Habari

Vikosi SMZ vyaonya

Vikosi SMZ vyaonya
November 1, 2018

NA MARYAM HASSAN

IDARA Maalum ya Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema hakuna uandikishwaji wa vijana kwa ajili ya ajira kwenye vikosi hivyo.

Akitoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari kwa niaba ya makamishna na wakuu wa vikosi hivyo, Kamisha wa Zimamoto na Uokozi Zanzibar, Ali Abdallah Malimusi, hakuna ajira zinazoandikishwa na kuwataka wananchi kutoyumbishwa na upotoshwaji huo.

Kamishna huyo alisema taarifa zilizonea sehemu mbalimbali kwamba vikosi vya SMZ vinaandikishwa vijana kwa ajili ya ajira, hazina ukweli wowote.

Alisema taarifa hizo si za kweli na kwamba wenye kuzitoa na kuzisambaza kwa wananchi wanasababu ambazo wanazielewa wenyewe.

Kamishna Malimusi alifahamisha kuwa hivi sasa hakuna ajira yoyote katika Idara Maalum ya SMZ, na kuwataka wananchi kutoshughulishwa na taarifa hizo za upotoshwaji.

Mkuu huyo wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi alisema wapo baadhi ya watu wamekua wakieleza uongo wa kuwepo ajira katika vikosi vya SMZ na baadae kuwatapeli wananchi kwa kuwatoza fedha, ili vijana wao waandikishwe kwenye ajira hizo.

“Kama wapo watu wenye kuwatoza wananchi fedha kwa ajili vijana wao wapate ajira katika vikosi vya SMZ, hilo ni kosa la jinai na atakaepatikana akitoa na kupokea fedha hizo watachukuliwa hatua za kisheria”, alisema Kamishna Malimusi.

Kamishana huyo alieleza kuwa hivi sasa katika kambi ya JKU Saateni zoezi linalofanyika ni la kawaida ambalo hufanyika kila mwaka la kuandikisha vijana wa kujitolea kwa mujibu wa sheria.

Alieleza kuwa uandikishaji wa vijana hao ulianza katika ngazi ya wilaya na kwenda Mkoa na hivi sasa katika kambi ya JKU ambao vijana hao watajitolea kwa mujibu wa sheria.

“Niwaombe wananchi kupuuza taarifa hizo na hakuna uandikishwaji wa vijana kwa ajili ya ajira na wala wasikubali kutoa fedha kwa lengo la kuwania ajira hizo”, alisema Kamishna huyo.

Zanzibarleo

Share: