Habari

Wabunge, Wawakilishi Tafuteni Ridhaa za Wananchi

.Watakiwa Kuzungumza nao Kabla ya Kuwaamulia

Thursday, June 7, 2012
Na Madina Issa

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai amewapiga ‘stop’ wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuzungumzia masuala ya kitaifa yanayowahusu wananchi bila ya kupata ushauri wao.

Naibu huyo alieleza hayo alipokuwa akizungumza na wajumbe wa halmashauri kuu za Majimbo ya wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja.

Alisema haipendezi kwa Mbunge au Mwakilishi kutoa msimamo wake juu ya masuala yanayohusu taifa kupitia vyombo vya kutunga sheria huku akiwajumuisha wananchi wa jimbo lake, ilhali akijua kuwa hajawahi kwenda na kuzungumza nao.

“Nashangaa sana ninaposikia Mbunge au Mwakilishi anajitapa ndani ya Bunge au Baraza la Wawakilishi kwa kusema kwa niaba ya wananchi wa jimbo langu, tunaunga mkono au kukataa hoja, huku akijua fika kuwa hakukutana na kujadiliana na wapiga kura wake kutaka msimamo wao juu ya hoja fulani ya maslahi ya nchi”, alisema Naibu huyo.

Alisema wakati umefika kwa viongozi hasa waliochaguliwa na wananchi majimboni kuacha tabia ya kujipigia kifua na kuwasemea wananchi mambo yanayohusu mustakbali wa nchi, kwani kufanya hivyo kutaweza kuleta mitafaruku.

Akizungumzia suala la Muungano, Naibu Vuai alisema Chama cha Mapinduzi kitaendelea na sera yake ya serikali mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Aprili 26, 1964) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (Januari 12, 1964).

Akizungumzia juu ya uchaguzi mkuu wa CCM unaoendelea nchini kote aliwataka viongozi na wanachama wa CCM kuanzia ngazi za wadi, jimbo, wilaya na Mkoa, kuhakikisha wanawachagua viongozi bora, makini, wenye uwezo mkubwa wa kuchambua na kusimamia kwa nguvu ya hoja masuala mbalimbali ya kisiasa.

Hata hivyo alisema kuwa viongozi ndiyo wenye jukumu la kuhakikisha suala la umoja, maelewano na mshikamano unadumishwa ndani ya chama kwani umoja mshikamano ndio ngao na silaha thabiti itakayoweza kukipatia ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2015.

Alifahamisha kuwa nguvu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kisiasa zinaweza kupunguzwa na watu wasiokitakia mema Chama hicho na kusema hilo linaweza kufanikiwa endapo wanachama na viongozi wake watakubali kugawanywa na wenye kukubali kugawanyika.

“Iwapo viongozi katika ngazi mbalimbali wataanza kugombana wenyewe kwa wenyewe na kutoshikamana, hali hiyo itatoa mwanya kwa mahasimu wetu wa kisiasa kujijenga zaidi”. Alisema Naibu huyo.

Aidha alisisitiza kuwepo mashirikiano baina ya wanachama pamoja na viongozi wao kwa kuhakikisha wanafanya kazi ya Chama wakiwa nje ya Chama pamoja na ndani ya umma tena kwa bidiii zaidi, kwani wataweza kuleta maendeleo ya Taifa na wananchi wake.

Naibu huyo yumo katika ziara ya kisiasa ya siku sita katika wilaya zote 10 za Mikoa ya Zanzibar, kwa lengo la kuangalia na kuhimiza na uhai wa Chama cha Mapinduzi.

Chanzo: Zanzinews

Share: