Habari

Wachina watishwa

Na Mwandishi wetu
23rd September 2013
Maisha ya raia wa China wanaoishi nchini, yako hatarini, kutokana na mtu anayejiita kuwa ni ‘Kamanda wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Asilia’, kusambaza ujumbe kwenye mtandao wa kompyuta unaotishia kuwaua akiwatuhumu kwa makosa 21 dhidi ya Tanzania.

Ujumbe huo ulioandikwa kwa lugha ya Kiingereza wenye kichwa cha habari: “Yah: Killing of all Chinese citizens in Tanzania” (Yah: Kuwaua raia wote wa China walioko Tanzania), umeelekezwa kwa Balozi wa China nchini, Lu Younqing, ambaye umemtaja kimakosa kwa jina la Liu Xinsheng.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, aliahidi kufuatilia taarifa hizo.

Mtu huyo anaanza kudai katika ujumbe huo kuwa wamekasirishwa na kile alichokiita “Matusi ya Balozi Younqing dhidi ya Watanzania” kwa kuingilia siasa za Tanzania na kujifanya msemaji wa CCM.

“Tukiwa ni wananchi wa Tanzania, tunatangaza kwamba, tumekasirishwa na hilo. Hivyo, tunataka raia wote wa China waondoke haraka nchini na iwapo hawatafanya hivyo watakuwa walengwa wa mauaji,” ulieleza ujumbe huo na kuongeza:

“Tutawakata shingo zenu, kuwamwagia tindikali popote pale kutoka Mtwara hadi Moshi. Serikali na Uhamiaji hawawezi kufanya lolote. Ni lazima tuwashughulikie.”

Ujumbe huo unadai watatekeleza maovu hayo kwa madai kwamba, Balozi Younqing ndiye aliyesababisha kwa kuingilia mambo ya ndani ya Tanzania, baada ya kuwaibia Watanzania kila kitu.

Mbali na balozi kudaiwa kufanya hayo, ujumbe huo unasema pia raia wa China wamekuwa wakiingiza nchini samaki waliooza kwa nia mbaya ya kuwaua Watanzania.

Unadai kuwa maneno ya balozi huyo yameonyesha kuwa ni adui mkubwa kuliko kundi la Al-qaeda.

“Raia wa China watakuwa ndiyo lengo letu kubwa, tutawaua wote kwa wakati mmoja. Tunashauri uchukue taarifa hii kwa umakini kwa sababu CCM Asilia tutawaua nyote na vichwa vyenu kuvilisha mbwa,” unasema ujumbe huo.

Unadai CCM-Asilia ni watu wanaoendesha mambo yao chini kwa chini, wana mafunzo na mpangilio na wamejiunga na wanajeshi wastaafu wazalendo kukomboa nchi yao.

“Ni kundi ambalo lina sumu ya kukabiliana na tishio la Wachina nchini,” unaeleza ujumbe huo.

Ujumbe huo unaeleza kuwa CCM-Asilia wanamiliki silaha za kutosha na pia wana uwezo wa kiufundi wa kuua kila Mchina nchini kwa sababu mbalimbali, ikiwamo Wachina kuvamia hifadhi za Taifa na kuchimba dhahabu na madini mengineyo.

Sababu nyingine ni Wachina kuharibu misitu, kujihusisha na ukahaba jijini Dar es Salaam, vitendo ambavyo vinapingwa na Waislamu.

Unataja sababu nyingine kuwa ni Wachina kupora ardhi iliyopo kwa ajili ya chakula cha Watanzania na kuitumia kwa manufaa yao na kuwatesa Watanzania kila mahali wanakokwenda.

Sababu nyingine ni kuchafua mazingira, kuharibu uchumi wa nchi, kuuza dawa za kulevya, kupora ajira ya Wamachinga Kariakoo, kupora ajira ya ujenzi na kwamba, sasa wanataka pia kupora kazi zote za gesi.

Unadai sababu nyingine ni Wachina kuuza chakula kibovu kinachohatarisha maisha ya Watanzania, kuua tembo na vifaru, kujihusisha na rushwa kubwa, ambayo haikubaliki katika nchi yao.
Pia kutumia vibali bandia, kujenga barabara na majengo mabovu nchini.

Alipoulizwa na NIPASHE jana kuhusiana na ujumbe huo, Kamishna Manumba alisema bado hajaupata, lakini akaahidi kuwa atafuatilia.

“Nashukuru kwa kunipa taarifa hiyo. Tutafuatilia,” alisema Kamishna Manumba.
Hata hivyo, jitihada za NIPASHE kumpata Balozi wa China ili azungumzie vitisho hivyo, hazikufanikiwa baada ya simu yake kutopatikana.

CHANZO: NIPASHE

Share: