Habari

Wanafunzi waliofaulu wazawadiwa Kengeja Pemba

Afisa mdhamin ofisi ya Makamo wa kwanza wa Rais Pemba Mh.Amran Massoud Amrani akimkabidhi mwanafunzi zawadi

Afisa mdhamin ofisi ya Makamo wa kwanza wa Rais Pemba Mh.Amran Massoud Amrani akimkabidhi mwanafunzi zawadi

AFISA mdhamini Ofisi ya makamu wa pili wa rais Pemba Amran Massoud Amran, ametika jamii kuelekeza nguvu zao kuwapatia watoto wao elimu, na sio kukazania fedha za mahari, kwa watoto wao wa kike.

Alisema wakati umefika sasa kwa jamii kuunga nguvu na jitihada za pamoja, kwa lengo la kuwasomesha watoto wao, na kuacha tabia ya tamaa ya mahari pale wanapowakatisha masomo watoto na kuwaoza waume.

Afisa mdhamini huyo alitoa tamko hilo jana, skuli ya sekondari ya Kengeja wilaya ya mkoani Pemba, kwenye hafla ya kuwakabidhi zawadi za sare na fedha taslimu kwa wanafunzi wa skuli hiyo waliofaulu ngazi ya michepuo na wale wa kuingia darasa la kumi na tatu mwaka 2013/2014.

Alisema elimu ndio kila kitu, na ndio maana kwenye kitabu kitakatifu cha qur-an, kumesisitizwa kuifuata elimu hata masafa ya mbali (china) kutokana na umuhimu wake kwa mwanadamu.

Alisema zipo aya kadhaa zilizoelezea umuhimu na faida kubwa ya elimu, na suala la ndoa limetajwa kwa mtazamo wa sunna kwa muislamu, hivyo sio vyema kumkatisha mtoto kitendo cha faradhi na kumpeleka kwenye sunna.

‘’Jamani wazazi na walezi wangu, tuone umuhimu mkubwa na mpana wa elimu, na ndio maana tumekuwa tukisisitizwa hata kwenye nyumba za ibada, lakini tumejisahau na kuelekeza nguvu zaidi kwenye ndoa ambayo imetajwa kuwa ni sunna’’,alifafanua.

Katika hatua nyengine amewataka wanafunzi, waalimu na wazazi wa wanafunzi hao waliofaulu kuthamini ushirikiano na mchango mkubwa uliotolewa na mzaliwa wa Kengeja Dk, Omar Dadi Sahajaki.

‘’Watu kama Dk Omar Dadi, ndio hawa wakuthaminiwa maana wamekuwa wakielekeza nguvu kwenye jambo ambalo ‘Allah’ amelizungumza sana la elimu’’,alifafanua.

Hata hivyo amewataka wazazi hao kuendelea kuchangia katika sekta ya elimu, wakijua kuwa wanapowasomesha watoto wao, ndio wamewajengea msingi madhibuti wa maisha yao ya baadae.

Mapema mwenyekiti wa kamati ya skuli ya sekondari ya Kengeja Hassan Abdalla, amesema juhudi zilioonyeshwa na wanafunzi hao zisiishie hapo na wajipange ili wafike vyuo vikuu.

Nae mratibu wa hafla hiyo, Khamis Juma Salim alisema uamuzi uliochukuliwa na dk Omar Dadi Shajaki wa kutoa gharama zake za kuwaweka kambini wanafunzi hao, unafaa kuungwa mkono na kila mmoja.

Katika hafla hiyo wanafunzi 18, wakiwa 16 ni waliofaulu dara la kumi na mbili kuingia kumi na tatu na wawili waliofaulu michepuo, walikabidhiwa vitambaa vya sare, pamoja na fedha taslimu za kushonea na kununulia viatu.

Afisa mdhamini akisalimiana na wanakengeja mara baada ya kufika skulini hapo kwa ajili ya utowaji wa zawadi

Afisa mdhamini akisalimiana na wanakengeja mara baada ya kufika skulini hapo kwa ajili ya utowaji wa zawadi

Baadhi ya wanafunzi waliofanikiwa kupata zawadi wakiwa pamoja na walimu wao

Baadhi ya wanafunzi waliofanikiwa kupata zawadi wakiwa pamoja na walimu wao

Share: