Habari

“Viongozi muwe waadilifu”

Posted on  

Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Zakiem, Jimbo la Temeke.

Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Zakiem, Jimbo la Temeke.

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema viongozi wa serikali wanapaswa kufanya kazi kwa uadilifu bila ya kuwabagua wananchi kwa misingi yoyote ikiwemo ya itikadi ya vyama vya siasa na udini. Amesema kiongozi akishachaguliwa kuongoza serikali katika ngazi yoyote, anakuwa kiongozi wa wananchi na anapaswa kuwatumikia wananchi wote kwa kuwapatia huduma na haki zao zinazostahiki.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameeleza hayo katika ziara yake ya siku moja ya kutembelea miradi ya maendeleo na shughuli za kichama katika Wilaya ya Temeke mjini Dar es Salaam.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya watendaji wa serikali za mitaa, juu ya kuwepo kwa ubaguzi katika utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi.

Miongoni mwa mitaa iliyolalamikiwa ni pamoja na mtaa wa Magogoni katika Jimbo la Kigamboni pamoja na kata ya Keko katika Jimbo la Temeke.

Hata hivyo Maalim Seif amewapongeza watendaji wa CUF wanaoshikilia serikali za mitaa mbali mbali ya Dar es Salaam kwa kutoa huduma muhimu bila ya malipo kwa wananchi wote, na kuvitaka vyama vyengine kuiga mfano huo.

Amesema kufanya hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa sera za CUF ambazo zinalenga kusogeza karibu huduma muhimu za kijamii na kuzitoa bila ya malipo kwa wananchi, na hatimaye  kutimiza azma yake kutoa haki sawa kwa wananchi wote.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara Julius Mtatiro akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Zakiem, Jimbo la Temeke.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara Julius Mtatiro akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Zakiem, Jimbo la Temeke.

Katika ziara hiyo Maalim Seif ameahidi kumaliza ujenzi wa visima vinne vya maji katika kata ya Tungi Kigamboni, ili viweze kutoa huduma kwa wananchi wa eneo hilo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Zakiem Temeke, Maalim Seif ameviomba vyombo vya dola kuimarisha ulinzi Bara na Zanzibar ili kuzuia vitendo vya kihalifu vinavyoonekana kujitokeza kwa kasi katika siku za hivi karibuni.

Amesema vitendo hivyo ni vya kusikitisha na wala haviendani na utamaduni wa Watanzania, na kuiomba serikali ya Muungano kuangalia uwezekano wa kuitisha mjadala wa kitaifa ili kutathmini chanzo cha maovu hayo.

Amefahamisha kuwa suala la ulinzi na usalama wa raia na mali zao ni jukumu la serikali ya Muungano, lakini iwapo litatolewa katika orodha ya mambo ya Muungano Zanzibar itaweza kujilinda na kuzuia uhalifu.

“Namuomba ndugu yangu Rais Jakaya Kikwete asiyachukulie matukio haya kwa wepesi, ni vyema awaongoze Watanzania kupata majibu ya masuala mazito kama hayo”, alifahamisha Maalim Seif na kuongeza,

“Nashangaa wakati haya yakitokea hakuna kiongozi yoyote wa serikali aliyewajibika, na badala yake wanakuja Zanzibar wanatoa kauli zisizokuwa na msingi eti ni ugaidi”, alisisitiza.

Ameelezea haja ya matokeo ya uchunguzi wa mauwaji ya Padri Evarist Mushi yaliyotokea Zanzibar yawekwe bayana, ili mataifa na wananchi waweze kujiridhisha juu ya yale yaliyotokea.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Temeke, Rehema Kawambwa, amewataka wanawake wa Wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi ndani ya chama hicho katika uchaguzi unaotarajiwa kuanza mwezi ujao.

Stori na Hassan Hamad. Picha na Salmin Said, OMKR Zanzibar

Share: