Habari

Wananchi wanayo haki ya kujilinda usalama wao na mali zao


IMekuwa hali ya kawaida sasa katika nchi yetu kusikia watu wamepotea, hawajulikani walipo au wamechukuliwa katika mazingira ya kutatanisha. Hali hii imeleta mashaka makubwa kwa watu wenye usalama wao, familia na jamaa zao. Wako waliokumbwa na wimbi hili wakibahatika kuonekanwa wako hai. Pia wako waliobahatika angalau kuonekanwa maiti zao. Mbaya zaidi ni kwa wale waliokumbwa na wimbi hili ikiwa hawajulikani chochote kwao wao. Si uzima, si umaiti, wala hawajulikani walipo au wanachofanya.

Jamii sasa inaanza kuzowea hali hii, kuonekana kama ni kitu cha kawaida kupokea taarifa hizo. Huku wengine wakibeza, kukebehi au kufanya tashtiti kama vile jambo la kawaida. Kwao wao hakuna anayepata hisia za utamu wa maisha waliyokuwa nayo nyumbani wala shida na madhila wanayopata huko waliko kusiko julikanwa.

Kwa upande wa serikali chini ya wakala wake Polisi, ambaye anajulikana ndio mlinzi wa usalama wa watu na mali zao wao wakifanya usanii wa mchezo wa kuigiza. Taarifa zinapopelekwa hujisahau wajibu wao wa kuwa ndio walinzi wa maisha ya watu. Nyakati nyengine ndio wao hujigeuza wakawa kinyume chake, badala ya kuwa walinzi wa maisha ya watu huwa nduli wa maisha ya watu. Ni khatari iliyoje jamii kufikia hapo. Mlinzi kujigeuza kuwa ndio nduli.

Ni haki na wajibu kwa wananchi wao wenyewe kujilinda usalama wa maisha yao na mali zao. Hata hizo sheria zilizotungwa hili linalikubali. Kuwa kila raia anayo haki ya kujilinda pale atakapovamiwa kwa lengo la kudhuriwa. Adui anapokukabili hujuwi ana lengo gani, anaweza akakifikia akiwa kama kondoo, kumbe ni chui.

Wakati umefika kwa wananchi kukabiliana na uvamizi wa uadui wowote ule. Hivi iweje mtu akujie nyumbani kwako usiku wa manane bado wewe umezubaa na kumuamini kuwa huyo ni mtu mwema. Wengine wetu tunafahamu sauti za jamaa zetu pia sauti za wageni. Mara mtu anapokwita au kupiga hodi nyumbani kwako nyakati za usiku, maamuzi ya haraka unatakiwa ufanye kazi.

Maendeleo ya teknologia yamebadili maisha yetu. Hata iwe kuna taarifa ya kifo sasa hivi italetwa kwa njia ya simu au ujumbe mfupi wa maneno. Tofauti na zamani mtu kutolewa masawa ya mbali kwa baskeli kuja kukupa taarifa. Tumia simu yako kufahamisha jamaa zako, mara tu usikiapo sauti ngeni inakwita usiku wa manane, au mtu anagonga mlango wako.

Watu pia wamiliki silaha za kujilinda hasa nyakati za usiku. Sio busara kulala usingizi ndani ya nyuma huna panga, shoka, mkuki, na silaha nyengine zozote zile. Kumiliki silaha kutakupa nguvu ya kujilanda na adui wako wakati wa uvamizi. Hasa kwa vile hujuwi kaja kwa dhamira na silaha gani anayo mkononi mwake.

Zama zimebadilika, usalama wa maisha yako yape umuhimu wake. Usisubiri wengine waje wakulinde wakati wao wanaweza kuwa ndio nduli numbar one.

Kwenye hiyo picha Bw Osborn-Brooks wakati akiwa amelala nyumbani kwake alivamiwa na majambazi wawili waliokuwa na silaha. Alikabiliana nao na aliweza kumjeruhi mmoja ambapo majeraha yake yalipelekea kifo chake. Hivyo kushikiliwa na polisi kwa masaa 24 kwa madai ya kuuwa. Hata hivyo Bw Osborn-Brooks ameachiwa kwa dhamana huku polisi ikiendelea kufanya uchunguzi.

Share: