Habari

Viongozi wa majimbo watakiwa kutatua shida za wananchi

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akihutubia viongozi wa chama hicho wa Wilaya ya Wete Pemba katika mkutano wa kuhitimisha ziara yake ya Mikoa ya Pemba Kusini na Kaskazini.

Wete, Pemba
Jumapili, Februari 24, 2019

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amewataka viongozi wa chama hicho wa Majimbo ya Pemba kwenda kwa wananchi waliowapigia kura kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Dk Shein amesema hayo leo Jumapili, Februari 24, 2019 kwenye ukumbi wa Baraza la Wawakishi Wete, wakati akizungumza na viongozi wa CCM katika mkutano wa kufanya majumuisho ya ziara yake wilayani humo.

Amesema viongozi wa majimbo wakiwamo wawakilishi na wabunge wa viti maalum wa CCM kwenda kwa wananchi ili kujuwa changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi hatua ambayo itasaidia kukiimarisha CCM.

Amesema kuwa CCM haitamvumilia kiongozi mtoro wa jimbo ambaye amechaguliwa na wananchi na baadaye haonekani jimboni kuwasaidia wananchi waliyompigia kura. Amewataka kuacha kukaa maofisini.

Amesema viongozi wa majimbo wataendelea kuwa karibu na wananchi pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi hali hiyo itapelekea kuiunga mkono CCM na kuendelea kushinda katika uchaguzi mkuu ujao wa 2020.

Aidha, Dk Shein amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na CCM itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwapelekea maendeleo endelevu wananchi wote wa Unguja na Pemba bila ya ubaguzi.

Amesema kuwa CCM itahakikisha wananchi wote wanapata huduma sawa bila upendeleo, siyo kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni ambapo huduma hizo zilikuwa zikitolewa kwa upendeleo hususan elimu na afya.

Amesema kuwafuata wananchi na kutatua shida zao ni agizo la CCM ambalo lilitolewa katika Mkutano Mkuu wa chama hicho uliyofanyika Dodoma kama njia muhimu katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.

Dk Shein alieleza kuvutiwa na taarifa ya Chama na Serikali ya wilaya hiyo na kutoa pongezi zake na kusifu ushirikiano uliopo kati ya pande mbili hizo hatua ambayo imepelekea mafanikio makubwa.

Pia, amesema jukukumu jingine muhimu kwa viongozi wa majimbo ni kuwaeleza wananchi mafanikio na mipango ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dk Shein amesema kwenye siasa za vyama vingi hakuna kutishana na wala kutukanana na kuwataka viongozi wote wa CCM wa Mkoa wa Kaskazini Pemba kufanya kazi za kukiimarisha chama chao bila hofu.

Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar aliupongeza uongozi wa Serikali wa Wilaya ya Wete kwa kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kufikia lengo kwa kukusanya mapato yake vizuri.

Share: