Habari

Vuta nikuvute Zanzibar

NA MWINYI SADALLAH
14th November 2015

Vuta ni kuvute ya kushiriki au kutoshiriki uchaguzi wa marudio ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, kati ya vyama vya CCM na Cuf, imezidi kuwaweka wananchi wa kisiwa hicho njia panda.

Hali hiyo imeendelea kujitokeza baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), kutangaza rasmi katika Gazeti la Serikali kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, visiwani humo.
Uchunguzi wa Nipashe Mjini Zanzibar, umebaini kuwa wakati Chama cha Mapinduzi (CCM), kikikubali kushiriki uchaguzi wa marudio, Chama cha Wananchi (Cuf) kimegoma kushiriki uchaguzi huo.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Waride Bakar Jabu, alisema kuwa suala la CCM, kushiriki uchaguzi wa marudio halina mjadala baada ya uchaguzi wa awali kutawaliwa na vitendo vya udanganyifu kinyume na misingi ya demokrasia.

Alisema uamuzi wa kurudiwa uchaguzi ni muafaka kwa sababu uchaguzi wa Oktoba 25, ulitawaliwa na vitendo vya udanganyifu na kupoteza sifa ya kuwa uchaguzi huru na wa haki kabla ya matokeo kufutwa.
‘CCM tunaunga mkono uamuzi wa Zec wa kutangaza rasmi kurejewa kwa uchaguzi, hatua hii itasaidia kupatikana viongozi waliochaguliwa kweli kwa kufuata misingi ya demokrasia,’ alisema.

Alisema mbali na kuwashukuru wananchi waliojitokeza katika uchaguzi uliofutwa, CCM imeanza kujipanga upya kwa matayarisho ya uchaguzi wa marudio baada ya Tume kutangaza tarehe ya kufanyika uchaguzi huo.
Hata hivyo, alisema Zec inatakiwa itangaze mapema tarehe ya kurudiwa uchaguzi ili wananchi wapate kufahamu na kujiandaa na uchaguzi huo.

‘Tupo tayari kushiriki uchaguzi wa marejeo kwa sababu uchaguzi wa mwanzo ulipoteza sifa za kidemokrasia baada ya kutawaliwa na vitendo vya udanganyifu,’ alisema.

Alisema CCM kimsingi inakubaliana na hoja zilizotumiwa na Tume kufuta matokeo ya uchaguzi kwa sababu ni kweli kulikuwa na vitendo vya vurugu na udanganyifu wakati wa upigaji kura na kufanya majumuisho.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa Cuf, Omar Ali Shehe, alisema hawakubaliani na uamuzi wa Zec kurudia uchaguzi wakati wa awali haujakamilika na kutangazwa mshindi.

Alisema kwa mujibu wa ripoti za waangalizi wa ndani na nje uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu, ulikuwa huru na wa haki na Mwenyekiti wa Zec hakuwa na sababu za msingi za kufuta matokeo ya uchaguzi huo.
Alisema jambo la msingi ni mwenyekiti kurudi kazini amalizie kazi ya kuhakiki na kutangaza matokeo na mshindi wa uchaguzi, badala ya kurudiwa uchaguzi.

Alisema, kama wanataka kulazimisha kufanyika kwa uchaguzi huo, Cuf haipo tayari kushiriki na badala yake Zec, wakamilishe uchaguzi wa Oktoba, mwaka huu.
‘Kama mtu mmoja anaweza kufunga ndoa basi mwaka huu tutashuhudia, lakini suala la Cuf kushiriki uchaguzi wa marejeo halipo,” alisema.

Alisema kitendo alichofanya Mwenyekiti wa Tume kufuta matokeo baada ya kuona mwelekeo wa uchaguzi mzito dhidi ya CCM, ni kwenda kinyume na misingi ya demokrasia na utawala bora.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Zec, Salum Kassim Ali, alisema baada ya kutangazwa rasmi katika gazeti la serikali kufutwa matokeo ya uchaguzi, hatua inayofuata ni kutangaza tarehe ya kufanyika uchaguzi huo.
Akizungumza na Nipashe jana, alisema wanaendelea kukamilisha utaratibu wa kutangaza tarehe hiyo na wakati ukifika watatangaza rasmi ili wananchi wapate kufahamu.

‘Wakati wa kutangaza tarehe ya kufanyika uchaguzi wa marejeo bado, wakati ukifika tutatangaza wananchi wafahamu,’ alisema Salum.

Wagombea wa Urais wa Zanzibar Juma Ali Khatib (Tadea), Kassim Bakar Ali (Jahazi asilia), walisema watatoa msimamo wa kushiriki uchaguzi huo au la baada ya vikao vya chama kukutana na kuamua.

Mgombea wa Urais Soud Said Soud (AFP) alisema Chama chake kinaunga mkono uamuzi wa Zec kurudia uchaguzi.
Hata hivyo, alisema kuna haja kwa Rais wa Zanzibar kufanya mabadiliko ya makamishna wa Zec kuondoa tatizo la kutetea maslahi ya vyama. na kukwamisha kazi za tume wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Hatua ya Zec kutangaza kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar imekuja wakati viongozi wakuu wa kitaifa wakiwamo marais wastaafu wakiendelea kukutana Ikulu Zanzibar kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar.
Tayari vikao viwili vimefanyika wiki hii na kuhudhuriwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, na mgombea mwezake Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar (Cuf), Seif Sharif Hamad.

Wengine ni Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, Rais mstaafu (Muungano) Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk Salmin Amour na Amani Abeid Karume.
CHANZO: NIPASHE

Share: