Habari

Wanafunzi wote Zanzibar kufanya mitihani ya kidato cha sita – Serikali

Na Ali Issa Maelezo Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzíbar imetoa taarifa rasmi ya kuruhusiwa kufanya mitihani ya kidato cha sita, mwezi Februari mwakani, wanafunzi wote 243 wa Zanzíbar waliopewa barua za kusimamishwa kufanya mitihani hiyo kwa kukosa sifa za kuwa na alama tano.

Taarifa hiyo imetolewa leo na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzíbar, Ali Juma Shamhuna huko Ofisini kwake Mazizini mjini wakati alipokutana na wandishi wa habari.

Waziri Shamhuna amesema maamuzi hayo yamefikiwa baada ya mazungumzo yake na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa Tanzania Bara Dk. Shukuru Kawambwa yaliyofanyika tarehe 30 Mwezi uliopita mjini Dar es salaam.

Amesema kutokana na maamuzi hayo wanafunzi wote waliosajiliwa kufanya mitihani watafanya mitihani yao baada ya marekebisho ya kasoro zilizojitokeza ambazo zilisababishwa na baadhi ya watendaji kutoka Wizara ya Elimu Bara kujichukulia mamlaka bila kuijulisha serikali ya Zanzíbar.

“Masula ya Elimu ya juu ni masuala ya Muungano, hivyo maamuzi yake yanapaswa kuwa ya pamoja kwa kushirikisha vyombo husika ambavyo vipo kwa mujibu wa taratibu na sheria kuwatumikia wananchi wa pande zote mbili za Tanzania na si vyenginevyo”. alisema Shamuhuna.

Alisema maamuzi ya awali ya kuwasimamisha wanafunzi waliokuwa hawana alama tano, yalitolewa bila ya kuwepo kikao halali cha Baraza la Mitihani Tanzania NECTA na lililofanyika ni kuwaandikia barua walimu wakuu wa skuli za Zanzibar jambo ambalo halikupaswa kutekelezwa kwani vipo vyombo vimewekwa kisheria na taratibu za kufuatwa.

“Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya Tanzania Bara mwenziwe ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Zanzbar, ilitakiwa Katibu Mkuu Bara amuandikie barua rasmi Katibu Mkuu wa Zanzibar kumueleza juu ya mabadiliko yaliyofanyika na sio kuandikiwa walimu wakuu wa skuli juu ya mabadiliko hayo”. Alisema Shamuhuna

Waziri Shamhuna alisema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ina wajumbe wane katika Baraza la mitihani la Tanzania ambao wote hawajui kupitishwa kwa maamuzi hayo ispokuwa walikua wakifuata agizo la Serikali ya Muungano.

Aliwataja wajumbe hao kuwa ni Kamishna Baraza la mitihani, Mkurugenzi elimu ya juu, Mkurugenzi wa Taasisi na lugha za kigeni na mjumbe mwengine kutoka Chuo Kikikuu cha Taifa Zanzíbar (SUZA).

Waziri Shamhuna alisema pamoja na kasoro hiyo iliyojitokeza bila kutegemewa, Wizara hizo mbili za Elimu za Tanzania Bara na Zanzíbar kwa muda mrefu zimekuwa zikifanya kazi kwa mashirikino makubwa na kuleta ufanisi wa hali ya juu.

Share: