Habari

Vyama vya upinzani vyatumia siku ya uhuru kudai uhuru

Na Aurea Simtowe – Mwananchi

Jumapili, Disemba 9, 2018

Vyama 15 vya siasa vya upinzani vimetoa tamko lao kupinga mswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa uliosomwa bungeni, Novemba 16 mwaka huu.

Miongoni mwa vyama vilivyoshiriki katika kutoa tamko hilo ni pamoja na ACT-Wazalendo, NLD, ADC, Chauma, Chadema, CTK, CUF, UDP, NCCR Mageuzi.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chauma) Hashim Rungwe amesema wameamua kutoa tamko hilo siku ya leo kwa sababu ni siku muhimu ambapo nchi ilizaliwa upya na kuingia katika historia ya kukumbukwa.

“Tumetumia siku hii kwa sababu tunaona dalili za mkoloni mweusi kurejea nchini mwetu na tunampinga ili asiweze kufanikiwa kwa sababu sheria inapendekeza wanasiasa kufanya shughuli zao kwa uhuru lakini hivi sasa jambo hilo linapotea.

“Tumeona nchi nyingi zimeingia katika vurugu kutokana na wao kudai haki zao kwa nguvu ila sisi hatutaki kufanya hivyo ndiyo maana tumeamua kuudai kwa utulivu,” amesema Rungwe.

Amesema sheria hiyo inaweza kuingiza taifa katika vurugu kubwa siku za baadaye kwa sababu inapinga katiba ya nchi inayotoa uhuru wa kujumuika na kushiriki katika shughuli mbalimbali.

Katika habari nyingine ya Aurea Simtowe, iliyopewa kichwa cha habari: ‘Chadema na CUF watapinga mswada wa vyama kwa nguvu zote’

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji amesema mswada wa marekebisho wa sheria ya vyama vya siasa unaondoa uhuru wa kushirikiana kisiasa na kumpa msajili kinga ya kutoshtakiwa au kupingwa katika vyombo mbalimbali vinavyotoa haki.

Ameeleza hayo leo Jumapili, Desemba 9, 2018 wakati wa mkutano uliovikutanishwa vyama 15 vya siasa vya upinzani wakati vikitoa tamko lao la kupinga mswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa uliosomwa bungeni Novemba 16 mwaka huu.

Dk Mashinji amesema Chadema haikubaliani na inapinga mswada huo kwa sababu unalenga kumtengeneza mfalme mpya ndani ya vyama vya siasa.

“Hatukubaliani, mswada huu ni dhaifu, wa hovyo na unalenga kuondoa ushirikiano baina yetu,” amesema Dk Mashinji.

Naibu Katibu Mkuu CUF , Joram Bashange amesema sheria hiyo imechukua mapendekezo mengi yaliyofanywa na nchi ya Rwanda 2013 uliompa nguvu Rais wa nchi hiyo Paul Kagame kufanya kile anachokihitaji.

“Hivyo tutapinga kwa nguvu zote kuhakikisha suala hili halifanikiwi ili kuweza kukinga madhara yanayoweza kutokea baadaye na nitashirikiana na mtu yoyote atakayesimama kupinga suala hili,” amesema Bashange.

Naye, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amesema mswada wa marekebisho wa sheria ya vyama vya siasa ukiwa sheria mfumo wa vyama vingi vya siasa utaondoka. “Mswada utaondoa mfumo wa vyama vingi nchini.’

Zitto amesema hayo wakati wa mkutano uliovikutanisha vyama 15 vya siasa vya upinzani kupinga mswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa, uliyofanyika leo Jumapili, Desemba 9, 2018 kwenye Hotel ya Bahari Beach, Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano huo, Kabwe amesema wapo watu waliopambana ili kuhakikisha demokrasia ya mfumo wa vyama vingi unakuwepo nchini.

“Wengine walikuwa ni wanafunzi walijitolea kuhakikisha demokrasia hiyo inakuwapo kikamilifu hivyo na sisi tunaahidi kuwa tutaudhibiti kikamilifu ili kuhakikisha haupitishwi kuwa sheria,” amesema Zitto

Amesema japo kuwa mswada huo bado haujapitishwa lakini utekelezaji wake kupitia chama tawala umeanza kuonekana na unalenga kudhoofisha na kuua vyama vingine vya siasa.

“Tutasimama kikamilifu kuhakikisha hilo halitokei japo kutakuwa na chokochoko nyingi zinazolenga kutugawa lakini tutasimama imara,” amesema Kabwe.

Katika hatua nyingine, Pater Elias wa Gazeti la Mwananchi ameripoti habari hiyo hiyo kwa kichwa cha maneno kuwa upinzani unasema mswada wa vyama umejaa makosa ya jinai.

Vyama vya upinzani nchini vimetoa tamko kupinga mswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa vikidai kwamba mswada huo una lengo la kuua upinzani nchini.

Akisoma tamko la vyama hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chaumma), Hashimu Rungwe amesema wanapinga sheria hiyo kwa sababu inakiuka haki ya kikatiba ya uhuru wa watu kukusanyika kwenye shughuli za kisiasa.

Amesema mswada huo umejaa makosa ya jinai ambayo yanatishia uwepo wa vyama hivyo na Msajili wa Vyama vya Siasa amepewa mamlaka makubwa ikiwemo kumvua uanachama mtu yoyote kwenye chama cha siasa.

“Kwenye mswada huu, msajili wa vyama vya siasa amejipa mamlaka makubwa ambayo yanaingilia uhuru wa vyama, kwani msajili anaweza kumfukuza mwanachama wa chama chochote cha siasa. Msajili sasa amekuwa mdhibiti wa vyama vya siasa na siyo mlezi,” amesema Rungwe.

Rungwe amesema maoni yaliyotolewa na vyama vya siasa kuhusu mswada huo hayajaingizwa kwenye mswada huo, jambo linalowafanya wadhani kwamba hizo ni njama za serikali kutaka kuua vyama vya upinzani.

Akifafanua yaliyomo kwenye mswada huo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema – Zanzibar, Salum Mwalimu amesema kifungu cha 5 (a) kwenye mswada huo unaeleza kwamba msajili wa vyama anatakiwa kupata taarifa na kutoa kibali cha mafunzo kwa viongozi wa chama.

Amesema kifungu kingine cha 5 (d) nacho kinasema msajili anaweza kuhitaji taarifa zozote za chama cha siasa kutoka kwa mwanachama yoyote.

“Huu ni utaratibu gani jamani, si bora wangesema apate taarifa kutoka kwa viongozi?. Watapandikiza watu wao kwenye vyama na kutumia taarifa zao kuviadhibu vyama vya siasa,” amesema Mwalimu.

Amesema sura ya 18 inaeleza kwamba chama cha siasa kikipata hati chafu kwenye ukaguzi wa hesabu zake basi ruzuku yake itazuiliwa kwa kipindi cha miezi sita.

Amesema kifungu hicho kina lengo la kuviadhibu vyama vya siasa kwa kuvinyima fedha kwa ajili ya kujiendesha.

Share: