Habari

Viongozi wa Z’bar wagundulika kuvamia ardhi’

Zanzibar. Kamati ya Kudumu ya Mawasiliano na Ujenzi imegundua kuwapo kwa baadhi ya viongozi ambao hawahusiki na masuala ya ardhi, lakini wamekuwa wakiyatumia mamlaka waliyonayo kusababisha migogoro ya ardhi Zanzibar.

Hayo yalielezwa na Mwakilishi wa Kitope, Makame Mshimba Mbarouk wakati akitoa taarifa ya muhtasari wa kamati hiyo katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Zanzibar. Mshimba alisema kuna baadhi ya viongozi hutumia mamlaka yao kwa kutaka kuuziwa maeneo ambayo tayari yana umiliki wa wananchi au tayari yameshauzwa kwa taasisi nyingine.

Alisema kamati imetoa ushauri kuwa si jambo la busara kwa viongozi wenye kuheshimika kufanya kitendo kama hicho.

Alisema kamati yake inashauri idara husika katika upimaji au uzaji wa ardhi zisiwe na muhali kwa kumwangalia mtu kwa cheo chake na badala yake haki itendeke kwa uamuzi utakaokuwa hauna athari kwa mtu yeyote.

Mshimba alisema masuala ya ardhi yamekuwa na malalamiko mengi hapa nchini na kusababisha kesi nyingi za ardhi kuwa katika mahakama ya ardhi.

Alisema ardhi ni miongoni mwa rasilimali muhimu sana matatizo mbalimbali hujitokeza kutokana na udogo wa nchi na matumizi kuwa ni mkubwa.

mwananchi

Share: