Habari

Wageni watakiwa kuwalinda popo

DECEMBER 6, 2017 BY ZANZIBARIYETU
Wageni watakiwa kuwalinda popo

NA HAJI NASSOR, PEMBA

WAGENI wanaotembelea hifadhi ya popo wa Pemba, ambao hawapatikani sehemu nyengine duniani, wametakiwa kuacha tabia ya kuwalazimisha wanyama hao kuruka.

Popo hao wanahifadhiwa katika hifadhi iliopo Kidike shehia ya Mjini Ole, wilaya ya Chake Chake.

Kauli hiyo imetolewa na mtembeza wageni kutoka hifadhi hiyo, Omar Aminia Hamad, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uhifadhi wa wanyama hao.

Alisema licha ya kutoa elimu kwamba popo hawatakiwi kuamshwa wakiwa wamepunzika nyakati za mchana, bado baadhi ya wageni wananaopuuza taratibu hizo.

Alisema usiku mzima popo hao huwa katika harakati za kujitafutia chakula, hivyo sio busara kuamshwa wakati wanapokuwa wamelala.

“Wapo baadhi ya wageni hawaheshimu taratibu za ndani ya hifadhi na kupinga maelezo yetu, kwamba popo mchana hawatakiwi kufanyiwa kelele au kuamshwa kwa sababu ni muda wao wa kupumzika,” alisema.

Aidha alisema uwepo wa hifadhi hiyo imetoa fursa kwa wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo kupata michango ya miradi ya maendeleo.

“Hifadhi ya Kidike inasaidia huduma ya umeme kwenye msikiti mkuu, uimarishaji wa elimu ya maandalizi na kuchangia yanapotokezea maafa kijijini hapa,” alisema.

Kwa upande wake mwananchi Omar Shaame (50), alisema yeye hajaona manufaa ya aina yoyote ya kuwepo kwa hifadhi hiyo, ingawa anaona bado kuna umuhimu wa kuwahifadhi wanyama hao.

Alisema anashuhudia wazungu na watu wengine wakiingia katika hifadhi hiyo lakini hakuna manufaa anayoyaona kama mwanakijiji.

“Hii ni hazina yetu, lakini mimi sijawahi kushiriki au kushirikishwa hata mkutano mmoja wa kijiji juu ya uhifadhi huu,” alisema.

Nae Mwanaisha Bakar, alisema hifadhi hiyo ina msaada mkubwa kwao hasa kwenye sekta ya elimu ya maandalizi.

Alisema uwepo wa popo hao, umesaidia kupata rutba kwenye mimea yao na kupata miche ya baadhi ya miti kama miembe, mishokishoki ambayo anaamini imeletwa na popo hao. Hifadhi hiyo iliyoanzishwa mwaka 1992 ina popo zaidi ya 5,000.

Zanzibar Yetu

Share: