Habari

Waandishi wazuiwa kuripoti kesi ya Uamsho

Wanachama wa kundi la uamsho wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakiwa chini ya ulinzi Askari Magereza. Picha na Maktaba

Na Tausi Ally

Ijumaa,Juni19 2015

Imeelezwa kuna watu huwa wanarekodi mwenendo wa kesi hiyo na kurusha kwenye mitandao ya kijamii hali ambayo ni kinyume cha sheria.
Dar es Salaam. Waandishi wa habari jana walizuiwa kuripoti kesi ya ugaidi inayowakabili viongozi 23 wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo saa 3:15 asubuhi na kupelekwa kwenye chumba cha mahakama ya wazi namba moja wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari polisi na wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), waliokuwa wamebeba silaha na mabomu ya machozi.

Baada ya kuingia mahakamani hapo wakiwa wanamsubiri hakimu anayeisikiliza kesi yao, waandishi wa habari walijisogeza kutaka kuingia kwa lengo la kuripoti kesi.

Lakini cha ajabu, walipofika askari wa FFU waliokuwa wamebeba silaha na askari kanzu wa magereza waliokuwa wameuzingira ukumbi huo, waliwakataza waandishi kusogelea mlango wa kuingilia.

Hata hivyo, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Inspekta Jackson Chidunda alidai kuwa upande wa mashtaka wameiomba mahakama na imeridhia kuwa kuanzia leo (jana), waandishi wa habari hawapaswi kuripoti tena kesi hiyo kwa sababu za kiusalama na kiintelejensia.

Chidunda alidai kuwa ombi hilo lilitolewa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Peter Njike mbele ya Hakimu Mkazi, Renatus Rutta kupitia kifungu cha 34 (4) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.

Kwa upande wa mawakili wanaowatetea washtakiwa hao, Ubaidu Hamidu na Abdulfattah Abdallah walidai kuwa upande wa mashtaka waliomba waandishi wa habari kuzuiwa kuripoti kesi hiyo kwa sababu inasadikiwa kuna watu wanarekodi na kwenda kurusha mwenendo wake katika mitandao ya kijamii, kitu ambacho ni kinyume na matakwa ya Mahakama.

Hata hivyo, walidai kuwa Hakimu Rutta aliwaeleza kuwa kwa sababu kesi hiyo bado haijaanza kusikilizwa bali inatajwa, hakuna haja ya kuwapo kwa watu wengi mahakamani hadi hapo itakapoanza kusikilizwa.

Ilipofika saa tano asubuhi, washtakiwa waliondolewa eneo la Mahakama kwa kutumia basi la magereza lililoongozwa na gari moja la maji ya kuwasha la polisi na Land Rover Deffender tano za FFU.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao akiwamo Sheikh Farid Hadi Ahmed (43), ambaye pia ni kiongozi wa jumuiya hizo na wenzake, wanakabiliwa na makosa manne ya kushiriki vitendo vya ugaidi.

Chanzo Mwananchi

Tagsslider
Share: