Habari

Wajumbe wapya ZEC tazameni hapa

JULY 21, 2018 BY ZANZIBARIYETU

Zanzibar imepata Tume mpya ya Uchaguzi (ZEC), lakini sura za wajumbe wake wengi si mpya katika masuala ya uchaguzi, sheria na siasa za Zanzibar.

Mwenyekiti wake ni Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar, Hamid Mahmoud Hamid ambaye aliwahi kuwa ofisa mwandamizi wa Jeshi la Polisi na makamu mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Tume hii inayo miaka miwili na miezi minne ya kutayarisha uchaguzi wa sita wa mfumo wa vyama vingi nchini.

Nani asiyetambua kuwa chaguzi zilizopita zililalamikiwa ndani na nje ya nchi kwamba zilikuwa na dosari za wazi na zilizojificha.

Hali hii ilizusha mtafaruku wa kisiasa ambao kila ulipoonekana kupatiwa ufumbuzi paliibuka tena mvutano mwingine uliopelekea watu kadhaa kupoteza maisha yao, wengine kuwa vilema na mamia kuhama nchi.

Ni vizuri wajumbe wakaelewa na kukubali kwamba wamebeba jukumu zito na historia ndiyo itakayo wahukumu kwa namna watakavyoendesha uchaguzi ujao.

Kwa mfano, haiingii akilini kwa kura zilizopigwa katika jimbo, kama ilivyowahi kutokea siku za nyuma, kuwa nyingi kuliko idadi ya watu waliojiandikisha kuwa wapiga kura.

Vile sifahamu wala sitafahamu kwa nini vyombo vya habari vizuiwe kutangaza matokeo yaliyobandikwa ukutani na maofisa wa uchaguzi kwenye vituo au hata na kuyafanyia majumuisho na kuyatangaza.

Sitafahamu inakuwaje, kama nilivyoona katika kituo kimoja Unguja, kutokea watu wanafika kituoni dakika chache kabla ya zoezi la kupiga kura kumalizika wakiwa wamebeba sanduku la kupiga kura na haikujulikana kilichokuwamo ndani.

Nimeona taarifa nyingi juu ya uteuzi wa tume uliofanywa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ambaye anamaliza ngwe yake ya pili na ya mwisho ya uongozi kwa mujibu wa katiba.

Zaidi kwenye vyombo vya habari vya serikali ambavyo huelezwa kuwa ni vya umma ni za pongezi kwa uteuzi mzuri wa wajumbe wa Tume, lakini havijagusia kundi ambalo haliridhiki na muundo wa ZEC. Kujenga taswira hii ni kujidanganya na kufumbia macho hali halisi. Hili unaweza usilione kama umeamua kufumba macho usione lililopo mbele yako.

Mwenendo wa kuukataa ukweli au kutafuta njia ya kupata suluhisho la kudumu katika jamii ya Wazanzibari utapelekea siku zote kuendelea kuwepo mgogoro wa kisiasa Zanzibar.

Kwa kiasi fulani sifa iliyokuwepo visiwa hivi vya marashi ya karafuu vyenye mchanganyiko wa watu wenye ustaarabu, waliopendana, kusikilizana, kuheshimiana na kuvumiliana imekuwa sehemu ya historia.

Hapa napenda kukumbusha nukuu maarufu ya Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, aliyoitoa miaka iliyopita. Alisema waliojijengea dhana kuwa hapana matatizo Zanzibar waelewe wao ndio wenye matatizo.

Kauli hii iliungwa mkono na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Jakaya Kikwete, ambaye baadaye alikuja kuwa Rais wa Muungano.

Bado ninaamini kauli ya Warioba ilikuwa ya hekima na busara na yenye na mantiki na isingefaa kupuuzwa wakati ule na hata hivi sasa.

Wapinzani wapongeza

Ukiangalia viongozi wa vyama vya vinavyoitwa vya upinzani waliopongeza uteuzi wa wajumbe na kusema tume ipo huru hata kabla ya kuanza kazi, utagundua ni watu ambao idadi ya wafuasi wao wanahesabika vidoleni.

Baadhi yao waligombea uchaguzi wa Rais wa Zanzibar na sasa wanashika nafasi za mawaziri katika serikali.

Lakini, nataka ikumbukwe katika chaguzi hizo watu hao hawakuungwa mkono na Wazanzibari wengi na kama kura za wote zingechanganywa zisingejaza hata mfuko wa plastiki wa rambo.

Hili si vizuri kulifumbia macho kundi linalotoa ushindani mkubwa katika chaguzi zote linaloongozwa na aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Huu ndio ukweli ijapokuwa ukizungumziwa wapo wanaokasirika na kununa, lakini yoyote anayeitakia mema Zanzibar hawezi kufumbia macho suala hili.

Nimetoa maangalizo haya kukumbusha wajumbe wapya wa Tume na viongozi wa SMZ kwamba hili lipo na haistahili kufumbiwa macho wala kulizibia masikio.

Ni vizuri tukakataa kuongozwa na utashi wa kisiasa na kuikabili kwa ujasiri hali halisi na kutafuta njia itakayohakikisha hatima njema kwa Zanzibar ya kesho na siku zijazo.

Tukatae kuongozwa na jazba, ari, utashi wa kisiasa au maslahi binafsi.

Mazingira yaliyopelekea Zanzibar kuelezwa ni njema atakaye aje (kwa kheri na sio kwa shari) yalitokana na ujasiri mkubwa wa watu wake.

Nao ni kuikubali hali halisi ya mchanganyiko wa watu wake, wenye fikra na mawazo tafauti, lakini wakaamua kuishi kwa maelewano na kupendana licha ya tafauti zao hata za umbo na rangi.

Ni vizuri kuiga mfano mzuri wa wazee wetu waliotangulia mbele ya haki. Kupuuza mwenendo wao ni kutowatendea haki wao na kizazi kijacho.

Tuitafakari kwa makini hali ya Zanzibar wakati tunaelekea kwenye uchaguzi wa mwaka 2020. Wajumbe wapya wa ZEC waitafakari hali halisi.

Tusikubai kurejea makosa tuliyoyafanya siku za nyuma. Kila mtu na zaidi wajumbe wa tume ajue kitu kinachoitwa dhima na aweke masilahi ya Zanzibar na watu wake mbele na mengineyo nyuma ya kisogo chake.

Tujifunze kwa tunayoyaona na kuyasikia hapa kwetu na nchi nyengine na tuzingatie ule msemo wa wazee wetu wa “Asiyekubali kufunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu”. Sisi tuliopo tutaondoka, lakini Zanzibar itabaki.

Tujitahidi kila mmoja wetu siku za mbele aje kuhukumiwa na historia kwa mema aliyoyafanya na sio maovu aliyoyatenda.

Tusameheane kwa maovu tuliotendeana na kuangalia ni mema gani kila mmoja atayafanya ili Zanzibar ing’are na sifa yake za zama za kale kurejea.

​CHANZO: MWANANCHI

Share: