Habari

Wananchi Pujini waridhishwa historia ya Mkamandume kurejeshwa

IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WANANCHI wa vijiji vya Pujini Wilaya ya Chake Chake Pemba wamesema, kuimarishwa na kutangazwa kwa sehemu ya kihistoria ya Mkamandume ni chachu ya maendeleo kwa wakaazi wa vijiji hivyo pamoja na nchi nzima kwa ujumla.

Walisema kuwa, zipo fursa mbali mbali za kiuchumi katika makumbusho hayo ambayo yanaweza kuwafanya wananchi wa vijiji hivyo kufaidika na kupata maendeleo wakati wageni wanapoingia kuangalia historia ya Mkamandume.

Wakizungumza mara baada ya kuwasilishwa ripoti ya utafiti wa sehemu ya kihistoria Mkamandume iliyopo Pujini, katika ukumbi wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale walisema kuwa, itakapoboreshwa na kutangazwa, itavutia wageni na wenyeji na kuwa na hamu ya kwenda kuangalia, jambo ambalo litakuza uchumi wao.

“Kwa kweli sehemu ya historia ya Mkamandume inaweza kuleta mabadiliko kwa wananchi kiuchumi, kwani tunafuga samaki, kuna wajasiriamali mbali mbali, hivyo wageni watakapoingia itasaidia sana, kwani hivi sasa tayari kumeanza mabadiliko”, alisema Nassor Rashid Kombo mkaazi wa Pujini.

Kwa upande wake mkaazi Sabahi Seif Said alisema, elimu inahitajika zaidi ili wanajamii waelewe historia, pamoja na kuwapeleka wanafunzi wa skuli mbali mbali katika eneo la Mkamandume ili wajue historia, jambo ambalo litasaidia kuhamasisha wengine kufika katika eneo hilo.

“Ipo haja kwa Serikali kuandaa sinema inayoonesha kumbukumbu ya Mkamandume, pia kuwe na ulinzi mkali katika maeneo hayo, kwa usalama wa wageni wanaoingia katika eneo hilo”, alisema.

Akiwasilisha ripoti ya Utafiti wa sehemu ya historia Mkamandume Pujini, Mratibu wa Makumbusho na Mambo ya Kale Omar Khamis Juma alisema, lengo la utafiti huo ni kukusanya data za eneo hilo la kihistoria pamoja na kuchambua taarifa ya utafiti, kuonesha mapendekezo na maoni ya wananchi katika kuboresha sehemu za historia nchini.

“Matokeo ya utafiti wakati tulipochukua maoni ya wananchi walisema miundombinu isiyorafiki kama vile barabara, maji na umeme inadhoofisha sehemu hiyo ya kihistoria, imani za kiitikadi zinazopelekea watu kuvunjika moyo wa kufanya kazi katika sehemu za kihistoria”, alieleza.

Aidha akiendelea kuelezea matokeo ya utafiti huo alisema ni kuwa, hakuna utaratibu mzuri wa ufuatiliaji, kukosekana kwa mashirikiano baina ya Idara husika na jamii, pamoja na uharibifu unaofanywa na wafugaji, wakulima na wakataji miti”, alisema.

Mapema akifungua mkutano huo Afisa Mdhamini Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale Khatib Juma Mjaja alisema, utafiti huo utasaidia kuwanufaisha wanajamii kuanzisha shughuli mbali mbali za kibiashara, ili kujipatia kipato kitakachowawezesha katika maisha yao ya kila siku.

Utafiti huo ulifanyika kuanzia Novemba 23 mwaka 2018 mpaka Mei 5 mwaka 2019, ambapo jumla ya wananchi 120 walihojiwa wakiwemo wanaume 65 na wanawake 55 kwenye vijiji vya Dodo, Kumvini, Kibaridi, Kijili, Mkamandume, Tondooni na Mtimbu Pujini Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.

MWISHO.

PembaToday

Share: