila hatua…tunaiambia ZEC suala la kukagua mipaka ya majimbo si jambo la wanasiasa ni utekelezaji wa katiba kwa maslahi ya wananchi,” alisema Shaka na kuongeza:

“Ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 iliweka wazi kuwa hakuna uwiano wa watu wanaoishi katika majimbo 50 ya Unguja na Pemba na kwa sababu hiyo ZEC haiwezi kukwepa kazi ya kupitia upya majimbo ya uchaguzi.”

Pia, Shaka aliponda hatua ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad kutaka kuwania kwa mara ya tano urais wa Zanzibar, kwa kutumia vitisho.

“Maalim Seif ameanza kutoa vitisho kwamba safari hii hatakubali kunyang’anywa urais wa Zanzibar kama ilivyozoeleka katika uchaguzi uliopita.”

“Anajua wazi kauli zake hizi zinakwenda kinyume na miko ya demokrasia huru na zinaweza kusababisha ghasia tena hapa kwetu Zanzibar,” alisema Shaka.

Share: