Habari

VIJANA TUKIZEEKA TUZEEKE KAMA MAALIM SEIF.

Na: Suphian Juma

.Historia fupi ya Maalim Seif

.Nini cha Kujifunza kwake

.Musiba, kibaraka wa dola anayetumika kama gari taka dhidi ya Maalim Seif, Zitto

Kama ilivyo matamanio ya binadamu yeyote katika matarajio ya kuishi na kuacha alama duniani, basi huwa si vibaya pia kwa umri wa ukijana kuziishi ndoto za waliotutangulia kwa kuiga nyendo zao hususani zile zilizotukuka.

Binafsi nilipokuwa shule ya msingi, miongoni mwa maswali magumu darasani ni pale mwalimu alipotuuliza “What are you going to be”, maana nilijikuta na machaguo mengi na makubwa mno huku nisijue namna na uwezekano wa kuyafikia ukizingatia kwetu ‘kwa upande wa baba yangu’ Singida nilipozaliwa hakuna hata mmoja aliyewahi kuwa hata Mwenyekiti wa Kijiji, japo nilijifariji inawezekana hasa pale nilipouwaza busara na ukomavu wa baba yangu katika kuiongoza familia yetu na pili pale nilipoukumbuka uzao wa mama yangu ulipo mkoani Tanga, maana huko angalau mmoja alikuwa Waziri tena tukimwandika hadi darasani (jina nalihifadhi).

Japo hadi hapa nilipo sijatimiza yoyote kati ya hayo ‘machaguo ya kuwa nani’ ila huwa napata tabasamu la furaha pale ninapobaini machaguo yangu yote yalilenga kuwa sauti wakilishi ya maslahi ya watu, na sasa ninachokifanya ni palizi tu kuelekea kwenye hayo machaguo yaliyotukuka.

Swali ni je, ni rahisi kufika kwenye machaguo hayo? Jibu ni “Si rahisi” ila inawezekana, kwanini? Kwasababu tunao maandiko, simulizi na hata ushuhuda kutoka kwa watu waliofanikiwa kufika huko au kukaribia kufika huko licha ya changamoto za hadi hata kukaribia watesi wao kuunyofoa uhai wao, na hapa mmojawapo ni Seif Sharif Hamad almaarufu Maalimu Seif.

Kwa wasiojua kwa ufupi tu, Maalim Seif alishawahi kuwa MwanaCCM, pamoja na vyeo vingine aliwahi kuwa Mjumbe Barza la Mapinduzi Zanzibar na Waziri wa Elimu wa visiwa hivyo kati ya mwaka 1977-1980, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi la kati ya mwaka 1980-1989, na kuwa Mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango wa CCM. Pia alikuwa kuwa Waziri kiongozi wa Zanzibar kuanzia Februari 6, 1984 hadi Januari 22, 1988 ambapo ndipo 1988 alifukuzwa ndani ya CCM akiwa na wenzake, Shaban Mloo,Ali Haji Pandu,Khatib Hasan, Soud Yusuf Mgeni, Hamad Rashid na Ali Salim baada ya kukorofishana na baadhi ya maafisa wa CCM.

Ila cha ajabu Maalim Seif hakukoma kuipenda siasa akitumaini ndiyo njia ya kupambania haki za watu, hivyo 1992 akawa miongoni mwa waanzilishi wa chama cha CUF kutoka kwenye vuguvugu la KAMAHURU (Kamati ya Mwelekeo wa Vyama Huru), ambapo CUF kwa umahiri wake wa kuongoza vema, amefanikiwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho takribani miaka 26 sasa.

Sote tunajua pamoja na ukatili mwingi uliofanywa na Serikali ya CCM visiwani Zanzibar katika chaguzi mbalimbali ila hakika kwa werevu, ujasiri na busara zake Maalim Seif kama Katibu Mkuu tangu 1992 aliweza kukipa heshima iliyotukuka Chama cha CUF na hatimaye kuongoza majimbo karibia yote kwa kila chaguzi zilizofanyika huko visiwani Zanzibar.

Aidha kwa sababu ya uongozi mujarabu wa Maalim Seif, wanaZanzibar kwa zaidi ya awamu mbili, wamempa kura za kutosha za kuwa Rais wa Zanzibar, mwanasiasa huyu ngangari asiyekubali Kutishwa na dola, kura ambazo kutokana na yeye mwenyewe Maalim Seif na hata taarifa za ndani na nje ya visiwa hivyo zilionesha yeye kushinda uRais mara kadhaa ila alihujumiwa bila soni wala haya na Serikali ya CCM.

Kikawaida kwa mfano kwa mwaka 2015 alipohujumiwa uRais na hatimaye uchaguzi kurudiwa, wengi tulidhani huyu Mwanasiasa Mzee-Kijana angekoma siasa ila kwakuwa anajua yeye ni sauti ya wengi hakuwakatisha ndoto waZanzibar, na hivyo kuendelea kudai haki mbalimbali za wanzanzibar licha ya misuguano (ambayo kwa asilimia kubwa inachagizwa na dola) na Mwenyekiti wake wa chama, Prof Ibrahim Lipumba (aliyeukacha uenyekiti mwaka 2015) mpaka March mwaka huu (2019) ambapo Mahakama ilimrejeshea uenyekiti Lipumba na ndipo Maalim kuamua kuachana na CUF na kuishangaza dunia baada ya kuungana na chama kichanga ila ‘pasua kichwa’ kwa Serikali nunda ya CCM, ACT WAZALENDO.

Kuonesha Maalim Seif ni gwiji haswa la siasa na kipenzi cha watu, alipotangaza tu kuhamia ACT WAZALENDO, dola ambayo imekuwa mstari wa mbele kumkingia kifua Prof Lipumba iliduwaa kuona maelfu kwa maelfu ya wanachama wa CUF Tanzania Bara na Visiwani wakitangaza kuungana na Maalim Seif kujiunga na ACT WAZALENDO bila shuruti, huku msemo wa “Ulipo Tupo” ukishika kasi, huku mamia ya matawi ya CUF yakigeuzwa kuwa ya ACT WAZALENDO.

Dola haikuridhika, kwakuwa ilijua imemkomesha kupitia kibaraka wake Lipumba kumfuta uanachama, ikaamua kuanza kuhangaika na kukifuta ACT kupitia Msajili wa vyama kwa sababu hovyo za kuwa waliohamia ACT WAZALENDO walichoma bendera za CUF na kutumia maneno yenye ‘udini’, hoja amabazo kimsingi ni za ‘kitoto’, na kulazimika kwa haraka, kwa ukomavu wa ACT WAZALENDO, chini ya Kiongozi ‘jemedari’ wa Chama Zitto Kabwe hoja zote hizi mufu zilipanguliwa kisomi na kuiacha dola isijue cha kufanya. AIBU!

Serikali ya CCM, ambayo kwa sasa imezidi kuonekana kukosa pumzi kutokana na mshikamano na nguvu mpya ya Maalim Seif na wafuasi wake na uongozi mahiri wa Zitto Kabwe, imeendelea bila aibu kujaribu kukwamisha mikutano halali ya chama, mfano mwezi jana nilipata fursa ya kujumuika na Viongozi wa Chama akiwemo Zitto Kabwe na mwanachama namba moja Maalim Seif katika kuzindua matawi mapya mkoani Tanga ila cha ajabu mwenye ukumbi wa Hindu Mandal amabapo tungeenda kufanyia mkutano wa ndani alitishiwa na Polisi na kufunga ukumbi huo, na hapohapo RPC wa Tanga nae akaagiza tusifanye mikutano wala uzinduzi wowote eti kisa ‘entelijensia’ yao inaonesha wafuasi wa CUF wangekuja kutuvamia, yaani sababu za kilozi kabisa ambazo haziooni na Tanzania ya kidemokrasia inayofuata utawala wa kisheria.

Kwakuwa mimi Suphian nimekuwa mstari wa mbele kuikosoa Serikali na kuishauri kwa maslahi ya watanzania, na kwakuwa nimekuwa nasapoti harakati lulu anazozifanya kaka Zitto Kabwe, Maalim Seif, ACT WAZALENDO na Upinzani kwa ujumla, kibaraka wa Serikali aitwaye Cyprian Musiba kupitia kipeperushi chake cha TANZANITE aliamua kunichafua kwa kudai nafanya ufuska na nashiriki tendo la ndoa na viongozi hawa, yote hii ni kuhakikisha viongozi hawa na mimi pia kwa pamoja turudi nyuma kimisimamo…wasijue WATANZANIA WA LEO SIO WAJINGA, sio mazwazwa, na niwapongeze na kuwashukuru watanzania kwa KUMPUUZA huyu kibaraka wa dola ambaye anatumika kama gari la kubebea takataka.

Nilishaamua kuingia kwenye siasa, sijabipu, najua gharama zake, sibabaishwi na habari takataka, nitaendelea kusimama imara kama nilivyoelezea kwa ufupi Safari ya Maalim Seif licha miiba iliyomchoma njiani. Propaganda za Musiba ni upuuzi kama upuuzi mwingine, tunakijua kigenge chake kinachomtuma na kumfadhili, kigenge hicho nakiahidi kitaendelea kupata sonona maana ndio kwanza moto tumeuwasha unless wajisahihishe kwa maslahi ya Watanzania. Maana hatujaiweka Serikali itende kwa ajili ya Serikali, bali Serikali itende kwa ajili ya Wananchi wenye nchi.

Musiba anayejiita mwanaharakati huru, ambaye ameendelea kuchafua watu wengi kwa kichaka cha kumtetea Rais, ni vema Rais/Taasisi ijitafakari upya, imchukulie hatua otherwise tunahitimisha Taasisi hiyo ‘inayopaswa’ kuwa iliyotukuka, itakuwa ina ubia na kiumbe huyu ambaye anadhani watu kukaa kimya labda wajinga au wamemwogopa, kumbe tunamwona ‘kituko’ fulani linachohangaika kucheua viroja vinavyofaa kupelekwa jalalani.

Mwisho, niwaombe vijana tujitafakari je hadi sasa tumeipigania nchi yetu inayozidi kuchafuliwa kimataifa na matendo ya Serikali hii kwa kiasi gani? Je tuna misuli ambayo anayo Maalim Seif? Au hatutaki kuzeeka tukiwa lulu kwa Watanzania kama yeye? Au furaha yetu ni kuzeeka tukiweka alama za UNAFIKI, UMIMI na UWOGA mbele ya dola dhalimu? Tukumbukwe kwa kuwa kizazi cha kizwazwa ambacho hakikuthubutu kupanua mdomo kukemea matendo mabaya ya Serikali tulizoziweka zituongoze tupendavyo? Haiwekani Haki za Binadamu, misingi ya Utawala Bora na Demokrasia, Utu, Umoja wa kitaifa, Ajira, Uwekezaji, Uchumi, Amani, Uhuru wa Kujieleza na Uhuru wa Vyombo vya Habari visiginwe tangu 2015 ila kijana upo tu, unadai eti ni mapito tu au unatetea kwamba nchi ipo sawa kisa upo kwenye ‘system’, huu ni UZWAZWA usiokubalika. VIJANA TUAMKE, TUSEME HAPANA!

VIJANA TUULIZANE, TUNATAKA TUZEEKE KAMA NANI?

Mwandishi, Mwanasiasa, Mwanaharakati.

Suphian Juma May 11, 2019.

Share: