Habari

Vikosi vya ulinzi vyahitaji mafunzo- Maalim Seif

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema vikosi vya ulinzi vya Tanzania na vile vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vinahitaji kupatiwa mafunzo ya ziada juu ya kukabiliana na vitendo vya vurugu na kulinda amani ya nchi.

Amesema vikosi hivyo vimekuwa vikitumia nguvu za ziada katika kukabiliana na vitendo hivyo, hali inayopelekea kuleta madhara kwa raia wasiokuwa na hatia pamoja na mali zao.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo ofisini kwake Migombani Mjini Zanzibar alipokuwa na mazungumzo na ujumbe wa Umoja wa Mataifa uliofika kwa ajili ya kubadilishana mawazo.

Ameeleza kuwa mara nyingi vikosi vya ulinzi vya Tanzania vimekuwa vikifanya kazi kwa kufuata matakwa ya wanasiasa na kusahau mwongozo na maadili ya kazi yao, huku vikosi vya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vikifanya kazi bila ya kuwa na taaluma ya kutosha, na kwamba mafunzo hayo yatasaidia kuleta mabadiliko ya kiutendaji ndani ya vyombo hivyo vya ulinzi.

Kwa upande mwengine Makamu wa Kwanza wa Rais ameelezea haja ya kulifanyia mapitio daftari la kudumu la wapiga kura ili liweze kwenda na wakati.

Amesema ucheleweshaji wa kulifanyia mapitio daftari hilo unaweza kusababisha baadhi ya wananchi kukosa haki yao ya kupiga kura baada ya kutimiza masharti na sifa za kuwa wapiga kura.

“Daftari hili linatakiwa kufanyiwa mapitio kila mwezi wa Oktoba lakini hadi sasa halijapitiwa, na sidhani kuwa kuna mpango huo kwa sasa”, alikumbusha Maalim Seif.
Hata hivyo amesema huenda tatizo hilo limetokana na ukosefu wa fedha, na kusisistiza haja kwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar kufanya kazi kwa uwazi ili kujenga matumaini kwa wananchi.

“Ukweli ni kwamba tunahitaji kuwa na chaguzi huru na za haki katika nchi yetu, na hali halitowezekana kama Tume ya Uchaguzi haitofanya kazi kwa uwazi ‘transparent’”, alitanabahisha.

Akizungumzia kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Maalim Seif amesema inafanya kazi vizuri licha ya changamoto ndogo ndogo ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa baadhi ya watendaji hasa katika ngazi ya Shehia.

“Huku juu tunashkuru kwamba tunakwenda vizuri, lakini mgawanyo wa madaraka uko katika ngazi ya Mawaziri tu. Kinachojitokeza ni kuwa bado baadhi ya watendaji wa ngazi za chini hawajataka kubadilika hasa masheha” alifahamisha na kuongeza,

“Mfumo huu wa serikali ya umoja wa kitaifa ndio unaotufaa kuliko mfumo wowote ule kwa Zanzibar kwa sababu umewaunganisha Wazanzibari na ndio walioamua kuwa na mfumo huo”, aliongeza.

Akijibu hoja za wajumbe hao waliotaka kujua juu ya nafasi ya mwanamke wa Zanzibar kuhusu siasa, Makamu wa Kwanza wa Rais amesema Serikali inafanya juhudi za kuwashajiisha wanawake kugombea nafasi za uongozi badala ya kusubiri nafasi za uteuzi pekee.

Kwa upande wake kiongozi wa ujumbe huo Bw. Akinyemi Adegbola ambaye ni msaidizi wa masuala ya uchaguzi wa Umoja wa Mataifa kutoka makao makuu New York, amesema Umoja huo utaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbali mbali zinazojitokeza kwa nchi wanachama zikiwemo zile zinazohusiana na masuala ya uchaguzi.

Tagsslider
Share: