Habari

Waislamu wawaunga mkono UKAWA

by Shehe Semtawa 01/08/2014

Sheikh Rajab KatimbaWAKATI Umoja wa Katiba (UKAWA) ukiwalaumu baadhi ya viongozi kwa kupendelea CCM, Jumuiya, Taasisi za Kiislamu na Shura ya Maimamu nchini, wamewataka wasirejee bungeni hadi watakapohakikishiwa kuwa mawazo ya wananchi yaliyopendekezwa kwenye rasimu yanazingatiwa.

Kauli hiyo imetolewa jana na msemaji wa jumuiya hiyo, Sheikh Rajab Katimba, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema mchakato wa katiba unasimamiwa na wananchi, hivyo kupuuza mawazo yao si sahihi.

Alisema wananchi ndio waliopendekeza serikali tatu kwa sababu ya kero mbalimbali zinazoikabili Serikali ya Muungano kwa kipindi chote cha zaidi ya miaka 50.

Sheikh Katimba, alisema katiba inayotaka kuandikwa siyo ya chama chochote, ni katiba ya Watanzania wote, wawe na dini au wapagani. Kwamba inamhusu kila mtu, hivyo hakuna sababu ya kupuuzwa kwa mawazo yao na kuthaminiwa ya vyama.

Alisema taasisi hizo zimeamua kuwaunga mkono UKAWA kwakuwa mawazo yao ndiyo yanayolingana na rasimu ya katiba inayotaka muundo wa serikali tatu kama yalivyoratibiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

“Hata kabla ya mawazo ya wananchi, wao waliwahi kukaa kwa pamoja na kupendekeza kwamba kutokana na kero zilizodumu ndani ya Muungano kwa zaidi ya miaka 50, ni bora kuwa na serikali tatu ambazo ni ile ya Tanganyika, Zanzibar na ya Muungano ambazo wana imani zitapunguza kero za muungano,” alisema.

Alisema wameshangazwa kuona maoni ya wananchi yalipofikishwa bungeni yalibadilishwa na hivi sasa wajumbe wanatakiwa kujadili maoni ya serikali mbili ambayo hayakuwa ya wananchi.

“Hilo la serikali mbili hatulikubali na sio sahihi, tutaendelea kutetea mwananchi yeyote mpenda haki ambaye anazingatia maoni ya wananchi, na wanaomba UKAWA wasirudi bungeni hadi Bunge hilo litakapokubali kujadili mawazo ya wananchi na sio mawazo ya wale wanaotaka serikali mbili,” alisema Sheikh Katimba.

Alitoa rai kwa wananchi kufuatilia kwa karibu mchakato huo kwa sababu katiba inayoandaliwa ndiyo sheria mama ambapo sheria zote ndogo ndogo za nchi zitaundwa kutoka humo.
Chanzo Tanzania Daima

Tagsslider
Share: