Habari

Vituo vya ujasiriamali vyaja kila wilaya Pemba

IMEANDIKWA NA MASANJA MABULA, PEMBA

WIZARA ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Pemba inakusudia kuweka kituo kila wilaya, ambacho kitatoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto za ajira.

Afisa Mdhamini wizara hiyo, Fatma Hamad Rajab ameyasema hayo wakati akitoa taarifa kwa wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM, Mkoa wa Kaskazini Pemba kwenye kikao cha majumuisho ya ziara ya kamati hiyo kuangalia utekelezaji wa ilani kwa wizara hiyo.

Fatma amesema vituo hivyo ambavyo vitasimamiwa na wizara kupitia mabaraza la vijana na vitakuwa ni msaada mkubwa katika kuwakomboa vijana.

Aidha amesema kuwa wizara itahakikisha vijana ambao wanahitaji kupatiwa elimu ya ujasiriamali wanaipata kwani wataandaliwa wataalamu wa masuala ya ujasiriamali na muda wote watakuwa kwenye vituo hivyo.

“Mkakati wa wizara ni kufungua vituo vya ujasiriamali kila wilaya za Pemba, lengo ni kuwakomboa vijana,”alisema.

“Tunatambua kwamba changamoto kubwa kwa vijana ni ukosefu wa ajira, hivyo kupitia vituo hivi, watapewa mbinu ya kukabiliana na maisha,”aliongeza.

Wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM, Mkoa wamesema ni vyema wizara hiyo kuimarisha elimu ya ujasiriamali kwa vijana.

Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake –UWT-Miza Khamis Haji ameshauri taaluma ya ushoni kuboreshwa ili kuwafanya vijana wa kike wanaoamliza skuli kujiunga.

“Vijana wengi wa kike wanaomaliza masomo ya kidato cha pili, wanakosa kazi za kufanya,hivyo iwapo kutakuwa na vituo vya kutoa elimu ya ushoni kutawasaidia”alisema.

Naye katibu wa CCM, Mkoa huo Khadija Abdi Nassor amewashauri vijana kutovunjika moyo kutokana na changamoto zinazowakabili.

Amesema kila hatua ya maendeleo, inakuwa na changamoto zake, hivyo wanapaswa kuendelea kupambana kwani CCM kipo pamoja nao.

“Tunatambua kwamba, kila unapopiga hatua ya maendeleo changamoto nazo zinazidi kutokea hivyo, nawaomba sana msivunjike moyo,”alishauri.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo Mberwa Hamad Mberwa amepongeza juhudi zinazochukuliwa na wizara hiyo katika kutekeleza ilani ya chama hicho.

“Mnafanya kazi nzuri ya kutekeleza ilani ya uchaguzi, CCM imefurahi na tunaomba kasi mliyoanza nayo muendelee nayo”alisema.

Kamati hiyo imetembelea vikundi mbali mbali ikiwemo ufugaji wa ngombe wa maziwa, vikundi vya ushonaji pamoja na vikundi vya sanaa.

PembaToday

Share: