Habari

Wajumbe wa Z’bar watishwa

Samuel-Sitta

Na Daniel Mjema, Mwananchi

Jumapili,Septemba 21 2014

Baadhi ya kamati za Bunge zimependekeza Rais wa Zanzibar awe makamu wa kwanza wa Rais na Waziri Mkuu awe makamu wa pili wa Rais wa muungano.
Dodoma. Hali imeanza kuwa tete Bunge la Katiba kutokana na ujumbe unaosambazwa kwa kasi katika mitandao ya kijamii, ili kuwagombanisha na kuwafitinisha wajumbe wa kundi la 201 kutoka Zanzibar.

Ujumbe huo ambao gazeti hili limeuona, ulianza kusambazwa juzi, ukiwataka wajumbe wa kundi la 201 kutoka Zanzibar, kuondoka bungeni ili theluthi mbili ya Katiba inayopendekezwa isipatikane.

Upigaji wa kura kulingana na masharti ya Ibara ya 37 ya kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, unatarajiwa kuanza Septemba 29 na kukamilika Oktoba 2 mwaka huu.

Hata hivyo, taarifa nyingine zimedai ujumbe huo unatumwa na baadhi ya wanaCCM kama mbinu ya kuwakatisha tamaa kundi la 201 wanaoonekana kuwa na msimamo thabiti ili hatimaye warudi upande wa CCM kwa kuona wamenyanyapaliwa.

Ujumbe huo unaaminika unaweza kuwa ni sehemu ya propaganda kutoka kwa baadhi ya wanaCCM kutoka Maskani ya Kisonge Zanzibar ili wajumbe hao waanze kusalitiana na wale wenye msimamo wajenge chuki na kusalimu amri.

“Tunawaambia wazi wajumbe hao wa kundi la 201 watoke katika Bunge la Katiba mara moja kabla ya upigaji wa kura vinginevyo hatutawaelewa,” unasomeka ujumbe huo wa WhatsApp na kuongeza;

“Hatuhitaji wapige kura ya siri wala ya wazi. Tunachohitaji ni theluthi mbili ya Zanzibar isipatikane kabla hata ya huo upigaji wa kura”, unasomeka ujumbe huo ambao umeweka picha za baadhi ya wajumbe baadhi ya wanaCCM kama mbinu ya kuwakatisha tamaa kundi la 201 wanaoonekana kuwa na msimamo thabiti ili hatimaye warudi upande wa CCM kwa kuona wamenyanyapaliwa.

Ujumbe huo unaaminika unaweza kuwa ni sehemu ya propaganda kutoka kwa baadhi ya wanaCCM kutoka Maskani ya Kisonge Zanzibar ili wajumbe hao waanze kusalitiana na wale wenye msimamo wajenge chuki na kusalimu amri.

“Tunawaambia wazi wajumbe hao wa kundi la 201 watoke katika Bunge la Katiba mara moja kabla ya upigaji wa kura vinginevyo hatutawaelewa,” unasomeka ujumbe huo wa WhatsApp na kuongeza;

“Hatuhitaji wapige kura ya siri wala ya wazi. Tunachohitaji ni theluthi mbili ya Zanzibar isipatikane kabla hata ya huo upigaji wa kura”, unasomeka ujumbe huo ambao umeweka picha za baadhi ya wajumbe.

“Na kama hawakutoka, tunawataka Wazanzibari wawatambue wasaliti hawa, wawalaani kwa nguvu zote na wawaorodheshe katika daftari la wasaliti wa Zanzibar kama wenzao akina Balozi Seif Ali Idd (Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar),” umesisitiza.

Balozi Idd ambaye ni kada wa CCM, amekuwa akitamka wazi kuunga mkono mchakato wa Katiba unaoendelea mjini Dodoma, tofauti na baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar wanaotaka muundo utakaoipa Zanzibar mamlaka kamili.
Watumaji wa ujumbe huo wanaotumia mtandao wa WhatsApp, wametaka ujumbe huo usambazwe kwa Wazanzibari wenzao waliopo ndani na nje ya nchi.

“Linalotusikitisha ni sehemu ya hili kundi la 201 ambao kwa nje wanaonyesha kuunga mkono madai ya Wazanzibari, lakini kwa ndani wanaonekana kumbe na wao ni mpini wanalitumikia shoka kuimaliza Zanzibar,”unadai ujumbe huo.

“Wazanzibari hatuko tayari kupoteza nchi yetu na vizazi vyetu kwa masilahi ya wanafiki wachache walioamua kwa njaa zao kufakamia mamilioni ya fedha ili kuiangamiza Zanzibar,” unasomeka ujumbe huo.

Baadhi ya kamati za Bunge zimependekeza Rais wa Zanzibar awe makamu wa kwanza wa Rais na Waziri Mkuu awe makamu wa pili wa Rais wa muungano.

Hata hivyo, zipo kamati zilizopendekeza kuwapo makamu watatu wa Rais ambapo Rais wa Zanzibar anapendekezwa awe makamu wa kwanza wa Rais, mgombea mwenza awe makamu wa pili wa Rais na waziri mkuu awe makamu wa tatu.

Wajumbe wauona

Hata hivyo, Mjumbe wa Bunge hilo kundi la 201 kutoka Zanzibar, Salma Said alikiri kuuona ujumbe huo na kwamba hana wasiwasi na kilichoandikwa katika waraka huo kwa kuwa anaamini wametumia njia yao ya kidemokrasia ya kujieleza na kutoa maoni yao kama wananchi ingawa njia waliyotumia siyo sahihi ya kuwaita watu wasaliti.

Alisema wakati huu ni muhimu wa kujenga umoja wa Wazanzibari na siyo kujenga uadui kwa kushutumiana.

Naye Dk Alley Nassoro kutoka kundi hilo alikiri kuuona ujumbe huo na akasema una lengo la kuwavuruga Wazanzibari wenye msimamo thabiti wa kutetea masilahi ya Zanzibar katika katiba.

“Baadhi yao walioandaa ujumbe huo tunawafahamu na wamefanya mambo ya ajabu hata kule Zanzibar na nataka niwaambie Wazanzibar kuwa watu hao ndiyo wametufikisha hapa tulipo,” alisema.

Dk Alley alisema ujumbe huo unasambazwa na maadui wa Zanzibar na lengo la kusambaza ni kuwafarakanisha wajumbe wanaotoka visiwani wasiwe na mshikamano.
Mjumbe mmoja wa Bunge hilo anayetajwa kwenye ujumbe huo alisema ana matumaini bado ataendelea kuwapo bungeni kwa vile alishiriki mchakato huo tangu hatua za mwanzo za Bunge.

“Nataka niwahakikishie Wazanzibari kuwa watulie, msimamo wetu ni thabiti wala hauyumbi. Huo ujumbe ni mbinu tu ya kutaka kutufitinisha na kutukatisha tamaa. Tumekuja kuwakilisha masilahi ya Zanzibar,” alisema mjumbe huyo na kuongeza;

“Tukiona ipo haja ya kuondoka na kuliacha Bunge tutafanya hivyo kwa masilahi ya Zanzibar. Sisi ni watu wazima na tunaamini hizi ni nchi mbili na zitabaki kuwa mbili na Zanzibar yenye dola kamili.”

Kanuni ya 37 ya Bunge la Katiba, inaeleza ili ibara au sura iweze kupitishwa na Bunge ni lazima iungwe mkono na theluthi mbili ya wajumbe wa Tanzania Bara na idadi kama hiyo ya wajumbe wa Zanzibar.

Ni kutokana na hofu ya kutopatikana kwa theluthi mbili, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta aliwataka mawaziri na naibu mawaziri kuwepo bungeni kuanzia Septemba 29.

Wito kama huo ameutoa pia kwa wajumbe wa Bunge hilo walioshiriki mjadala wa Bunge hilo, bila kuhusisha Ukawa waliosusia Bunge hilo tangu Aprili 16.

Sitta mara zote tangu kuanza kwa Bunge hilo Agosti 5 amekuwa akiwahakikishia Watanzania kuwa Bunge hilo litakamilisha kazi yake na kuwapatia Watanzania Katiba bora.

Hata hivyo, habari kutoka kwa baadhi ya wajumbe zinadai kwamba ili Katiba hiyo iweze kupata theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar, CCM na washirika wake wanahitaji kura 79.

“Jumla ya Wazanzibar wote ndani ya Bunge ni 217 na theluthi mbili yake ni wajumbe 144 kwa hiyo ukitoa wajumbe 66 wa Ukawa ambao tayari hawapo ina maana theluthi mbili ni kura 78,” kilidokeza chanzo hicho.

Hata hivyo, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro amenukuliwa akisema wajumbe wote wa Bunge hilo ni 630 na kati ya hao, wajumbe waliotoka ni 130, idadi ambayo ni sawa na asilimia 21 ya wajumbe wote.

“Wajumbe waliobaki ndani ya Bunge ni 500 sawa na asilimia 79 ya wajumbe wote na idadi hii ni pamoja na wajumbe 189 kutoka kundi la 201 ambao wamebaki bungeni,”alisema.

“Wajumbe wanaotoka Tanzania Bara ni 348 na kati ya hao 125 ni wanaotoka kundi la 201. Ukitazama takwimu zote hizi, wajumbe wa 201 ni sehemu ya Bunge hili,” alisema Dk Migiro na kuongeza;
“Kwa Zanzibar wajumbe waliobaki ndani ni 152 na kati ya hao 64 wanatokana na kundi la 201. Waliosusia Bunge kwa pande zote za muungano hawafikii theluthi moja ya wajumbe waliobaki.”

“Hii ina maana kwa kuzingatia matakwa ya kisheria kuwa uamuzi upatikane kwa majadiliano na kushawishiana kwa hoja, wajumbe waliobaki kwa wingi wao wanao uhalali wa kisiasa na kisheria,” alisisitiza Dk Migiro.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis Hamad alisema kuwa hajapata taarifa za kusambaa kwa ujumbe huo, lakini anaamini mtu anayefanya hivyo ana nia mbaya na Bunge hilo.

Pia, alisema ni rahisi mtu kuamini kuwa ujumbe huo unasambazwa na Ukawa kwa kuwa wao ndio waliotoka bungeni na kwamba wametangaza maandamano nchini nzima ya kupinga Bunge hilo.

“Ungeniambia ni Ukawa ningekuelewa kwa sababu wao ndio wametoka nje na wanatangaza maandamano nchi nzima…lakini kwa sababu bado sijaouna siwezi hasa kusema unaweza kuwa na athari kiasi gani kwenye Bunge la Katiba,” alisema.

Chanzo Mwananchi

Share: